Lindeni na kutunza mazingira nyumba ya wote!
Baba Mtakatifu Francisko, Jumatano tarehe 1 Juni 2016 kabla ta katekesi yake, alikutana na kuzungumza na wawakilishi wa Taasisi ya “Jainology” kutoka London, Uingereza na kuwapongeza kwa kusimama kidete kulinda na kutunza mazingira, zawadi ambayo Mwenyezi Mungu amewakirimia wanadamu, ili waweze kuilinda, kuitunza na kuiendeleza kwa ajili ya mafao ya kizazi cha sasa na kile kijacho. Baba Mtakatifu anasema, mazingira ni taswira ya Mungu Muumbaji na kwamba, mazingira bora ni chanzo cha maisha na taswira ya binadamu wote.
Baba Mtakatifu anaendelea kufafanua kwamba, wengi wao wanapenda kulinda na kutunza mazingira kwani mazingira ni chemchemi ya maisha; mazingira ni nyumba ya wote inayotoa hifadhi kwa binadamu na kwamba mazingira ni dada ya binadamu kwani yanawasaidia katika mchakato wa maisha yao hapa duniani. Kwa masikitiko makubwa Baba Mtakatifu anakaza kusema, binadamu ameshindwa kulinda na kutunza mazingira bora kwa kuwajibika, upendo na amani.
Baba Mtakatifu amewapongeza na kuwashukuru wajumbe wa Taasisi ya “Jainology” kwa kutekeleza dhamana na wajibu wao barabara katika mchakato wa utunzaji bora wa mazingira. Baba Mtakatifu anawataka kuendelea kuungana pamoja na katika utekelezaji wa dhamana hii ya utunzaji bora wa mazingira na kwa njia ya kutunza na kulinda mazingira, dunia pia inasaidia kulinda na kuwatunza binadamu wote.
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.
Comments
Post a Comment