SIFA ZA PADRI BORA
Kardinali Beniamino Stella, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Wakleri anasema, Mapadre wameteuliwa kutoka kati ya watu kwa ajili ya mambo matakatifu na kwa namna ya pekee kabisa ni wahudumu wa Neno na Sakramenti za Kanisa. Katika maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu, Sakramenti ya Upatanisho inapewa kipaumbele cha pekee ili kuwawezesha waamini kuonja huruma na upendo wa Mungu.
Katika Sakramenti ya Upatanisho, Mwenyezi Mungu mwingi wa huruma na mapendo anakutana na binadamu dhaifu, ili kumponya na kumwondolea dhambi zake, tayari kutembea katika mwanga wa maisha mapya. Hii ndiyo dhamana ambayo Mapadre wanapaswa kuitekeleza kwa ari na moyo mkuu, kwa ibada na uchaji; pamoja na kujisadaka bila ya kujibakiza hata kidogo. Wakleri watambue kwamba, kama lilivyo Kanisa hata wao wanapaswa kuendelea kutembea katika mchakato wa kuinjilishwa sanjari na kuyapyaisha maisha yao kwa njia ya malezi na majiundo endelevu na makini.
Hakuna Padre ambaye amekwishafikia utimilifu wa utakatifu wa maisha na kumbe haitaji tena kufundwa na kuundwa upya kila siku ya maisha ili hatimaye, awese kusema, “Mimi hapa Bwana, nitume”. Katika maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa huruma ya Mungu, Wakleri wanahamasishwa kujifunza kutoka katika Moyo Mtakatifu wa Yesu, ili kugundua Uso wa huruma ya Mungu, ili wao pia waweze kutenda kadiri ya mafundisho ya Yesu mchungaji mwema. Mapadre wawe makini sana ili wasimezwe na malimwengu na kujikuta wanakuwa ni watu wa sheria, kanuni na taratibu kiasi cha kushindwa kuguswa na mahangaiko ya waamini wao.
Mapadre wawe ni alama na vyombo vya Injili ya furaha vinavyotumiwa na Roho Mtakatifu, ili kufikiri na kutenda kwa haki, amani na utulivu wa ndani, wakitambua kwamba, kama Upadre ni chombo cha neema, huruma na mapendo ya Mungu kwa waja wake. Ikumbukwe kwamba, huruma ya Mungu inavuka mipaka na vigezo vinavyoweza kutolewa na moyo wa binadamu, hii inapaswa kuwa ni shule endelevu kwa maisha na utume wa Kipadre.
Padre kwa njia ya Sakramenti ya Daraja Takatifu anawekwa wakfu kuwa ni chombo cha huruma ya Mungu, inayomwilishwa katika uhalisia wa maisha yake, licha ya udhaifu na mapungufu ya kibinadamu. Mapadre wanatambua kwamba, wao pia ni wadhambi na wanahitaji kukimbilia huruma ya Mungu mara kwa mara katika Sakramenti ya Upatanisho, ili kwa kuguswa, kuponywa na kusamehewa dhambi zake, awe mwepesi na tayari kuwashirikisha wengine huruma na upendo wa Mungu katika maisha yao.
Kutokana na changamoto zilizopo, Kardinali Beniamino Stella anapenda kufafanua mambo makuu matatu katika maisha na utume wa Kipadre: Upatanisho, mahusiano ya kijamii na mahusiano binafsi. Mama Kanisa anapenda kuwahamasisha Mapadre kutoa kipaumbele cha pekee katika huduma ya Sakramenti ya Upatanisho, kwa kutoa muda na nafasi ya mashauri, ili waamini wanaotubu na kumwongokea Mungu waweze kuonja huruma na upendo wake usiokuwa na mipaka. Mapadre wajenge utamaduni wa kukaa kwenye kiti cha huruma ya Mungu, tayari kuwasikiliza waamini wanaotaka kujipatanisha na Mungu pamoja na jirani zao.
Sakramenti ya Upatanisho ni mahali patakatifu ambapo huruma na upendo wa Mungu unakutana na binadamu mdhambi, anayemgusa, anayemponya na kumwinua mdhambi ili aweze kuendelea mbele na safari ya maisha yake ya kiroho. Hapa Mapadre wawe wanyofu kuwapokea na kuwahudumia waamini wao kwa ari kuu na moyo wa ibada, tayari kuonesha dira na mwongozo mpya wa maisha. Mwenyezi Mungu anaganga na kumponya mdhambi anayetubu na kumwongokea. Kiti cha kitubio kiwe ni mahali pa kuonja huruma na upendo wa Mungu na wala si mahali pa kushambulia na kuwadhalilisha waamini. Mapadre wanapojisadaka kwa kukaa kwenye kiti cha huruma ya Mungu, waamini waoneshe pia ujasiri wa kukimbilia huruma na upendo wa Mungu katika maisha yao, kama ilivyokuwa kwa Mwana mpotevu aliyekua “amekomba vijisenti vya Baba mwenye huruma” kwa kuvinjari na makahaba mjini.
