‘Kiongozi mwadilifu na mchaMungu aepuke ubinafsi na chuki’
WAZIRI
Mkuu Mstaafu Mizengo Pinda amesema kuwa viongozi wanatakiwa kuwa waadilifu na
wacha Mungu badala ya kufanya kazi kwa ubinafsi, chuki na kula rushwa. Ametoa
kauli hiyo alipokuwa akifunga Kongamano la Maombi ya kuliombea taifa pamoja na
viongozi lililofanyika mjini Dodoma.
|
Pinda amesema kuwa ili
uweze kuwa na taifa lenye viongozi wazuri wasiojihusisha katika vitendo vya
rushwa na kuwa na utawala bora ni lazima kupata viongozi ambao ni wacha Mungu
na wenye hofu ya kimungu.
Amesema kuwa viongozi
wote ndani ya serikali, kwenye vyama vya siasa pamoja na kwenye taasisi
mbalimbali lazima wafanye kazi zao kwa hofu ya Mungu kutoka moyoni na siyo
maigizo, ili kuweza kuwapatia wananchi maendeleo.
“Maombi ambayo yamekuwa
yakifanyika kwa ajili ya kuliombea taifa pamoja na viongozi mbalimbali yawe
chachu ya kuwaletea maendeleo wananchi na viongozi wanatakiwa kutambua wazi
kuwa ili nchi iweze kuwa na maendeleo ni lazima kuwepo na utawala bora. Kama
viongozi watafanya kazi zao kwa uadilifu ni wazi kuwa kila Mtanzania ataweza
kujivunia na kujiongezea kipato kutokana na rasilima zinazotokana na vyanzo
mbalimbali ambavyo Mungu ameviweka katika nchi yetu” amesema Pinda.
Mbali na hayo Pinda
ameongeza kuwa kuna haja ya kuanzishwa kwa vikundi vya maombi kuanzia ngazi ya
shule za msingi hadi vyuo vikuu ili kuwekeza njia bora ambayo watoto watakiwa
waaminifu katika utendaji wao wa kazi kwa misingi ya kujitenga na ufisadi,
rushwa pamoja na wizi wa mali ya umma.
Kwa upande wake aliyekuwa
Makamu Rais wa Benki ya Dunia Kanda ya Afrika, Dk.Oby Ezekwesili kutoka nchini
Nigeria akitoa mada katika kongamano la maombi juu ya utawala bora, uwazi na
uwajibikaji amesema kuwa ili nchi iweze kusonga mbele ni lazima kuwa na
viongozi ambao wanazingatia misingi ya utawala bora.
Mbali na kuwepo kwa
utawala bora pia Dk. Ezekwesili amehimiza uongozi ambao unazingatia masuala ya
utekelezaji wa demokrasia, uwazi, uwajibikaji pamoja na utawala bora ili kila
mmoja aweze kujivunia rasilimali za nchi.
Katika hatua nyingine
kiongozi huyo amehimiza utoaji wa elimu juu ya kutunza maliasili za nchi huku
suala zima la uzalishaji likipewa kipaumbele kwa njia ya kutunza vyanzo vyote
vya mapato ikiwa ni pamoja na kujiepusha na masuala ya rushwa, ufisadi na
ubadhirifu wa mali ya umma.
Comments
Post a Comment