Pinda aongoza harambee ya ujenzi wa kituo cha hija Ifucha
Waziri Mkuu Mstaafu
Mizengo Pinda amewahimiza waamini wa
Jimbo Kuu Katoliki Tabora na wenyenji wa Kijiji cha Ifucha Nholo Tabora kutunza
uoto wa asili na Mazingira ili kuenzi kazi ya Uumbaji wa Mwenyezi Mungu.
|
Rai hiyo ameitoa hivi
karibuni alipotembelea eneo la Ifucha Tabora mahali ambapo Jimbo Kuu Katoliki
Tabora linaendelea na ujenzi wa kituo cha Huruma ya Mungu .
Mh. Pinda alipokea
taarifa iliyotolewa na Padri Mhandisi wa Jimbo Kuu Gosbert Kalaso iliyosema
kuwa kituo hicho kutagharimu kiasi cha fedha kisichopungua shilingi milioni 717
za kitanzania.
Aidha Padri Kalaso
amesema hadi ujenzi wa kituo ulipofikia , kituo kimeshagharimu shilingi milioni
sitini na nne, laki mbili na ishirini na tano (64,225,000).
Baada ya kupokea maelezo
hayo, Mh. Pinda aliwatoa hofu wanatabora hao na kusema kituo kitakamilika kwa
wakati na akapendekeza mikakati iwekwe ikiwemo kuandaa na kupanga siku maaalumu
ili kufanya harambee itakayoshirikisha watu ndani na nje ya mkoa wa Tabora.
Akielezea lengo la kituo
hicho, Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki Tabora, Mhashamu Paul Ruzoka amesema
kuwa, kituo hicho ni kwa ajili ya kupata eneo la kupata utulivu wa moyo kama
jina lilivyo yaani “Ifucha nholo” watu watapata sehemu wanayoweza kusikia na
kusikiliza sauti ya Mungu.
Sanjari na ujenzi wa
kituo hicho cha kiroho, Jimbo Kuu Tabora limesaidia wenyeji wa eneo hilo kwa
kuwagawia wanakijiji mbegu ya kisasa ya mihogo inayokinzana na magonjwa na
kuvumilia hali ya hewa jambo lilisababisha
mbegu hiyo kuitwa,”Mkombozi.”
Aidha jimbo pia
limesaidia kutoa elimu ya kilimo na
ufugaji kwa kaya zisizopungua 120, kwa kutumia kiasi cha milioni 400 pesa za
kitanzania.
Jimbo Kuu Tabora
limeanzisha kilimo cha korosho ili kuwasaidia wanatabora kubadili fikra na
kuanzisha kilimo hicho cha biashara.
Jimbo pia limepanda miti
ili kuwa kielelezo cha utunzaji mazingira na kuhamasisha wananchi kuotesha miti
na kuchana na tabia mbaya ya kukata miti hovyo.
Akizungumza kwa niaba ya
Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Mkuu wa Wilaya
ya Tabora mjini Mwl. Queen Mlozi alitanabaisha fursa zinazopatikana
mkoani hapo ambazo kila mwanatabora anapaswa kuzichangamkia kwa wakati
yaani; ujenzi wa reli ya kisasa, uhakika
wa usafiri wa ndege, ujio wa maji toka ziwa Victoria, ujenzi wa barabara za
lami unaoendelea ili kuufungua mkoa wa Tabora na mikoa mingine jirani na uwepo
wa makao makuu ya Serikali hapo Dodoma.
Katika hafla hiyo fupi,
Mh. Pinda aliendesha harambee na kupata
kiasi cha shilingi milioni 12,920,000 zikiwa ahadi na pesa taslimu.
Pia ameomba utaratibu
ufanyike haraka ili harambee nyingine ifanyike mwaka huu (2018) ili Kanisa la
Tanzania litakapo adhimisha Kongamano la Ekaristi Takatifu kitaifa 2020 kituo
kiwe katika hatua nzuri.
Jimbo kuu Tabora
linatarajia kujenga shule, zahanati, kumbi za mikutano, nyumba ya kulala wageni
na nyumba ya utulivu au “rehabilitation centre.”
Comments
Post a Comment