Miaka 9 baada ya kifo cha Mgandu: watunzi wa sasa mna cha kujifunza!

Na Pascal Mwanache

TUNAPOENDELEA kusherehekea Jubilei ya miaka 150 ya Uinjilishaji Tanzania Bara, tuna kila sababu ya kujivunia kwa uwepo wa Utume wa Uimbaji hapa nchini.
Uwepo wa kwaya katika maadhimisho ya Misa Takatifu umesaidia sana kukoleza Liturujia na kuwasaidia waamini kusali vizuri, ili Mungu atukuzwe na mwanadamu atakatifuzwe. Ili malengo ya utume wa uimbaji yaweze kufikiwa ni lazima kuwe na mahusiano mazuri na ya pande mbili kati ya watunzi wa muziki mtakatifu na waimbaji (wanakwaya).
Hawa kwa pamoja wanakamilisha mzunguko wa mawasiliano, ambapo mtunzi huwa kama mtumaji wa taarifa (sender) huku waimbaji wakiwa wapokeaji na watekelezaji (receivers) wa kile kilichoandaliwa na mtunzi. Hivyo basi, ili mawasiliano haya yaweze kuleta tija kwa waamini ni lazima watunzi wawe msaada kwa wanakwaya, ili wanakwaya wawasaidie waamini kusali vizuri.
Kwa miaka ya hivi karibuni kumeibuka wimbi la watunzi ambao kwa namna fulani wanaenda nje ya mstari. Utunzi wao haukaisi liturujia, haudhihirishi ule utajiri wa mafundisho ya Kanisa. Ndiyo kusema kwamba, wengi hutunga nje ya maandiko matakatifu, mafundisho ya kanisa na mapokeo kwa kile wakiitacho kwenda na wakati.
Kwa hakika huku ni kuibinfsisha liturujia. Kama wanakwaya wanageuza kanisa kuwa sehemu ya burudani, huko ni kubinafsisha liturujia. Iwapo watunzi wanatunga nyimbo kwa kutumia maneno ya mtaani, huko ni kubinafsisha liturujia. Utunzi wa nyimbo ngumu zenye kona nyingi eti kwa kigezo cha kuonyesha ufundi, huko ni kubinafsisha liturujia.
Hayo yote hayamsaidii muumini kusali vizuri, tena zaidi haimfanyi Mungu atukuzwe na binadamu atakatifuzwe. Ndiyo maana tuna kila sababu ya kujifunza kutoka kwa watunzi walioturithisha tunu na hadhi bora za muziki mtakatifu. Wapo walio hai na wengine wametangulia mbele ya haki, lakini mifano yao ingali inaishi. Tuchote na tuutumie utajiri huo.
Mmoja kati ya watunzi ambao walijitahidi kutumia karama zao katika kuwasaidia waamini kusali vizuri kwa njia ya uimbaji ni Mwalimu John Stephano Mgandu.Yeye alizaliwa Oktoba 8, 1940 kijijini Busondo, katika Parokia ya Ndala-Nzega, mkoani Tabora.
Alipata elimu katika Shule ya Msingi Puge (1951-1953), kisha Seminari ya Lububu (1954 – 1955), baadaye Seminari ya Itaga (1956 – 1959) na Seminari ya Kipalapala 1964. Mwaka 1960 hadi 1970 alikuwa katika Chuo cha Ualimu cha Chang’ombe.
Elimu ya muziki aliipata katika Chuo Kikuu cha Toronto nchini Canada ambako alisomea Shahada ya Muziki (Bsc – Music) 1972 – 1976, na baadaye Chuo Kikuu cha Dar es salaam akisomea Shahada ya Uzamili (MA – Music) 1987.
Amewahi kufanya kazi katika maeneo mbalimbali pamoja na Benki ya NBC tawi la Masdo (1968), Shule ya Sekondari ya Kibasila (1970), Shule ya Sekondari ya Mirambo (1971), Shule ya Sekondari ya wavulana Tabora (1976 – 1978), Taasisi ya Elimu (1978 – 1980) na kisha Chuo Kikuu cha Dar es salaam katika Idara ya Sanaa na maonyesho (Julai 1980 – Julai 2008)
Alifunga ndoa na Elizabeth Kulwa Binti Constatino Ngelegi, na kupata watoto wawili, wa kiume na wa kike. Licha ya kuwa mtunzi, Mwalimu Mgandu alikuwa mpiga kinanda, filimbi na ala nyingine nyingi. Pia alikuwa mwalimu na muongozaji wa muziki na kwaya mbalimbali.

