PAPA HANA SABABU YA KUANZISHA VITA VYA KIDINI


Padre Federico Lombardi msemaji mkuu wa Vatican anakiri kwamba, hija ya kitume ya Baba Mtakatifu Francisko nchini Armenia kuanzia tarehe 24- 26 Juni 2016 imekuwa na mafanikio makubwa na kwamba, ilijikita katika mambo makuu matatu: kwanza kabisa Baba Mtakatifu amepata fursa ya kuweza kukutana na kuzungumza na familia nchini Armenia na kwamba, wananchi wamefurahishwa sana na uwepo wa karibu wa Baba Mtakatifu katika maisha yao. Imekuwa ni nafasi ya kufanya rejea katika utajiri mkubwa unaofumbatwa katika historia ya wananchi wa Armenia na kwamba, sala ya kiekumene ni kati ya matukio makubwa yaliyogusa watu wengi wakati wa hija ya kitume ya Baba Mtakatifu nchini Armenia.
Padre Lombardi anakaza kusema, dhana ya Uekumene, Ukarimu, Umoja na Udugu ni fadhila ambazo zimeshuhudiwa na Patriaki Karekin II katika kipindi cha siku tatu za uwepo wa Baba Mtakatifu Francisko katika makazi yake. Kuna matukio makubwa yaliyopamba hija ya Baba Mtakatifu huko Armenia ambayo yataendelea kukumbukwa na wengi katika mchakato wa kujenga na kudumisha umoja miongoni mwa Wakristo, ushuhuda wa uekumene wa damu na huduma makini kwa familia ya Mungu. Baba Mtakatifu ameweza kushiriki katika Liturujia Takatifu na kuonja utajiri wa maisha ya kiroho unaofumbatwa katika maadhimisho haya.
Hatima ya yote ni tamko la pamoja lililotolewa na Baba Mtakatifu Francisko na Patriaki Karekin II linalowataka Wakristo kushikamana ili kushuhudia na kutangaza Habari Njema ya wokovu kwa watu wa mataifa sanjari na kukabiliana na changamoto mbali mbali zinazojitokeza katika ulimwengu mamboleo! Baba Mtakatifu Francisko katika hotuba zake nyingi amekazia kwa namna ya pekee umuhimu wa Makanisa kuendelea kujikita katika nchakato wa majadiliano ya kiekumene na kidini; ili kuimarisha nia na umoja wa Wakristo, tayari kuanza hija ya kuelekea katika maadhimisho ya Fumbo la Ekaristi Takatifu kwa pamoja.
Padre Lombardi anakiri kwamba, hii ni hatua muhimu sana katika mchakato wa majadiliano ya kiekumene kwa Kanisa la Kitume nchini Armenia. Lakini, ikumbukwe kwamba, waamini wa Kanisa Katoliki ni wachache kwa idadi nchini Armenia, lakini inashiriki kikamilifu katika maisha ya familia ya Mungu nchini Armenia hususan katika huduma kwa maskini na wale wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii, kielelezo cha imani tendaji. Imekuwa ni sherehe kubwa kwa Waarmenia wanaoishi ndani na nje ya Armenia, kumbe, Baba Mtakatifu kati yao amekuwa ni Mhudumu wa Injili ya Kristo na mjumbe wa amani.
Padre Lombardi akijibu shutuma nzito zilizotolewa na Serikali ya Uturuki dhidi ya Baba Mtakatifu Francisko aliyetumia neno la “mauaji ya kimbari” dhidi ya wananchi wa Armenia anasema hapa jambo la msingi ni kwamba, ukweli na nia njema ya Baba Mtakatifu inapaswa kuzingatiwa na kuheshimiwa. Baba Mtakatifu hana sababu ya kuanzisha vita ya kidini, bali ni kutaka Jumuiya ya Kimataifa kutambua mateso na mahangaiko ya wananchi wa Armenia, ili kwa siku za usoni, tunu ya maisha iweze kuheshimiwa na kuthaminiwa na kwamba, utu na haki msingi za binadamu zinapaswa kuzingatiwa. Huu ndio msimamo wa Baba Mtakatifu na Vatican katika ujumla wake.
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.

Comments

Popular posts from this blog

SALA YA ASUBUHI:SALI HIVI..

Ujio wa Wamisionari wa Kwanza Tanzania Bara (2)

MJUE MTAKATIFU MARIA GORETTI