Mwenyeheri Paulo VI & Oscar Romero kutangazwa watakatifu mwaka huu
Baba Mtakatifu Francisko hivi karibuni baada ya kukutana na kuzungumza na Kardinali Angelo Amato, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Kuwatangaza Waamini kuwa wenyeheri na watakatifu ameridhia kwamba, Papa Giovanni Battista Montini, maarufu kama Mwenyeheri Paulo VI, aliyetangazwa kuwa Mwenyeheri tarehe 19 Oktoba 2014 wakati wa maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu kuhusu familia, atangazwe kuwa Mtakatifu katika kipindi cha Mwaka 2018, Mama Kanisa anapoendelea kujizatiti katika kukuza na kudumisha tunu msingi za maisha ya familia, zinazofumbata Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo! Mwenyeheri Paulo VI alizaliwa tarehe 26 Septemba 1897 na kufariki dunia tarehe 6 Agosti 1978 kwenye Ikulu ndogo enzi hizo ya Castel Gandolfo, nje kidogo ya mji wa Roma.
Mwenyeheri Askofu mkuu Oscar Arnulfo Romero Galdamez, aliyezaliwa tarehe 15 Agosti 1917, huko El Salvador na kuuwawa kikatili kutokana na chuki za kidini kunako mwaka 1980. Alikuwa ni mchungaji mwema aliyejitahidi kujenga na kudumisha amani kwa nguvu ya upendo, kashuhudia imani kwa Kristo na Kanisa lake kiasi hata cha kuyamimina maisha yake. Mwenyezi Mungu anaendelea kuwakumbuka watu wake na kwa sasa Baba Mtakatifu Francisko ameridhia kwamba, atangazwe kuwa Mtakatifu hasa kutokana na ushuhuda wake wa kuwalinda, kuwatetea na kuwahudimia maskini na wale wote waliokuwa wanasukumizwa pembezoni mwa jamii, kiasi hata utu na heshima yao kama binadamu vikawekwa rehani. Mwenyeheri Romero alitekeleza dhamana na wajibu wake wa kufundisha, kuongoza na kuwatakatifuza watu wa Mungu kama Askofu, mintarafu Mafundisho ya Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican.
Baba Mtakatifu pia ameridhia miujiza iliyotendwa na Mwenyeheri Vincenzo Romano, Padre wa Jimbo nchini Italia, aliyezaliwa kunako mwaka 1751 na kufariki dunia, tarehe 20 Desemba 1831. Katika orodha hii, wamo pia: Mwenyeheri Francesco Spinelli, Padre wa Jimbo na muasisi wa Shirika la Masista Waabuduo Ekaristi Takatifu, aliyezaliwa kunako mwaka 1853 na kufariki dunia mwaka 1913. Mwenyeheri Maria Katharina Kasper, muasisi wa Shirika la Watawa fukara wa Yesu, alizaliwa mwaka 1820 huko Ujerumani na kufariki dunia mwaka 1898.
Mama Kanisa pia ametambua na kuridhia muujiza uliotendwa kwa maombezi ya Mtumishi wa Mungu God Maria Felicia wa Yesu wa Ekaristi Takatifu, Mtawa aliyezaliwa mwaka 1925 na kufariki dunia mwaka 1959. Kanisa limetambua ushuhuda wa Mtumishi wa Mungu Bernardo Lubienski, Mtawa kutoka Poland aliyezaliwa mwaka 1846 na kufariki dunia mwaka 1933. Mtumishi wa Mungu Cecilio Maria Cortinovis; mtawa kutoka Italia alizaliwa mwaka 1885 na kufariki dunia mwaka 1984. Wengine ni Mtumishi wa Mungu Giustina Schiapparoli, muasisi wa Shirika la Kitawa aliyezaliwa Italia mwaka 1819 na kufariki dunia mwaka 1877.
Mtumishi wa Mungu Maria Schiapparoli, muasisi wa Shirika la kitawa aliyezaliwa mwaka 1815 na kufariki dunia mwaka 1882. Kanisa limetambua fadhila ya kishujaa iliyoshuhudiwa na Mtumishi wa Mungu Antonella Bordon, mwamini mlei na muasisi wa udgu wa masista wadogo wa Mama wa Mungu, aliyezaliwa mwaka 1916 na kufariki dunia mwaka 1978. Mwishoni katika orodha hii yumo Mtumishi wa Mungu Alessandra Sabattini, mwamini mlei kutoka Italia, aliyezaliwa kunako mwaka 1961 na kufariki dunia mwaka 1984.
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.
Vatican News!
Comments
Post a Comment