Wito ni kazi ya Mungu siyo mwanadamu-Ask. Kinyaiya
ASKOFU Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki Dodoma
Mhashamu Beatus Kinyaiya amesema kuwa wito anaoitiwa mwanadamu yeyote siyo
wake bali ni wito unaotoka kwa Mwenyezi
Mungu.
Ameyasema hayo wakati wa
adhimisho la misa takatifu ya utoaji wa daraja takatifu la ushemasi kwa
mafrateri Dickson Komba na Justine Bonifasi wa Shirika la Wamisionari wa Damu
Azizi ya Yesu, iliyofanyika katika Parokia Bikira Maria Mama wa Damu azizi ya Yesu
Kisasa Jimbo Kuu Katoliki Dodoma.
Amesema kuwa mtu anapoitwa katika
wito fulani na Mungu anapaswa kuitikia hima ‘ndio’ mpaka tamati na siyo
kukatiza akiwa njiani.
Askofu Kinyaiya amesema kuwa
Mungu anajua aina ya watu anaowachagua katika kuingia katika wito mtakatifu.
“Mfano Yesu alimchukua Petro na
kuwa mfuasi wake lakini siku Yesu anateswa Petro alimkana kuwa hamfahamu, hivyo
msiwe kama Petro nyie simameni katika njia iliyo bora mliyoichagua” amesema
Askofu Kinyaiya.
Hata hivyo amewataka kuhakikisha
katika maisha ya wito walioitiwa katu wasikubali kuukana wito huo, bali
waukumbatie katika hali zote watakazokumbana nazo katika utume wao.
Aidha Askofu Kinyaiya amewataka
waamini mahalia kuwasaidia mashemasi hao katika wito wao pasi kuwaingiza kwenye
vishawishi vitakavyowakwaza katika utume wao.
Amesema kuwa kila mmoja wetu anao
udhaifu wake lakini katu usikubali kuuonyesha kwa watu wengine kuwa thabiti
katika utume wako na kuweni jasiri na kila mlifanyalo mtangulizeni Mungu mbele.
Amesema kuwa kama wao walivyochaguliwa
katika kundi la watu wanapaswa kuonyesha mfano wa kuigwa na katu wasiwe vikwazo
bali wawe ni daraja ambalo litawavusha watu kutoka sehemu moja kwenda nyingine
kwa hali ya amani na upendo.
“Mmekabidhiwa na kutumwa mkawe
wavuvi, wavuvi ni watu ambao wanavua samaki, ila nyie samaki wenu ni kundi
kubwa la kondoo waliokabidhiwa na mwenyezi mungu amablo ni waamini mahalia
hivyo wawafundishe yale wanayowapasa hususani katika kulihubiri neno la mungu.”
Aliongeza.
Comments
Post a Comment