Wizara ya Elimu yatahadharishwa mabadiliko ya mara kwa mara
ASKOFU
wa Kanisa la Anglikan Tanzania, Dayosisi ya Mount Kilimanjaro (DMK), Dk.
Stanley Hotay ameishauri Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kutofanya
mabadiliko ya mara kwa mara katika Sera ya elimu nchini.
Kauli hiyo
ameitoa mjini Moshi hivi karibuni wakati wa Ibada ya kuweka wakfu jina la Shule
ya Bishop Alpha Memorial High School iliyohudhuriwa na mgeni rasmi Naibu Waziri
wa Elimu, Sayansi na Teknolojia William Ole Nasha.
Ibada hiyo
ilifuatiwa na changizo la kuchangia fedha kwa ajili ya ujenzi wa Bwalo la
chakula shuleni hapo ambapo kiasi cha Sh milioni 56.3 zilikusanywa huku Naibu
Waziri Ole Nasha akichangia Sh milioni 8.
Akizungumza
baada ya kumalizika kwa ibada ambayo mahubiri yake yalitolewa na Mkuu wa Mkoa
wa Singida Dk. Rehema Nchimbi, Askofu Dk. Hotay amesema mabadiliko ya mara kwa
mara yamekuwa yakiyumbisha elimu.
“Wizara ya
elimu fikirini kwa upya sera ya elimu mnawezaje kumsaidia mtoto wa Tanzania,
mabadiliko haya ya kila wakati hayamsaidii mwanafunzi,” amesema Askofu Dk.
Hotay.
Kwa upande
wake Naibu Waziri Ole Nasha akizungumza kwenye uzinduzi wa jina jipya la
sekondari hiyo amesema kuwa, serikali inatambua mchango unaotolewa na shule binafsi
na za Taasisi za dini katika maendeleo ya sekya ya elimu.
“Sera ya
elimu na mafunzo ya mwaka 2014 inasema serikali itaweka mazingira bora na
kuhakikisha kuwa sekta ya elimu na mafunzo inatoa rasilimaliwatu ya kutosha na
mahiri ili kukidhi mahitaji ya sekta mbalimbali kwa maendeleo ya taifa.
“Ili kufikia
azma hiyo ushiriki wa wadau wengine kama shule binafsi na taasisi za dini ni
muhimu, hivyo Serikali itaendelea kutoa ushirikiano kwa shule hizi ili ziweze
kufikia malengo ya kuanzishwa kwake,” amesema Naibu Waziri Nasha.
Akifafanua
kuhusu kupanua kwa fursa za elimu nchini, Naibu Waziri Ole Nasha alisema mpango
wa ElimuMsingi bila malipo umewezesha zaidi ya wanafunzi 462,530 kuingia darani
kutoka mwaka 2015 hadi 2017.
“Serikali
inatoa kila mwezi Sh Bilioni 23 kwa ajili ya kutekeleza mpango ElimuMsingi bila
malipo. Na mpango huu umeongeza wanafunzi walioandikishwa darasa la kwanza
kutoka 1,386,592 mwaka 2015 hadi 1,849,122 mwaka 2017,” amesema Naibu Waziri
Nasha.
Aidha serikali
imefanya pia ukarabati na ujenzi wa miundombinu ya shule za msingi na sekondari
kupitia mpango wa lipa kulingana na matokeo (P4R), ikiwa ni pamoja na ukarabati
wa shule zote kongwe 88 nchini.
Kupitia
Ibada hiyo Naibu Waziri Ole Nasha ametolea pia ufafanuzi suala la wazazi na
walezi kuchangia katika maendeleo ya elimu akisema kwamba serikali hajiakataza.
Amesema ni
muhimu kuzingatia maelekezo ya Waraka wa Elimu namba 3 wa mwaka 2016 katika
uchangiaji kwa kuhakikisha kuwa michango yote inaratibiwa na Ofisi ya
Mkurugenzi wa Halmashauri kama ilivyo kwenye michango mingine ya maendeleo.
Wanafunzi
wasifungamanishwe na mchango wa aina yeyote kwa maana ya kumzuia kuhudhuria
masomo au kumnyima cheti kwa kigezo cha mzazi au mlezi kushindwa kuchangia,”
amesisitiza.
Akisoma
taarifa ya shule hiyo Afisa wa uongozi shuleni hapo, Fadhili Chibago aliyataja
malengo ya shule hiyo iliyojulikana awali kama Pasua Sekondari, kuwa ni
kurudisha matumaini mapya kwa wanafunzi waliokosa nafasi za kidato cha kwanza
kwenye shule mbalimbali za serikali.
“Shule yetu
imekuwa ikijitahidi katika ufaulu kitaaluma na ukilinganisha na aina ya
wanafunzi tunawapokea kama shule ya kanisa.
“Mfano mwaka
2015 kidato cha nne shule ilishika nafasi ya 79 katik ya shule 292 kimkoa na
906 kati ya shule 3,452 kitaifa. Pia jumla ya wanafunzi 23 walichaguliwa kwenda
kidato cha tano kati ya wanafunzi 70 waliofaulu,” alisema Chibago.
Awali Mkuu
wa Mkoa Dk. Nchimbi alisema kuwa Kanisa
la Anglika kumiliki na kuendesha shule hiyo ni moja ya dhamana kubwa waliyokabidhiwa
ya kuandaa taifa lijalo.
“Elimu
inayotolewa hapa itawapatia vijana wetu uelewa mpana wa kuelewa dunia
inakwendaje wao kuwa na uhakika wa kuishi mahali popote,’ amesema Dk. Nchimbi.
Comments
Post a Comment