Vijana wasitumike kama vibaraka wa wanasiasa
KUELEKEA
maadhimisho ya Jumapili ya matawi ambayo ni sikukuu ya vijana, wito umetolewa
kwa vijana nchini kuielewa siasa kwa undani badala ya kutumika na watu wachache
wenye nia ya kujinufaisha wenyewe.
Wito huo umetolewa na Mratibu wa Vijana
Taifa katika Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania Padri Liberatus Kadio huku
akiakisi ujumbe wa Baba Mtakatifu Fransisko kwa maadhimisho ya siku ya 33 ya
vijana ulimwenguni, na kuwataka vijana nchini kuwa makini na namna
wanavyojikita katika shughuli mbalimbali za kisiasa.
“Elimu yetu haiwaandai vijana kuwa
wanasiasa wazuri, na hii inasababisha vijana wengi kujiingiza katika siasa
wakiwa na dhana kwamba kuwa mwanasiasa ni njia ya kuwa tajiri. Wanasahau kuwa
siasa ni njia ya kuwatumikia watu yaani kutumika. Shida hutokea pale ambapo
wengi hawapati kile walichokitarajia, matokeo yake kwa shauku hiyo ya utajiri
wanajikuta wakitumika kama vyombo vinavyowafaidisha wengine” amesema.
Aidha ametahadharisha kuwa vijana wanaporuhusu
kutumika na wanasiasa, wao ndiyo wanakuwa waathirika wakubwa, kwa kuwa
wanaowatumia wengi hawana nia njema ya kuwafanya wawe wazalendo kwa taifa bali
vibaraka wao.
Vijana
na hofu ya maisha
Akiuelezea ujumbe wa Papa kwa vijana mwaka
2018 unaoongozwa na maneno ya Mwinjili Luka “Usiogope, Mariamu, kwa maana
umepata neema kwa Mungu”, Padri Kadio amesema kuwa vijana nchini wanakabiliwa
na hofu ya maisha inayochangiwa na mfumo wa elimu ambao haumuandai kijana
ajiamini na ajitegemee katika kukabiliana na maisha, na badala yake unamfanya
awe tegemezi.
“Mfumo wa elimu unamfanya kijana asubiri
kuajiriwa, huku akiwa na matarajio lukuki kama vile kuishi maisha bora,
kumiliki mali na kupata kazi nzuri. Sasa inapotokea kijana amekosa fursa ya
kuajiriwa licha ya kuwa na elimu ya kutosha hapo ni lazima awe na hofu ya
maisha” ameongeza.
Pia ametaja hofu nyingine zinazowakabili
vijana kuwa ni pamoja na hofu ya imani inayosababisha vijana kuhama makanisa
wakitafuta utajiri, hofu ya kutopendwa kwa sababu ya kukosa fedha, mali au
nafasi na hofu ya kukataliwa.
Akitoa ushauri wa namna ya kukabiliana na
hofu hizo Padri Kadio amewataka vijana kuwa na ujasiri wa kuyaweka mambo yote
mikononi mwa Mungu, huku wakiwa na uthubutu wa kutumia elimu, ujuzi na nguvu
walizonazo katika kukabiliana na changamoto za maisha.
“Wao ni kanisa la leo na kesho, hivyo
uthubutu wao ndiyo utasababisha tuwe na mapadri wazuri, watawa wazuri, wazazi
wazuri na waamini imara. Yote wayaweke mikononi mwa Mungu na wawe tayari
kujifunza kupitia maandiko matakatifu” ameongeza.
Vijana
na kitubio
Akitoa tathmini kuelekea kilele cha
Jubilei ya Miaka 150 ya Uinjilishaji Tanzania Bara Padri Kadio amesema kuwa
vijana wanapaswa wahimizwe juu ya umuhimu wa kukaa karibu na sakramenti ya
kitubio na sakramenti ya Ekaristi Takatifu na kuachana na dhana kwamba
sakramenti hizo ni kwa ajili ya wazee.
Amesema kuwa kitubio ni sakramenti
inayompa kijana ujasiri na uthubutu wa kutenda yaliyo mema hivyo hawana budi
kuijongea na kuachana na dhana potofu kuwa hakuna haja ya kuungama kwa padri au
dhana ya kujiungamisha.
Comments
Post a Comment