MKUTANO MKUU WA 17 ACWECA KUFANYIKA TANZANIA

n  Na Sarah Pelaji

UMoja wa Mashirika ya Watawa wa Kike Afrika Mashariki na Kati, (ACWECA) kufanya Mkutano Mkuu wa 17  Katika Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania( TEC) Kurasini jijini Dar es Salaam.
Katibu Mkuu wa umoja huo  Sista Eneless Chimbali amethibitisha kwamba Mwadhama João Kardinali Bráz de Aviz ndiye atakayeongoza Ibada ya Misa takatifu ya ufunguzi wa Mkutano huo  wa 17 wa ACWECA Agosti 27, maaskofu wengine kutoka nchi wanachama, Msimamizi wa Maisha ya wakfu kutoka Vatikani na Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania Mhashamu Tarcisius Ngalalekumtwa watahudhuria.
Mkutano huo wa juma moja  utaanza Agosti 26 hadi Septemba 2 mwaka huu ukiongozwa na kauli mbiu: “Kuimarisha umoja wetu katika uinjilishaji wa kina katika mazingira ya sasa.”
Rais wa Umoja huo, Sista Priscar Matenga amesema kuwa, dhamira ya mkutano huo inatoa mwito kwa wanachama wa ACWECA Kuimarisha umoja na kusherehekea umoja wao.
“Tupo na tunaishi katika ulimwengu uliounganishwa kama kijiji kimoja na mambo yanabadilika  kwa haraka na sisi kama watawa lazima turejee na kutafakari maisha yetu kwa pamoja na kuona mambo kama vile Kristo alivyoyaona, kwa hiyo tunahitaji ushirikiano kujiimarisha kwa ajili ya kuinjilisha. Hivyo, tunawasisitiza wanachama  kujiuliza, nini hitaji letu katika nyakati hizi? Tunataka kueleza nini, tufanye nini ili kujiunganisha pamoja kama wanachama wa ACWECA ili utume wetu uzae matunda yanayohitajika na kizazi cha leo  na watu tunaokutana nao katika maisha yetu ya siku?” amesisitiza Sista Matenga.
Katibu Mkuu wa Umoja huo, Sista  Eneless Chimbali ameelezea pia umuhimu wa umoja huo akisema kuwa, baadhi ya nchi wanachama wa ACWECA wanazo rasilimali nyingi zaidi ya wengine hivyo umoja wao utasaidia wanachama wengine walio katika nchi zilizo na upungufu wa rasilimali  hivyo kufikia malengo yao hayo kuliko kila watawa wangebakia katika nchi zao tu.
Amesema, “Wajibu wa Umoja wetu ni  kukuza ari ya ushirikiano na kushirikishana maisha ya kiroho, wanadamu na uchumi kati ya wanachama na na kuimarisha malezi ya utawa, uwezo wa uongozi kwa Uinjilishaji wa kina,” amesema.
Aidha ameeleza kuwa, Mkutano huo utawajumuisha wamama wakuu kutoka nchi mbalimbali wanachama, hivyo watapata fursa ya kufahamiana, kufarijiana na kupeana moyo katika kazi ya kuinjilisha.
Pamoja na mambo mengine ametaja moja ya mada zitakazojadiliwa kuwa ni : Watawa wa Kike wa Kanisa Katoliki kama mabingwa wa Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs).
“Umoja wa Mataifa daima huzungumzia kuhusu SDGs lakini mara nyingi sisi watawa hususani wa kike tunakwepa jukumu hilo bila kutambua kwamba watawa ndiyo wanaohusika wa shughuli hizo za maendeleo,” amesema.
Amesema majadiliano ya mada hiyo yatawasaidia watawa kuanza kuandika baadhi ya shughuli wanazofanya ili waweze kukubali  kikamilifu SDGs.
Katibu Mkuu pia ameeleza kuwa masista wengine wawili watafafanua zaidi dhumuni la Mkutano huo mkuu ili kuwasaidia watawa kuelewa zaidi.
Sista Mary Abut mwanachama wa Bodi ya umoja huo amesema kuwa, dhamira ya mkutano huo ni  matokeo ya tafakari na sala ndefu ya wanachama wa ACWECA.
“Suala la Uinjilishaji siyo jambo jipya kwa wanachama lakini uinjilishaji mpya unaohitajika katika ulimwengu wa sasa ni tofauti na wa zamani. Hivyo Wanachama walitaka dhamira itakayowawezesha kutafakari njia bora za uinjilishaji wa sasa katika Kanda ya Mashariki na Kati,” Amesema Sista Abut.
Aidha ameeleza kuwa, mkutano huo ni muhimu kwa watawa kwani utakuwa kama jukwaa la kutathmini majumuisho ya Mkutano Mkuu wa 16.
“Mkutano huo utatusaidia kujua kama mapendekezo ya Mkutano wa 16 yamefanyiwa kazi, yamefanikiwa au la na nini kilitufanya tufanikiwe ili tusiendelee na changamoto hizo kwa miaka mitatu ijayo,” Amesema Sista Mary.
Taarifa kutoka Ofisi ya Mawasiliano ya ACWECA zinafafanua kuwa mada nyingine zitakazotolewa ni pamoja na Uongozi wa ufanisi kwa maisha endelevu, ya watawa, 
“Masuala ya Uongozi na malezi endelevu hususani uchumi  ni mambo ya msingi kwa watawa ili wajue namna ya kufanya biashara endelevu.
Suala la Uongozi na malezi ni sehemu ya kwanza ya mpango Mkakati wa 2017-2022 wa ACWECA.
“Malezi ni suala nyeti na ndio kipaumbele cha maisha ya utawa. Lazima tuwaandae watawa wetu ipasavyo ili waishi maisha ya wakfu ipasavyo na kutumikia kikamilifu,” amesema Katibu Mkuu wa Umoja huo Sista Chimbali.
Ifahamike kuwa wanachama wa ACWECA ni watawa kutoka Ethiopia, Kenya, Uganda, Malawi, Tanzania na Zambia.


Comments

Popular posts from this blog

SALA YA ASUBUHI:SALI HIVI..

Ujio wa Wamisionari wa Kwanza Tanzania Bara (2)

HISTORIA YA SHEREHE YA MOYO MTAKATIFU WA YESU