SHEREHE YA WATAKATIFU PETRO NA PAULO NA FUNZO KWA JAMII
Maadhimisho ya Sherehe ya Watakatifu Petro na Paulo iwe ni fursa ya kuendelea kuimarisha uhusiano, umoja wa Wakristo pamoja kuwanufaisha binadamu wote. Ni nafasi ya kukumbuka ushuhuda wa pamoja uliofanywa na viongozi wa Kanisa la Kiorthodox na Kanisa Katoliki kwa ajili ya wakimbizi na wahamiaji huko Lesvos, nchini Ugiriki. Wote hawa wanahitaji kuhakikishiwa usalama wa maisha yao, amani na utulivu na kwamba, wimbi kubwa la wakimbizi na wahamiaji ni changamoto kubwa kuwahi kutokea baada ya vita kuu ya pili ya dunia.
Kuna watu wengi wanaoendelea kuteseka na kunyanyasika, wengi wao wakiwa ni wale wanaotoka huko Mashariki ya Kati. Ni wajibu wa Makanisa kusikiliza kilio cha wale wanaoteseka na kupondeka moyo; wahanga wa vitendo vya misimamo mikali ya kidini, ubaguzi, dhuluma, ukosefu wa haki jamii, umaskini na baa la njaa duniani. Wote hawa wanapaswa kuoneshwa mwanga wa matumaini katika maisha yao kwa kutambua kwamba, hawa ni binadamu na maisha yao ni matakatifu.
Hii ni sehemu ya barua ya Patriaki Bartolomeo wa kwanza kwa Baba Mtakatifu Francisko wakati huu wa maadhimisho ya Sherehe ya Watakatifu Petro na Paulo, miamba wa imani. Anaendelea kukaza akisema changamoto ya wimbi kubwa la wahamiaji inapaswa kupewa ufumbuzi wa kudumu kwa kuzingatia kanuni ya udugu na haki jamii badala ya Umoja wa Ulaya kuelemewa sana na faida za kiuchumi na utaifa usiojali utamaduni wa mshikamano unaofumbatwa katika maisha ya Kikristo. Maendeleo ya mitandao ya kijamii na ubora wa hali ya maisha ya binadamu vikuzwe na kudumishwa kwa wote.
Patriaki Bartolomeo wa kwanza anasema, Kanisa la Kristo litaendelea kusimama kidete kulinda, kuwatetea binadamu walioumbwa kwa sura na mfano wa Mungu ili kuonesha upendo na mshikamano unaobubujika kutoka katika maadhimisho ya Mafumbo ya Kanisa. Ni wajibu wa waamini kupambana na maovu, ili kweli haki na amani viweze kutawala akili na nyoyo za watu. Makanisa yaendelee kushikamana ili kupambana na changamoto zinazojitokeza katika ulimwengu mamboleo, kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya Kanisa la Kristo na binadamu katika ujumla wao.
Patriaki Bartolomeo wa kwanza anamshukuru na kumpongeza Baba Mtakatifu Francisko kwa kusimama kidete kulinda, kutetea na kutunza mazingira kwa njia ya Waraka wake wa kichungaji juu ya utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote, Laudato si, ili kupambana na uharibifu wa mazingira na kudumisha amri ya upendo kwa Mungu na kwa jirani kwa njia ya utunzaji bora wa ekolojia. Makanisa haya yanapaswa kuendelea kudumisha upendo wa Mungu kwa binadamu, huku wakitekeleza na kushuhudia mfano wa Kristo aliyekuja kuhudumia na wala si kuhudumiwa na kutoa maisha yake ili yaweze kuwa ni fidia ya wengi. Ni matumaini ya Patriaki Bartolomeo wa kwanza kwamba, Makanisa haya yataendeleza mchakato wa majadiliano ya kiekumene ili kufikia umoja kamili kwa kushirikishana mang’amuzi ya kitaalimungu, uzoefu wa kiekumene pamoja na utajiri wa Makanisa haya mawili, ili kuimarisha imani na ukweli kwa Kristo Yesu aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu. Awe ni chachu ya majadiliano ya ukweli na upendo, ili kufikia ukamilifu.
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.
Comments
Post a Comment