Kardinali Stella anaendelea kufafanua kwamba, kwa njia ya Sakramenti ya Upatanisho, waamini wanaanza maisha mapya, tayari kuambata mafao ya wengi, kwa kuonesha upendo na mshikamano kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya familia ya binadamu. Kumbe, Sakramenti ya Upatanisho licha ya kumwondolea mwamini dhambi zake, pia inampatia neema na baraka zinazomwilishwa katika maisha ya kijamii, kwa kuganga na kuponya mipasuko ya kijamii kwa kuambata mambo msingi ya maisha. Waamini waliotubu vyem, wanapata amani na utulivu wa moyo, tayari kuboresha mahusiano yao na jirani zao.
Mapadre ni watu wanaoweza kuemelewa na magumu ya maisha, kuchoka na hata pengine kukata tamaa. Wawe pia tayari kuwasaidia waamini wao kuondokana na upweke hasi unaoweza kuwatumbukiza katika hali ya kukata na kujikatia tamaa na hapo ni mwanzo wa kukumbatia utamaduni wa kifo. Wawe na ujasiri wa kuponya na hali ya kutaka kulipizana kisasi, ili kuwaelekeza watu njia inayowapeleka kwa Mwenyezi Mungu. Mapadre wanapokuwa na utulivu katika mahusiano yao na jamii inayowazunguka, waweza kuwa kweli ni msaada mkubwa wa huruma na upendo wa Mungu.
Mama Kanisa anawahamasisha Wakleri kutekeleza utume wao katika medani mbali mbali za maisha ya mwanadamu, tayari kutangaza na kushuhudia tunu msingi za maisha ya Injili. Wawe ni wadau wakuu katika mchakato wa utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote. Padre kwa njia ya mfano na ushuhuda wa maisha yake yanayojikita katika mambo msingi, anakuwa ni mfano bora wa Uinjilishaji katika Ekolojia ya binadamu. Padre awe ni mtu wa kiasi, asiyefungwa wala kumezwa sana na malimwengu kiasi cha kusahau dhamana na wajibu wake wa Kikasisi. Awe ni shuhuda wa ufukara kwa ajili ustawi na maendeleo ya familia ya Mungu; kwa kulinda, kutunza na kutumia vyema mali ya Kanisa ambayo amedhaminishwa ili kusaidia mchakato wa Uinjilishaji wa kina unaogusa mahitaji ya mtu mzima: Mapadre wasibinafishe mali ya Kanisa kwa ajili ya mafao yao binafsi
Baba Mtakatifu anawahamasisha Wakleri kuwa kweli ni vyombo muhimu vya kudumisha Ekolojia ya binadamu kwa kusaidia upatikanaji wa maisha bora zaidi kwa watu wanaowahudumia. Wawe mstari wa mbele kupambana na uchafuzi wa mazingira ambao umekuwa ni chanzo kikuu cha maafa kwa watu na mali zao; umaskini na kinzani za kijamii. Chuki, uhasama, vita na ubinafsi ni hatari sana kwa usalama na maendeleo ya wengi. Wakleri wawe mstari wa mbele kusimama kidete kulinda na kutetea haki msingi za binadamu, utu na heshima yake. Waoneshe mshikamano na watu wanaoteseka kwa umaskini, magonjwa, njaa na ujinga, tayari kusikiliza na kujibu kilio chao kadiri ya uwezo wao.
Kardinali Beniamino Stella, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Wakleri anahitimisha mahojiano maalum na Gazeti la L’Osservatore Romano kwa kusema kwamba, mmong’onyoko wa kimaadili na utu wema ni hatari sana katika ustawi na maendeleo ya binadamu. Wakleri wajitahidi kujenga mazingira yatakayosaidia kukoleza na kudumisha tunu msingi za maisha ya kimaadili na utu wema; amani na utulivu; umoja, upendo na udugu; matumaini na imani kwa kutambua kwamba, wote wameumbwa kwa sura na mfano wa Mungu. Ubinafsi, chuki na uhamasa; vita na mipasuko ya kijamii vinachangia kwa kiasi kikubwa uchafuzi wa mazingira anamoishi binadamu.
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.
Comments
Post a Comment