Kanisa halitaacha kukemea uovu bila woga

Na Silvanus Kayanda
KADIRI nyakati zinavyobadilika matatizo ya jumuiya hubadilika pia. Hata hivyo kanuni kuu za kuondoa matatizo hubakia zile zile kama zilivyotumiwa zamani. Ni vizuri basi zitumike katika mazingira ya siku hizi.
Yapo matatizo yaliyotokea zamani na jinsi wakuu wa Kanisa walivyotoa ufumbuzi wa matatizo hayo, ni hivyo hivyo inavyopasa kuwa katika kutoa ufumbuzi wa matatizo yanayojitokeza sasa tukitumia kanuni kuu.

Ipo mifano kadhaa hapa:
1. Nyakati za Papa Leo XII (Rerum Novarum, Mei 1891)
Tatizo lilikuwa hili: wafanyakazi walikuwa wamekandamizwa sana na matajiri wao, wakawa fukara kweli. Mishahara haikuwa yenye kutosheleza, pia watu walifukuzwa ovyo ovyo kazini, kwa hiyo kukawa na ukosefu mkubwa wa kazi. Matokea yake yakawa kuvunjika kwa familia nyingi. Ilikuwa marufuku wafanyakazi kuunda umoja na kufanya mgomo au maandamano ya aina yoyote.
Urasilimali (Capitalism) haukujali sheria ya wema na ubaya au haki ya wafanyakazi, ulitawaliwa na mashindano matupu. Kanuni ya wenye nguvu ndiyo iliyotawala, yaani “ Mwenye nguvu Mpishe”. Kadiri ya mawazo ya Leo XII ili kuondoa tatizo hilo, alianza kwa kukanusha kabisa uonevu huo wa matajiri uliokuwa umekithiri, akisema: “kazi ya mtu si kwa ajili ya faida tu, bali ikumbukwe kwamba cheo cha binadamu ni msingi”, yaani haki zake ni wakfu, si za kuchezea chezea ovyo.
Akasema kwamba “mali ya mtu binafsi ni haki yake ya asili ambayo serikali au tajiri yeyote hawezi kuinyang’anya”. Kwamba haki ya umoja ipo, kwa hiyo wafanyakazi wanayo haki ya kuunda vyama vya ushirika. Kwamba kazi ya Serikali ni kulinda haki za raia wake na kuangalia kwamba mapatano ya kazi ni ya haki kwao.

2. Nyakati za Papa Pio XI miaka 40 baadaye (Quadragesimo Anno, Mei, 1931).
Tatizo lilikuwa hili kwamba ingawa sasa hali ya mishahara ilikuwa nafuu, nguvu ya wenye rasilimali ilizidi mno. Hapo Serikali ikanuia kuchukua rasilimali yote ili iwe mikononi mwake. Mabwana wa kazi walikuwa wamebadilika ingawa bado uwezo mkubwa ulikuwa mikononi mwa wachache, kila mtu au jamii ndogo ndogo zilikuwa bado zikitawaliwa na wale wachache wenye mali, na wala watu hawakupata uhuru wa kutosha wa kuangalia maendeleo yao wenyewe.
Kadiri ya mawazo ya Papa Pio XI ili kuondoa tatizo hilo, alianza kwa kukaza kwamba watu wana haki ya kujifanyia ushirika au vyama vyao vidogo vidogo vya ufundi na vya uchumi, wala si lazima hayo yafanywe kila mara na serikali. Akasisitiza kwamba wafanyakazi lazima washiriki katika kumiliki hata vyombo vya kuleta uchumi tena mishahara isipimwe kadiri ya mapato tu, bali pia ni sharti kuangalia mahitaji ya wafanyakazi na wajibu zao za nyumbani yaani kuangalia familia. Papa pia aliweka msisitizo juu ya haki ya msingi ya ushirika.

3. Nyakati za Pio XII, yapata miaka 10 baadaye ( Pentekoste 1941) Papa Pio XII naye alitoa hotuba Siku ya Pentekoste, 1941 kuwaambia wale waliotoa malalamiko kwamba hawangependelea Kanisa kusema neno lolote kuhusu mambo ya kimwili.
Hata leo hii Kanisa linapojitahidi kukemea maovu yanayotendeka na matatizo mengine yanayowakumba watu katika nchi mbalimbali bado wapo wanaoendelea kunung’unika wakiulizana ni kwa nini Kanisa nalo lipate nafasi ya kusema juu ya haki za mwanadamu na mambo ya kimwili!
Ni haki kabisa isiyo na upinzani wa aina yoyote ile ya Kanisa kufikia hatua ya kusema kwamba njia hii au hiyo kuhusu matatizo ya maisha ya watu ni sawa au si sawa, haipingani na Amri ya Mungu ya kumtunza mwanadamu kimwili na kiroho.
Papa Pio XII, pia alisisitiza kuwa: Juu ya mali ni haki ya mtu ya kutumia mali ili apate kuishi, inatangulia hata haki ya kuwa na mali. Kwa hiyo mtu ana haki ya kujipatia shamba au kutafuta kazi ili apate jinsi ya kuishi. Tena juu ya kazi, ni wajibu na haki kabisa ya kila mwanadamu.
Watu wenyewe inawapasa kutengeneza hali za kazi. Serikali inaweza tu kujiingiza kufanya hivyo ikiwa watu wenyewe wanashindwa kufanya mambo hayo vizuri zaidi. Na juu ya maisha ya familia ni kweli kabisa kwamba mali ya kila mtu binafsi ndiyo inayosaidia kulinda, kuitunza na kuilisha familia. Kwa hiyo ni haki ya asili kabisa mtu kuwa na mali yake binafsi.

