Miaka 100 ya Upadri yaleta neema Njombe

n Na Innocent Chaula, Njombe
IMEFAHAMIKA kuwa Mwaka wa Jubilei ya Miaka 100 ya Upadri Tanzania Bara imezaa matunda mema baada ya Parokia ya Mt. Yosefu Njombe Mjini kufanikiwa kutoa Sakramenti ya kipaimara kwa vijana 750, tukio ambalo limefanyika ndani ya siku tatu.
Askofu wa Jimbo Katoliki Njombe Mhashamu Alfred Maluma katika mahubiri yake sambamba na kutoa Sakramenti hiyo, amewaasa watoto kuzingatia mpango wa Mungu katika maisha yao hasa katika mwaliko wa Mungu unaowaita wamtumikie yeye kwa namna mbalimbali za miito mitakatifu ya Upadri na Utawa.
“Mungu alituumba kwa sura na mfano wake, na hivi hakuna mtu aliyeumbwa kwa bahati mbaya. Kila mwanadamu ni chapa ya Mungu. Mungu ana malengo na makusudi yake katika uumbaji wa kila mwanadamu. Mpango huo wa Mungu unasikika katika kuitwa kwetu tumtumikie Mungu katika wito mtakatifu. Ili tuweze kusikia vyema na kuifuata sauti ya Mungu vizuri, tunahitaji kuwa na familia bora ambazo zitawalea vyema watoto na kuwafundisha maadili mema yatakayowasaidia vijana kuitambua sauti ya Mungu. Katika maadhimisho ya Maika 100 ya Upadri Tanzania, tumwombe Mungu awaite vijana wema watakaomtumikia katika wito wa upadri. Mavuno ni mengi lakini watenda kazi ni wachache. Tumwombe Bwana wa mavuno apeleke watenda kazi katika shamba lake. Daima zingatieni kazi ya Mungu na mwito wenu.”
Mara baada ya kupokea Sakramenti Takatifu ya Kipaimara, watoto wameahidi mbele ya Askofu na Kanisa zima kuwa watadumu katika imani yao Katoliki ya Mitume na pia wataitetea imani yao kwa nguvu zao zote kwani mapaji ya Roho Mtakatifu waliyoyapokea ni kwa ajili ya kulilinda na kulitetea Kanisa na imani yao.
Wazazi wa watoto hao waliopokea Sakramenti ya kipaimara wamemshukuru Askofu Maluma kwa kazi nzuri na nzito aliyoifanya kwa vijana wao huku wakimuahidi kuwalea watoto wao katika imani yao na kuwaongoza vyema katika kuitikia sauti ya  Mungu.


Comments

Popular posts from this blog

SALA YA ASUBUHI:SALI HIVI..

Ujio wa Wamisionari wa Kwanza Tanzania Bara (2)

HISTORIA YA SHEREHE YA MOYO MTAKATIFU WA YESU