Trilioni 1 kulipa madeni 2017/2018
SERIKALI imetenga jumla ya shilingi Trilioni 1 kwa mwaka wa
fedha 2017/2018 kwa ajili ya kulipa madeni mbalimbali ya watoa huduma, wazabuni
na watumishi wa Umma.
|
Mkurugenzi wa Idara ya Habari (MAELEZO) Dkt. Hassan Abbasi ameeleza hayo
Mjini Dodoma alipokuwa akiongea na waandishi wa habari juu ya utekelezaji wa
miradi na ahadi mbalimbali za Serikali.
“Kati ya shilingi Trilioni 1 zilizotengwa kulipia madeni kwa mwaka huu
wa fedha, shilingi Bilioni 896.3 zimeshalipwa kwa watoa huduma, wazabuni na
watumishi wa Serikali,” amesema Dkt. Abbasi.
Amesema hesabu hiyo inajumuisha shilingi Bilioni 43 ambazo zimelipwa
Februari, 2018 ikiwa ni malimbikizo ya wafanyakazi wa sekta ya Umma. “Madeni mengine uhakiki
unaendelea na yataendelea kulipwa siku zijazo na tutawajulisha,” amefafanua
Dkt. Abbasi.
Vile vile amesema kuwa Serikali ina mkakati wa kuwaondoleaa adha ya
usafiri wananchi wa maziwa makuu likiwemo Ziwa Nyasa, Tanganyika na Viktoria
ambapo kwa upande wa Ziwa Viktoria,
mkandarasi amepatikana na majadiliano ya mwisho na kusaini mkataba na
kampuni ya STX ya Jamhuri ya Korea vitafanyika mwezi huu kwa ajili utengenezaji
wa meli mpya itakayokuwa na uwezo wa kubeba abiria 1,200 na mizigo tani 400.
Kwa upande wa Ziwa Tanganyika zabuni kwa ajili ya utengenezaji wa meli
mpya ya abiria na mizigo itatangazwa mwezi huu. Meli hiyo mpya itakuwa na uwezo
wa kubeba abiria 600 na tani 400 za mizigo na italeta mapinduzi makubwa katika
usafiri ziwani hilo.
Aidha Dkt. Abbasi amesema Julai mwaka huu nchi itapokea ndege kadhaa
mpya ikiwemo Boeing Dreamliner na ukarabati wa viwanja vya ndege vya Kitaifa,
Kimataifa na Kimkoa unaendelea kwa kasi kote nchini.
Comments
Post a Comment