Ikumbukwe kuwa mwaka 2002  Mwalimu Mgandu alishinda tuzo ya kuwa Mpiga Kinanda Bora Tanzania (Tanzania Kilimanjaro Music Awards). Alifariki Julai 10 mwaka 2008.
Kuna mengi ya kujifunza kutoka kwa nguli huyu wa muziki mtakatifu, moja kati ya mengi ni taaluma ya muziki mtakatifu. Mwalimu Mgandu alikuwa mwanamuziki aliye na taaluma hata kuwa na Shahada ya uzamili (Masters) ya muziki. Cha ajabu watunzi wengi siku hizi huridhika kujifunza muziki mtakatifu kwa kuunga unga. Hii hupelekea kuzorota kwa taaluma hii, kwani kilichobaki kwa sasa ni watu kurithishana na kufundishana kienyeji tu.
Hii itukumbushe pia umuhimu wa kufufua madarasa ya muziki Mtakatifu katika Seminari, nyumba za malezi, vyuo vikuu vya kanisa ili tupate wataalamu wa kutosha.
Lakini kubwa zaidi, pamoja na kuwa na elimu kubwa mwalimu Mgandu daima tungo zake zilizingatia liturujia na alitumia maandiko matakatifu kama rejea ya nyimbo zake. Sasa watunzi wa leo wanaotunga nyimbo kama ‘chenga ya mwili’, ‘gari la shetani’ nk, wamejifunza wapi mambo hayo.
Ikiwa sisi tulirithi muziki mtakatifu uliokolezwa liturujia nyoofu kutoka kwa watunzi kama Padri Gregory Kayetta, Padri Malema, Padri Ntampambata, Nyundo, Syote, Makoye, Mujwahuki, Mkomagu na wengine wengi, kwa nini nasi tusirithishe muziki huo kwa vizazi vijavyo? Kwa nini tunataka kuwarithisha maneno ya mitaani?

Mchambuzi: 0657835343


Comments

  1. Habari za Kazi Mr Pascal. Pascal asante sana kwa makala yako nzuri inayowatahadharisha wwatunzi wa nyimbo za iabada kuendana na maandiko. Nakupongeza sana! Ila nahisi kuna makosa kidogo katika historia ya Mwl John Mgandu. Umeandika kuwa alikuwa Seminari ya Kipalapala mwaka 1964 na mwaka 1960 hadi 1970 alikuwa chuo cha ualimu Changómbe. Ina maana mwaka 1964 alikuwa Kipalapala na wakati huo huo yupo Changómbe. Naomba ucheck vizuri hizo tarehe

    ReplyDelete
  2. Mzee wetu mgandu apumzike kwa Amani. Hakika mchango wake wa uinjilishaji ni mkubwa sana ambao tuliobahatika kufundishwa kidogo naye tunajisikia wenye bahati na upendeleo mkubwa.
    Tunaendelea kumkumbuka na kumthamanisha sana.
    Tunamwomba Mungu amsamehe makosa yake na kumstahilisha tuzo mbinguni. Apumzike kwa Amani AMINA

    ReplyDelete

Post a Comment

Popular posts from this blog

SALA YA ASUBUHI:SALI HIVI..

Ujio wa Wamisionari wa Kwanza Tanzania Bara (2)

HISTORIA YA SHEREHE YA MOYO MTAKATIFU WA YESU