Onesheni unyenyekevu katika sala, ili upendo na huruma ya Mungu iwainue!


Baba Mtakatifu Francisko katika katekesi yake kama sehemu ya mchakato wa maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu, Jumatano tarehe 1 Juni 2016 amewataka waamini kuendelea kusali bila kuchoka na kwamba, wanapaswa kuwa na mwelekeo sahihi wanapokimbilia na kuomba huruma na upendo wa Mungu katika maisha yao, kama inavyojidhihirisha kwenye mfano wa Mfarisayo na mtoza ushuru aliyejinyenyekesha ili kuomba huruma na msamaha kutoka kwa Mwenyezi Mungu. (Rej. Lk. 18: 9- 14).
Hii ni changamoto kwa waamini kutafakari kwa kina na mapana ni mara ngapi wanajitahidi kusali; Jinsi wanavyosali na hatimaye, kuangalia hali halisi ya nyoyo zao! Farisayo katika sala yake anajigamba na kumshukuru Mungu kwa kuwa si kama watu wengine, wanyang’anyi, wadhalimu, wazinzi na watosha ushuru. Farisayo huyu anajiangalia mwenyewe na hivyo kushindwa kuuona ukuu wa Mungu, anajiona amesimama imara na kudhani kwamba, ndiye mkuu wa Hekalu.
Farisayo anaorodhesha matendo ya huruma aliyotenda katika maisha yake kama mtekelezaji mwaminifu wa Sheria; mambo ambayo ni kinyume kabisa cha matendo na maneno ya Mwenyezi Mungu. Farisayo anajiaminisha kuwa ni mtu mwenye haki na kutelekeza amri ya upendo kwa Mungu na jirani. Baba Mtakatifu anawaalika waamini kufanya tafakari ya kina katika nyoyo zao ili kuondokana na kiburi, majivuno na unafiki, tayari kuambata tunu msingi za maisha ya kiroho na ukimya, ili kukutana na Mwenyezi Mungu anayezungumza kutoka katika undani wa moyo wa mtu!
Baba Mtakatifu anawaalika waamini kumwendea Mungu wakiwa na moyo wa unyenyekevu, ili kuomba huruma na upendo wake, tayari kufanya mageuzi na upyaisho wa maisha na mahusiano yake na Mungu pamoja na jirani. Kwani kuwa Farisayo au Mtoza ushuru inategemea jinsi ambavyo mtu anajenga mahusiano yake na Mungu pamoja na jirani zake. Toba na wongofu wa ndani unamwezesha Mtoza ushuru kutambua mapungufu yake ya kibinadamu na hivyo kujikita katika mambo msingi katika sala, kwa kuomba huruma na msamaha wa Mungu. Mtoza ushuru anajifunua mbele ya Mungu akiwa na mikono mitupu na moyo uliovunjika na kupondeka kwa kutambua kwamba, yeye ni mdhambi, kielelezo cha mwamini thabiti. Yesu anahitimisha mfano wa Mfarisayo na Mtoza ushuru kwa kusema kwamba: Mtoza ushuru alirejea nyumbani kwake akiwa amehesabiwa haki kuliko yule Farisayo kwa maana kila ajikwezaye atadhiliwa, naye ajidhiliye atakwezwa.
Unyenyekevu ni hitaji msingi ili kuweza kuinuliwa na Mwenyezi Mungu kutoka katika unyonge wa maisha na dhambi, ili kuonja huruma na upendo wake usiokuwa na mipaka kama alivyofanya Bikira Maria katika utenzi wake wa “Magnificat” kwa kuwa ameutazama unyonge wa mjakazi wake…tokea sasa vizazi vyote wataniita Mwenyeheri na rehema zake hudumu  vizazi hata vizazi kwa hao wanaomcha! Hii ni changamoto ya kujifunza kusali kwa moyo mnyenyekevu kama ilivyokuwa kwa Bikira Maria. Baba Mtakatifu anawatakia waamini wote neema na baraka katika maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu, muda muafaka wa kufanya mageuzi na kupyaisha maisha ya kiroho.
Baba Mtakatifu anawaalika waamini kumwombea na kusali kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya Kanisa la Kristo. Waamini wawe na ujasiri wa kutoka katika ubinafsi wao, tayari kuwaendea jirani zao ili kushuhudia imani katika matendo, kwa kuwafariji na kuwapatia mwanga na matumaini. Amewapongeza waamini kutoka Poland wanaoendelea kuadhimisha Jubilei ya miaka 1050 ya Ukristo nchini mwao na kuendelea kusema, Amina!
Kwa namna ya pekee, Baba Mtakatifu amewataka washiriki wa kozi maalum ya kuwatangaza waamini kuwa wenyeheri na watakatifu, kusaidia kuhamasisha majimboni na mashirikani mwamko na ari mpya ya imani na utume kama sehemu ya mchakato wa kuambata utakatifu wa maisha binafsi. Maadhimisho ya Sherehe ya Moyo Mtakatifu wa Yesu kwa mwaka huu yanatajirishwa na kilele cha maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu kwa Wakleri na Majandokasisi. Baba Mtakatifu amehitimisha Katekesi yake kwa kukumbusha kwamba, Mwezi Juni umetengwa rasmi na Mama Kanisa kwa ajili ya Ibada kwa Moyo Mtakatifu wa Yesu, mwaliko wa kuwaenzi na kuwategemeza Wakleri wao kwa sala na sadaka ili kweli waweze kuwa kama Kristo mwingi wa huruma na mapendo.
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.

Comments

Popular posts from this blog

SALA YA ASUBUHI:SALI HIVI..

Ujio wa Wamisionari wa Kwanza Tanzania Bara (2)

MJUE MTAKATIFU MARIA GORETTI