Familia ya Mungu Barani Afrika hauna budi kuungana, kushikamana na kushirikiana kwa dhati ili kupambana na balaa la njaa na utapiamlo wa kutisha miongoni mwa watoto unaoendelea kudhalilisha utu na heshima ya binadamu kwa sehemu kubwa ya Bara la Afrika. Hiki ni kiini cha ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisko ulioandikwa kwa niaba yake na Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican, kwenda kwa Rais Alpha Condè, Mwenyekiti wa Umoja wa Afrika wakati huu ambapo, Umoja wa Afrika unafanya kikao chake cha thelathini kwa kushirikiana na Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa, FAO. Baba Mtakatifu anaunga mkono jitihada za utekelezaji wa Azimio la Malabo lililotiwa sahihi kunako mwaka 2014 huko Malabo, Equatorial New Guinea, ambapo Umoja wa Afrika (AU), uliziagiza nchi wanachama kutenga angalau asilimia 10% ya bajeti kwa ajili ya sekta ya kilimo. Mkwamo wa utekelezaji yakinifu wa Azimio la MAPUTO la mwaka 2003 na baadaye MALABO, 2014 katika nchi nyingi za Kiafrika, kumetajwa...