Wasanii wa mitaani wafunika ile mbaya mjini Vatican!


Maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu kwa wasanii wa mitaani, yamefikia kilele chake, Alhamisi tarehe 16 Juni 2016 kwa wasanii hawa kukutana na Baba Mtakifu Francisko mjini Vatican, ili kumtolea ushuhuda wa kazi na utume wao huko duniani. Baba Mtakatifu amewashukuru wadau mbali mbali waliwezesha kufanikisha maadhimisho haya katika Mwaka wa huruma ya Mungu, kwani wao ni mafundi wa furaha na kile kilicho chema na kizuri; ni mashuhuda wa imani na matumaini kwa watu wengi.
Baba Mtakatifu anasema, tunu hizi msingi katika maisha yao wanazishuhudia wakati wa michezo na maonesho yao mbali mbali, hali inayodhihirisha uwajibikaji, ujasiri na uhodari unaojikita katika uzuri na hivyo kuwapatia watu burudani yenye nidhamu. Sherehe na furaha ni mambo makuu mawili yanayoambata utambulisho, maisha na weledi na kwamba, katika maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu wameamua kushirikisha tunu hizi msingi, ili kuwaonjesha watu upendo na huruma ya Mungu inayomwambata mwanadamu.
Baba Mtakatifu anasema kutokana na kazi zao, wasanii hawa wanaweza kuwa ni Jumuiya za Kikristo zinazosafiri, mashuhuda wa Kristo anayejitaabisha kusafiri ili aweze kukutana na hata wale walio mbali zaidi. Baba Mtakatifu Francisko anawashukuru kwa kuwashirikisha maskini na wale wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii, utajiri wa sanaa zao, kielelezo cha huruma kinachopania kuwaonjesha jirani uzuri na furaha katika ulimwengu huu ambao umegubikwa kwa kiasi kikubwa na giza pamoja na simanzi.
Wasanii wa mitaani ni kati ya watu wanaotoa burudani kwa wote kwa kujenga na kudumisha utamaduni wa watu kukutana katika ujenzi wa mshikamano jamii katika burudani. Hii ni fursa ya kudumisha mchakato wa ujenzi wa umoja na udugu; chachu ya faraja, huruma na upendo kwa wadogo na maskini; kwa kutekeleza matendo haya ya huruma kwa njia ya furaha na kuwasaidia hata watoto kutabasamu na watu kujenga umoja na upendo kati yao.
Baba Mtakatifu anakiri kwamba, anatambua ugumu wa maisha yao kwani daima ni watu wanaozunguka sehemu mbali mbali za dunia kumbe, si rahisi kuwa na makazi ya kudumu, changamoto ya kuhakikisha kwamba, wanajitahidi kuboresha imani yao kwa kupokea Sakramenti za Kanisa; kwa kurithisha upendo wa Mungu kwa watoto na jirani zao pamoja na kutambua kwamba, Kanisa linawajali na kuwathamini na linataka kusaidia kuondokana na maamuzi mbele yanayowasukumizwa pembezoni mwa jamii zao. Anawataka kutekeleza dhamana na wajibu wao kwa furaha, kwa umakini mkubwa, daima wakiwa na imani kwa Mwenyezi Mungu wanayesindikizana naye katika maisha; mashuhuda wa matendo ya huruma kwa kuwa tayari kutoa amana ya usanii na weledi wao kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya wengi.
Katika hotuba yake, Kardinali Antonio Maria VegliĆ², amewatambulisha wasanii hawa kutoka: Amerika ya Kusini, Afrika, Ulaya na Marekani, ambao wamefika mjini Roma ili kumshukuru na kumpongeza Baba Mtakatifu Francisko kwa maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu: Kipindi cha ushuhuda wa imani, sala, tafakari pamoja na kuonja huruma ya Mungu katika maisha yao; tayari kujisadaka kwa ajili ya kumwilisha matendo ya huruma: kiroho na kimwili, kielelezo cha imani tendaji, uso wa huruma ya Mungu. Wasanii hawa ni chemchemi ya faraja, amani, upendo, mshikamano, urafiki na matumaini kwa watu waliokata tamaa. Ni chachu ya majadiliano ya kidini na kiekumene, ingawa pia wanakabiliwa na changamoto kubwa pamoja na ugumu wa maisha ya kuhama hama kila wakati!
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.

Comments

Popular posts from this blog

SALA YA ASUBUHI:SALI HIVI..

Ujio wa Wamisionari wa Kwanza Tanzania Bara (2)

MJUE MTAKATIFU MARIA GORETTI