KANISA KATOLIKI LAIKABIDHI SERIKALI JENGO LA OFISI YA KATA MOROGORO



n Na Angela Andrew, Morogoro
MAKAMU Askofu wa Jimbo Katoliki Morogoro Padri Patrick Kung’alo amesema kuwa Kanisa Katoliki limejiwekea malengo ya kuendelea kutoa huduma bora za kijamii hasa afya na elimu ili kuwahudumia waamini na wananchi wengi zaidi kimwili na kiroho.
Padri Kung’alo amesema hayo hivi karibuni katika hafla maalumu ya kumkabidhi Mkurugenzi wa wilaya ya Mvomero Frolent Laurenti jengo la ofisi ya Kata ya Kinda ambalo limejengwa na Kanisa Katoliki ili kutumika kama ofisi ya Kata hiyo.
Padri Kung’alo ameeleza kuwa malengo ya Kanisa Katoliki kusimamia huduma za kijamii ni kuisaidia Serikali kwa lengo la kuhakikisha kuwa mwanadamu anapata huduma msingi za kibinadamu ili kumtumikia Mwenyezi Mungu daima.
 Aidha padri Kung’alo amesema zipo shule nyingi, hospitali, vituo vya afya na zahanati mbalimbali katika ushiriki wa utoaji huduma za jamii, ambapo Serikali pia mara kwa mara imekiri wazi namna Kanisa linavyochangia utoaji wa huduma msingi za kijamii.
“Kanisa Katoliki linajulikana sana katika utoaji huduma za jamii kupitia elimu na afya, na litaendelea kufanya hivyo mpaka mwisho wa nyakati, tunazo shule zinazoendeshwa na Kanisa Katoliki kuhudumia jamii ikiwa ni kuisaidia Serikali yetu,” amesema padri Kung’alo.
Hata hivyo kiongozi huyo wa kiroho amesema kuwa Kanisa Katoliki litaendelea kuwa bega kwa bega na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania huku akiwaomba watumishi watakaotumia ofisi hiyo kutumia karama zao kuboresha huduma kwa wananchi.
Wakati huo huo padri Kung’alo amewaasa watanzania kumtanguliza Mwenyezi Mungu, kama ambavyo Rais John Magufuli anavyoendelea kusisitiza katika hotuba zake mbalimbali ili jengo hilo litumike kufanya mikutano mbalimbali kwa lengo la kuwagusa wanadamu kwa mujibu wa mapenzi ya Mwenyezi Mungu.
“Tuiombee ofisi hii na wale watakaoitumia kuguswa na mahitaji ya wanadamu, kila mtumishi ahakikishe anafanya kazi kwa kuzingatia mahitaji ya jamii, na nina hakika haya ni mapenzi ya Mwenyezi Mungu kwa sababu wote tupo kwa ajili ya kusaidiana na kuhurumiana,” amesema padri Kung’alo.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa wilaya ya Mvomero Frolent Laurent amelishukuru Kanisa Katoliki kuendelea kushirikiana na Serikali huku akiwaomba watumishi wa Kata hiyo kufanya kazi kwa ushirikiano na mshikamano kugusa mahitaji ya wananchi.


Comments

Popular posts from this blog

SALA YA ASUBUHI:SALI HIVI..

Ujio wa Wamisionari wa Kwanza Tanzania Bara (2)

HISTORIA YA SHEREHE YA MOYO MTAKATIFU WA YESU