4. Tukija nyakati zetu hizi, kwa upande wa elimu tunaona katika elimu ya sayansi mambo yamebadilika sana kadiri miaka inavyozidi kuendelea mbele. Kwa mfano elimu ya sayansi inaendelea kuleta nguvu ya atomiki, mitambo ifanyayo kazi yenyewe katika viwanda, ushindi wa anga, teknolojia mbalimbali n.k. kwa upande wa Jumuiya, katika mambo yanayohusu jumuiya tayari imetokea mipango mingi kabisa ihusuyo usalama, elimu imezidi, vifaa na maisha ya anasa zaidi yanazidi kuongezeka, tena hamu kubwa zaidi ya kujua mambo ya ulimwengu inazidi kujitokeza sana kwa kutumia Teknolojia Hama.
Hata hivyo kwa upande mwingine lakini matokeo yake ni kuleta kasoro za kuonyesha kuwa hakuna mizani iliyo sawa kati ya maendeleo ya ukulima na maendeleo ya viwanda. Maendeleo ya kilimo yako nyuma sana ingawaje tunasisitiza kwamba katika maendeleo yetu tujali “KILIMO KWANZA” hata kuliko yale ya viwanda. Hii ni hatari kweli.
Inaonekana hakuna uwiano ama mizani sawa kati ya maendeleo ya ustawi wa mikoa ya nchi ile ile, ipo tofauti kubwa. Bila kusahahu kwamba nchi nyingine ni tajiri mno na nyingine ni masikini mno. Kweli ufa huu mkubwa ni wa hatari.
Nikirudi kwenye upande wa Siasa nako ni kivumbi na jasho, mabadiliko mazuri ni kuwa mahali pengi sasa yaani, duniani raia wanachukua sehemu kubwa zaidi katika maisha ya kiserikali mwamko ni mkubwa na watu sasa wanayo sauti zaidi ukoloni umekwisha.
Watu sasa wanahitajiana, mara kwa mara hutokea mikutano ya kidunia ili kuweza kujishughulisha na mambo yanayoleta faida kwa watu wote. Kwa hiyo viongozi wa Kanisa wanapotoa ujumbe kwa njia ya mikutano mbalimbali ama kwa maandishi ni kutaka kumkomboa mwanadamu kimwili na kiroho kutokana na matatizo kadha wa kadha yanayokuwa yanajitokeza katika maisha yake ya kila siku.
Kanisa halipaswi kukaa kimya. Kanisa likifanya hivyo kwa kuwatumia viongozi wake litakuwa linatimiza wajibu wake kama Yesu alivyoagiza. Ni wajibu wa viongozi hao kukazia sana mafundisho ya watangulizi wao. Tena hii ni kuonesha wazi kwamba Kanisa linafikiri na kusema nini juu ya matatizo mapya yanayoendelea kujitokeza katika siku hizi tulizomo, likiwa ni Mama na Mwalimu wa nyakati zote kadiri Yesu alivyoliweka na kuliagiza lifanye.
Nao viongozi wa serikali hawana budi kujitahidi kuungana nao ili kuponya matatizo katika maisha ya watu wa karne hii tuliyomo. Kuponya matatizo hayo ni pamoja na kuona ni jinsi gani tunaweza kusawazisha mapato ya mabadiliko inavyofaa zaidi kwa mahitaji ya binadamu. Watu wasiangalie sehemu moja tu ya hali ya kibinadamu, na kusahau kuangalia pia upande wa watu kwa wajibu zake za kidini.
Kwani hapawezi kuwa na amani au haki duniani kama watu wanaharibu cheo walichopewa na Mungu. Mwanadamu akijitenga na Mungu, anakuwa kioja, si kwake tu, bali na kwa binadamu wenzake. Tukumbuke kuwa: Ukweli ni kiongozi, haki ni shabaha na mapendo ni nguvu iendeshayo maisha mazima ya mwanadamu katika jumuiya.

Mwandishi ni Padri wa
Parokia ya MUHINDA,
Jimbo Katoliki Kigoma,
P.o.Box 71 KIGOMA.


Comments

Popular posts from this blog

SALA YA ASUBUHI:SALI HIVI..

Ujio wa Wamisionari wa Kwanza Tanzania Bara (2)

HISTORIA YA SHEREHE YA MOYO MTAKATIFU WA YESU