Wanaoichafua nchi watajwa

Na Pascal Mwanache, Musoma
WATU wanaoshuhudia bila kuchukua hatua au kushiriki katika vitendo vinavyoondoa uhai wa binadamu kwa sababu za kisiasa au kijamii wametajwa kuwa wachafuzi wa amani na ustawi wa Tanzania, huku wananchi wakitakiwa kuungana na kukemea maovu hayo.
Wito huo umetolewa na Paroko wa Parokia ya Maria Mama wa Mungu Musoma Padri Benedikti Luzangi katika Misa Takatifu ya Dominika ya Pili ya Kwaresima, ambapo amesema kuwa Mungu anachukizwa na vitendo vya mauaji na hivyo kuwaomba waamini kusali daima ili yeye aliepushe Taifa dhidi ya chuki, hasira na visasi vinavyozidi kushamiri nchini.
“Nyakati hizi pamekuwa na vitisho vikubwa dhidi ya uhai. Nyakati hizi pamekuwa na mauaji ya kutisha na kuondokewa na amani katika nchi yetu. Tumesikia watu wanauana wengine kwa sababu za kisiasa, watu wengine wanauana kwa sababu za kijamii tu kama kugombea mipaka ya mashamba. Mungu kwa kumzuia Abrahamu asimtoe Isaka sadaka amekataa mauaji, anachukizwa na dhambi ya kutoa uhai” ameeleza Padri Luzangi.
Aidha amesema kuwa vitendo hivi ni matokeo ya mwanadamu kutokuwa tayari kusikiliza sauti ya Mungu na badala yake kwa ubinafsi wa binadamu wamejimilikisha mamlaka ya kuondoa haki ya uhai wa wengine na kuwanyima haki ya kuishi.
“Dhambi hii mbaya kabisa ambayo iliasisiwa na Kaini aliyeondoa uhai wa ndugu yake ina adhabu kali kama vile Mungu alivyompa adhabu Kaini. Tendo hili linapaswa kukemewa na wengi. Ninyi ni mashahidi kwa kusikia, kuona au kushiriki katika mambo haya yanayotoa uhai” ameeleza.
Pia Padri Luzangi amewaasa waamini kutumia kipindi hiki cha kwaresima kutathmini mchango wao kwa watu wenye mahitaji ambao wanaishi nao katika familia, jumuiya na jamii, huku akiwataka kuwatendea matendo ya huruma.


Comments

  1. TUMSIFU Yesu Kristu...kwenye Sala za asbui..Sala ya kutubu imekosewa "mwenye"

    ReplyDelete

Post a Comment

Popular posts from this blog

SALA YA ASUBUHI:SALI HIVI..

Ujio wa Wamisionari wa Kwanza Tanzania Bara (2)

HISTORIA YA SHEREHE YA MOYO MTAKATIFU WA YESU