TUWE NA HURUMA WAPENDWA


Harufu nzuri ya Kristo na mwanga wa huruma yake ndiyo tafakari ya tatu iliyotolewa na Baba Mtakatifu Francisko, Alhamisi, tarehe 2 Juni 2016 kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Paulo nje ya kuta za Roma, kama sehemu ya maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu, Wakleri na Majandokasisi, walipopanda kwenda Jangwani ili kusali na kutafakari maisha na utume wao kama Wakleri.
Kwa namna ya pekee, tafakari ya Baba Mtakatifu imejikita katika matendo ya huruma: kiroho na kimwili; umuhimu wa kiti cha huruma ya Mungu, mahali ambapo ukweli unawaweka huru; matendo ya huruma katika mwelekeo wa kijamii, changamoto kwa Wakleri kuwa kweli ni Mwili na Roho ya Kristo katika matendo ya huruma.
Waamini wanapaswa kushiriki kikamilifu katika utekelezaji wa matendo ya huruma, ili kweli Yesu aendelee kutenda miujiza katika maisha watu, kama ilivyokuwa kwa Bartimayo, mwana Timayo kipofu; kwa kusikiliza harufu kali kutoka kwa Yesu Msalabani inayoendelea kusikika katika hospitali zilizoko kwenye uwanja wa vita au katika maeneo ambamo umaskini unaendelea kuwanyanyasa watu, ili wote hawa waweze kugangwa na kuponywa na mafuta ya huruma ya Mungu yanayowafunulia matumaini mapya!
Mtakatifu Rosa wa Lima anasema kuwahudumia maskini na wagonjwa ni kumhudumia Yesu. Kamwe waamini wasishindwe kuwahudumia na kuwasaidia jirani zao kwa sababu ndani yao wanamhudumia na kumsaidia Kristo Yesu. Huduma kwa maskini ni dhamana, utume na kipaumbele cha Kanisa, licha ya udhaifu wake wa kibinadamu, lakini Kanisa limeendelea kutekeleza matendo ya huruma: kiroho na kimwili katika historia ya mwanadamu, kiasi cha watu wa mataifa kumtolea Mungu sifa na utukufu.
Watu wanawapongeza Wakleri wanaojikita katika matendo ya huruma katika shughuli na mikakati yao ya kichungaji; wanasikitishwa sana pale Wakleri wanapogeuka kuwa kama watu wa mshahara kwa kushindwa kumwilisha matendo ya huruma katika shughuli zao za kichungaji. Mwelekeo wa namna hii ni kinyume kabisa cha Kristo, mwaliko kwa Wakleri kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya huduma kwa Watu wa Mungu, ili kweli waweze kuwa ni vyombo na mashuhuda wa huruma ya Mungu inayoleta mageuzi kwa Watu wa Mungu kwa njia ya maadhimisho ya Sakramenti za Kanisa chemchemi ya huruma na upendo wa Mungu kwa waja wake.
Matendo ya huruma ni alama ya uwepo wa Mungu katika historia ya mwanadamu: Mungu anayeshirikiana na binadamu. Wakleri wawe na ujasiri wa kuomba huruma, ili kweli waweze kuwa na huruma wanapokuwa kwenye kiti cha huruma ya Mungu, ili matendo ya huruma yaweze kupata mwelekeo wa kijamii bila kuhukumu kama alivyofanya Yesu kwa yule mwanamke mzinzi kwa kumwonesha uso wa huruma na kumsamehe dhambi zake; kwa kuchukua muda wa kutafakari kabla kuhukumu na kusamehe, ili kumwezesha mwanamke mzinzi kufanya hija ya upendo.
