Vijana ni utajiri wa Kanisa-Padri asisitiza
Vijana ndiyo utajiri wa Kanisa hivyo wajitume kulitegemeza Kanisa
hasa kuiishi miito mitakatifu.
Vijana Wakatoliki
wametakiwa kuitikia miito mitakatifu wanayoitiwa na Mungu kwani Kanisa bado
lina mahitaji makubwa katika kuitangaza Injili.
Aidha wametakiwa
kuepuka tamaa za dunia ambazo zinawapumbaza na kukataa kuitikia sauti ya Mungu,
badala yake kuomba ushauri kwa Mapadri na maaskofu ili kupata msaada wa kufikia
safari yao ya miito.
Hayo yamesemwa na
Mkurugenzi wa Miito wa Shirika la Mateso ya Yesu (PASSIONIST FATHERS) Padri
Erasto Kamugisha alipokuwa akizungumza na Gazeti Kiongozi katika mahojiano maalumu kuhusu changamoto ya miito
ya Upadri kwa vijana katika karne hii.
Padri Kamugisha
amesema kuwa, Vijana wanaitwa na Mungu na wengi wana wito wa Upadri lakini wapo wanaopata vikwazo kufikia safari
yao kutokana na mazingira wanayoishi.
Hao wasipokuwa na
msaada ama kukosa nidhamu ya kiimani hawawezi kujiunga na seminari ama hata
wakijiunga na seminari wataacha katikati.
“Kanisa bado
linahitaji watenda kazi ,ni maamuzi ya Vijana kukubali wito wa Upadri waliotiwa
na Mungu na jambo kubwa wajikite katika sala na kuomba ushauri kwani hata mimi
nilisaidiwa katika kufikia wito wangu,” amesema Padri huyo.
Kuhusu changamoto
zinazowakabili Vijana Padri Kamugisha amefafanua kuwa Jimbo kuu Katoliki Dodoma
kupitia Shirika la Mapdari wa Mateso ya Yesu limeendelea kuwasaidia Vijana kwa
kuwapa elimu ya kujitambua na kuachana na mambo ya kishetani kama vile matumizi
ya dawa za kulevya, uasherati na mambo mengine ambayo ni dhambi kwa Mungu.
Amesema, wamekuwa wakiandaa makongamano mbalimbali ya
vijana na kuwafundisha Ujasiriamali,lengo likiwa ni kuwapa ufahamu Vijana
katika kukabiliana na tatizo la ukosefu wa ajira.
“Mpaka sasa
Vijana zaidi ya 200 walikuja katika semina ambayo tuliiandaa na tumeona matokeo
kwani wengi wao mara baada ya semina hiyo walionesha mabadiliko na wengine
kuanza kuonesha nia ya kupenda miito ya upadri na utawa na wengine kuachana na
mazingira waliyokuwa wakiishi zamani,” amesema.
Amewasihi Vijana
kuendelea kutambua thamani yao ndani ya Kanisa na taifa kwa ujumla na kujituma
katika kufanikisha malengo yao ili Kanisa na jamii iweze kunufaika na mchango
wao kwa siku za baadae.
Pia amewataka Mapadri na Watawa wa kike na kiume kuendelea kuwalea na
kuwatia moyo Vijana wanapowafuata kuomba
ushauri pale wanapokumbana na vikwazo ili wawe imara na kuendelea na safari yao
ya wito.
Comments
Post a Comment