PMS ni kwa ajili ya huduma ya kimisionari kwa Makanisa machanga!


Kardinali Fernando Filoni, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa watu anawataka waamini mahali popote pale walipo kuvuka mipaka ya kufikirika inayotenganisha kati ya utume wa Wakristo katika nchi za Kimissionari na wale walioko kwenye nchi zenye mapokeo ya Kikristo yaliyokomaa, kwani waamini wote wanapaswa sasa kujikita katika mchakato wa Uinjilishaji wa kina unaogusa mahitaji ya mtu mzima kiroho na kimwili sanjari na Uinjilishaji mpya unaofumbata ushuhuda wa maisha ya Kikristo.
Dhamana ya Uinjilishaji inavuka mipaka ya kijiografia ili kuwafikia watu wote wa Mungu mahali walipo. Changamoto hii imetolewa na Kardinali Filoni, Jumatatu tarehe 30 Mei 2016 wakati wa ufunguzi wa mkutano wa mwaka wa Mashirika ya Kipapa ya Kazi za Kimisionari, mkutano ambao unawashirikisha wakurugenzi wa Mashirika haya kutoka sehemu mbali mbali za dunia. Mashirika haya yanapaswa kuwa ni kwa ajili ya huduma kwa Makanisa machanga duniani, ili yaweze kutekeleza dhamana ya Uinjilishaji ambao kwa sasa unakumbana na changamoto nyingi.
Kardinali Filoni amesisitiza Mashirika haya ya Kipapa yanajenga madaraja ya huduma za kimisionari sanjari na kuamsha dhamiri kwa waamini wote kutambua na kuthamini dhamana ya utume katika maisha ya Kanisa. Umoja wa Mashirika ya Kazi za Kimisionari unaadhimisha Jubilei ya Miaka 100 tangu kuanzishwa kwake na wajumbe wa mkutano huu, Siku ya Jumatano tarehe 1 Juni 2016 wametembelea kaburi la Mwenyeheri Padri Paolo Manna muasisi wa Shirika hili.
Maadhimisho yote haya anasema Kardinali Filoni yanapaswa kuwa ni changamoto ya kufanya upyaisho wa utume wa Mashirika haya na kuangalia uwezekano wa kuwa na mwelekeo mpana zaidi, kwa kuyawezesha Makanisa Machanga kuanza kujikita katika mchakato wa kujitegemea kwani mwamko na ari ya kimisionari Barani Ulaya na Marekani unaanza kufifia na hata pengine moto wa Injili unaweza kuzimika kabisa kutokana na changamoto zilizoko katika ulimwengu mamboleo, ndiyo maana Kanisa linaendelea kujielekeza zaidi katika mchakato wa Uinjilishaji mpya.
Kwa upande mwingine anasema Kardinali Filoni, Makanisa machanga yanaendelea kuonesha hofu ya kuweza kujitegemea kwa hali na mali na matokeo yake yanazama katika hofu na ubinafsi. Waamini na wachungaji wao wanateseka sana kuweza kukabiliana na changamoto zinazoendelea kujitokeza katika ulimwengu mamboleo hususan katika masuala ya: kiuchumi, kitamaduni na kidini.
Lakini watambue kwamba, wote hawa wanahamasishwa kutoka huko wanakojificha tayari kujitoa sadaka kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya Makanisa mahalia kwa kutangaza na kushuhudia Injili ya furaha kwa watu walioko pembezoni mwa jamii, huko ambako watu bado wanaelemewa na umaskini, maradhi na ujinga, maadui ambao pia wanakwamisha maendeleo ya mtu mzima: kiroho na kimwili. Ili kufikia malengo ya Uinjilishaji mpya kuna haja kwa Mashirika ya Kipapa kujikita katika majiundo makini ya awali na endelevu, ili kuwafunda waamini na wakleri watakaoweza kusimama kidete kutangaza na kumshuhudia Kristo aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu. Wajumbe wa mkutano huu wanatakiwa kuibua mbinu mkakati utakaoweza kuamsha dhamiri safi ya utume wa Kanisa kati ya Watu wa Mataifa.
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.

Comments

Popular posts from this blog

SALA YA ASUBUHI:SALI HIVI..

Ujio wa Wamisionari wa Kwanza Tanzania Bara (2)

MJUE MTAKATIFU MARIA GORETTI