Watu walitaka kumpiga kwa mawe yule mwanamke mzinzi kwani alitenda dhambi ya kijamii. Yesu anajenga mahusiano ya ndani na kumkirimia tena uhuru wa kutembea tena katika upendo kama mtoto wa Mungu. Kiti cha huruma ya Mungu ni mahali ambapo ukweli unawaweka huru Wakleri kwa kukutana na watu wanaokimbilia kiti cha huruma ya Mungu. Padre anapoadhimisha Sakramenti ya Upatanisho, hutekeleza huduma ya Mchungaji mwema anayetafuta kondoo aliyepotea; huduma ya Msamaria mwema anayeponya majeraha na huduma ya Baba mwenye huruma. Kimsingi Padre ni alama na chombo cha huruma ya Mungu kwa wadhambi.
Baba Mtakatifu anaendelea kukazia kwamba Mwungamishaji si bwana, bali mtumishi wa huruma ya Mungu. Mhudumu wa Sakramenti hii lazima ajiunge na nia pamoja na mapendo ya Kristo. Mapadre ni alama na chombo kinachowakutanisha watu na Mwenyezi Mungu mwingi wa huruma na wao wenyewe wanajitambua kwamba, ni wadhambi na kwamba wako mikononi mwa Roho Mtakatifu anayelijenga Kanisa, anayewaunganisha watu na kulipyaisha kila wakati wanapokutana.
Hii ni changamoto ya kushinda kishawishi cha kujitafuta, kwa kuwa tayari kujisadaka  nakuwa ni madaraja yanayokazia mambo msingi ya maisha, tayari kujifunza kutubu na kuambata wongofu wa ndani ili kuanza upya. Wakleri wajifunze kuwa ni waungamishaji bora kwa kuwa wanyenyekevu mbele ya wadhambi wanaosamehewa dhambi zao na Kristo Yesu aliyeguswa na mahangaiko yao ya ndani na kutoa malipizi ya dhambi kadiri ya hali ya mdhambi. Yesu alikuwa anaponya, samehe, fariji, pumzika na kuwaonjesha watu uwepo wa Roho Mtakatifu mfariji.
Huruma ya Mungu iendelee kuboresha maisha ya wahudumu wa Sakramenti ya Upatanisho. Huruma ya Mungu iwawezeshe waungamishaji kujikita katika kanuni ya dhahabu yaani kuhukumu kama ambavyo wao wangependa kuhukumiwa kwa kuheshimu utu wa binadamu kwa kuufunika na joho la huruma ya Mungu.
Baba Mtakatifu anasema, matendo ya huruma yana mwelekeo wa kijamii kwani yanajikita katika huduma ya upendo kwa watu walioumbwa na kukombolewa na Mungu. Anawaalika Wakleri na majandokasisi kutafakari kwa kina Maandiko Matakatifu ili waweze kutambua na hatimaye kumwilisha matendo ya huruma: kiroho na kimwili; mashauri ya Injili, Amri za Mungu, Kusamahe, kufariji na kusahihishana kidugu. Matendo ya huruma hayana kikomo kwani yanaongezeka na kuwaambata wote pasi na ubaguzi kwani kiini cha matendo yote haya ni maisha ya mwanadamu katika ukamilifu wake yaani: kiroho na kimwili.
Mafungo haya ya kiroho katika maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu iwe ni nyenzo ya ujenzi wa utamaduni wa huruma kwa kumtegemea pia Roho Mtakatifu. Yawasaidie kuwa ni watumishi waaminifu wa huruma ya Mungu, kielelezo cha mshikamano na majiundo makini na kumwachia Yesu ili aweze kuwaongoza na kuwafunda.
Wakleri wamwombe Yesu Mchungaji mwema neema ya kuongozwa na utambuzi wa imani “Sensus fidei” na utambuzi wa Kristo “Sensus Christi”: Upendo na imani ambao unaoneshwa na waamini kwa Kristo Yesu. Wamwombe Yesu ili aweze kuwatakasa na kuwaokoa; kuzima kiu ya maisha yao ya ndani na kuwaosha dhambi zao pamoja na kuwafariji watu wao; awahifadhi katika Madonda yake matakatifu, ili daima waweze kuungana na huruma ya Mungu.
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.

Comments

Popular posts from this blog

SALA YA ASUBUHI:SALI HIVI..

Ujio wa Wamisionari wa Kwanza Tanzania Bara (2)

MJUE MTAKATIFU MARIA GORETTI