Papa Francisko: amani Colombia; utashi wa wananchi wa Uingereza!


Baba Mtakatifu Francisko akiwa njiani kuelekea nchini Armenia katika hija yake ya kumi na nne ya kimataifa, Ijumaa tarehe 24 Juni 2016 amepata nafasi ya kuzungumza na waandishi wa habari waliokuwa kwenye msafara wake. Padre Federico Lombardi, Msemaji mkuu wa Vatican akimkaribisha Baba Mtakatifu kuzungumza na waandishi wa habari amesema kwamba, wako 70 na wengine 600 wako nchini Armenia kutoka katika nchi na vyombo mbali mbali wa mawasiliano ya jamii, wanaotaka kuhabarisha jamii kuhusu tukio hili la kihistoria.
Baba Mtakatifu akizungumza na waandishi wa habari amegusia kwa namna ya pekee kuhusu mchakato wa upatanisho na amani nchini Colombia pamoja na Uingereza kuamua kujitoa katika Umoja wa Ulaya, tukio ambalo limeutikisa ulimwengu, huku watu wengi wakipokea uamuzi huu wa wananchi wa Uingereza kwa hisia tofauti. Baba Mtakatufu Francisko anasema, amefurahishwa na habari za kusitisha vita huko nchini Colombia, vita ambayo imedumu kwa takribani miaka 50, kiasi cha kumwaga damu ya watu wasiokuwa na hatia. Ni matumaini ya Baba Mtakatifu kwamba, mchakato huu utaendelea kuimarishwa na kudumishwa, ili hatimaye, Colombia kuondoka kabisa katika hali ya vita na kinzani.
Baba Mtakatifu Francisko anasema, kura ya maoni na hatimaye wananchi wa Uingereza kuamua kujitoa katika umoja wa Ulaya ni kielelezo cha demokrasia na utashi wa wananchi wenyewe, changamoto na mwaliko kwa Jumuiya ya Kimataifa kuhakikisha kwamba, inawasaidia wananchi wa Uingereza kuwajibika kwa ajili ya mafao ya wengi sanjari na mshikamano wa nchi za Ulaya. Haya ndiyo ambayo Baba Mtakatifu Francisko anatumaini kuona yanatekelezwa wakati huu, Uingereza inapoendesha mchakato wa kutoka katika Umoja wa Ulaya.
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.

Comments

Popular posts from this blog

SALA YA ASUBUHI:SALI HIVI..

Ujio wa Wamisionari wa Kwanza Tanzania Bara (2)

MJUE MTAKATIFU MARIA GORETTI