Ask.Nzigilwa aonya kuhusu kulipiza kisasi, kinyongo
Waamini wakatoliki nchini, wameshauriwa
kutenda mambo yale wanayoyaona kuwa ni madogomadogo katika maisha yao ya kila
siku, kwa kuwa hayo yanayoonekana madogo ndiyo yanamfikisha mtu mbinguni.
|
Wito huo umetolewa hivi karibuni na Askofu Msaidizi wa Jimbo Kuu Katoliki Dar es Salaam, Mhasham Eusebius Nzigilwa,
wakati wa Ibada ya Misa Takatifu ya Maziko ya Emmanuel Muunga, Mmisionari wa
Shirika la Utoto Mtakatifu jimboni humo iliyofanyika katika Parokia ya
Hananasifu.
Askofu Nzigilwa amesema kuwa watu walio wengi wana kawaida ya kudharau
mambo madogo madogo, huku wakiamini kuwa hayana uhusiano katika maisha yao ya
hapa duniani na mbinguni, hali ambayo amesema haifai katika maisha ya mwamini
mkatoliki.
Akimzungumzia Emmanuel Muunga, Askofu Nzigilwa amesema kuwa, marehemu
enzi za uhai wake alijitahidi sana katika kuziishi vyema sakramenti za Kanisa Katoliki, ambazo alijaliwa kuzipata
ikiwa ni Ubatizo, Kipaimara na Ndoa Takatifu, ambapo katika maisha yake yeye
kwa kushirikiana na mke wake na watoto
wake, walijitoa kiaminifu katika umsionari wa uinjilishaji kupitia Shirika la
Kipapa la Kimisionari Jimbo Kuu Dar es Salaam.
Aidha, ameongeza kwa kuwakumbusha waamini suala zima la msamaha, huku
akihusisha na kipindi hiki cha kwaresma kinachosimamia toba na msamaha akisema;
“Hakika nawaambieni msipowasamehe
watu makosa yao, hakika baba yenu wa mbinguni hatawasamehe milele, pia tusiwe
na tabia ya kuweka vinyongo wala kulipiza kisasi, tunapaswa kutambua kuwa sisi
sote tunahitaji msamaha na huruma ya Mwenyezi Mungu,”Askofu Nzigilwa.
Akiwasilisha salamu za Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki Dar es Salaam
Mwadhama Polycarp Kardinal Pengo Askofu Nzigilwa amesema kuwa, Mwadhama
amepokea taarifa za msiba huo kwa masikitiko makubwa sana na hivyo ametoa pole
zake za dhati kwa familia ya Mzee Gerald na Mama Muunga, pamoja na mke na kwa
watoto wa marehemu kwa kifo cha mpendwa wao Emmanuel Muunga.
“Hii familia huwa inamfurahisha sana, katika matukio ya kijimbo familia
hii imekuwa mstari wa mbele daima, kila anapoiona huwa inambariki sana, na amewataka
kupitia tukio hili wasitetereke bali waendelee kudumu katika Ibada na kujitoa
zaidi kwenye mambo ya Mungu”, Askofu Nzigilwa alipowasilisha salamu za Baba
Mwadhama.
Kwa Upande wake Paroko wa Parokia ya
Kimara Mtoni, alikokuwa anasali marehemu enzi za uhai wake, Padri
Patrick Msumba mmisioanari wa shirika la Marianhill amesema kuwa, kila mwamini
anapaswa kujifunza kuwa hata akiwa na nguvu kiasi gani, itafika wakati
atahitaji tuu japo kuinuliwa juu au kushikwa mkono na mtu mwingine ili usonge
mbele, hivyo amewataka watu kuishi kwa upendo na ushirikiano.
Amezungumzia namna alivyomfahamu Emmanuel na familia yake yote, anaamini
kabisa kwamba marehemu alijitahidi sana katika kutimiza wajibu wake katika
kutenda yale yote aliyopaswa kuyatenda, na kwa wakati, hali ambayo amedai kuwa
imeacha alama ndani ya Kanisa la Kimara, na wameahidi kuienzi hiyo hali pamoja
na familia ya marehemu kwa muda wote.
Padri Timoth Maganga Nyasulu ambaye yeye ni Mkurugenzi wa Mashirika ya
Kipapa Jimbo Kuu katoliki Dar es salaam, na Paroko wa Kanisa la Bikira Maria
Mama wa Huruma Mbezi Beach, amesema kila Mwamini mbatizwa anapaswa kukitazama
kifo na kisha kujitafakari upya katika mwenendo wa maisha yake ya kila siku,
huku akisisitiza kuwa ni vyema kila mmoja akatimiza wajibu wake kwa Umma, kwa
Kanisa na kwa ulimwengu mzima.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Mashirika ya Kipapa Taifa, Padri Jovitus
Mwijage, katika salamu zake za rambirambi amesema kuwa, kila mmoja anapaswa
kutambua kuwa uwepo wake hapa duniani anamtafuta Mungu, hivyo hana budi kuishi
kadiri ya maongozi ya Mwenyezi Mungu.
“Hata Emmanuel alikuwa akimtafuta
Mungu, na leo tunapomsindikiza tunaamini kuwa anakwenda kupata zawadi yake kwenye maisha ya milele”.
Emmanuel Gerald Mokiwa Muunga, aliyekuwa Mmisionari wa Shirika la Kipapa
Jimbo Kuu Katoliki Dar es Salaam, alizaliwa 05.12.1981, na kufariki tarehe
24.02.2018, katika Taasisi ya Mifupa ya Hospitali Ya Taifa Muhimbili, ameacha
mke mmoja Bi Maria Muunga na watoto wawili wakike Precious na Princess Emmanuel
Muunga, ambao wote ni Wamisionari wa Shirika la Utoto Mtakatifu Jimboni humo
Comments
Post a Comment