JPM: Kipaumbele ni kuhuisha teknolojia ya viwanda SADC
RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt.John Pombe
Magufuli amefungua maonesho ya wiki ya viwanda kwa nchi wanachama wa Jumuiya ya
Maendeleo Kusini mwa Africa (SADC).
Akizungumza katika
hafla hiyo ya Wiki ya Viwanda ya SADC, Jijini Dar es Salaam, Rais Magufuli
amesema kuwa ili kufikia uchumi wa kati viwanda ni kichochea muhimu katika
sekta nyingi kwani uwepo wa viwanda utasababisha uhakika wa uzalishaji na
uchakataji wa bidhaa na kufanya biashara kwa nchi wananchama.
Rais Magufuli
amezitaka nchi wanachama wa SADC kuweka kipaumbele kwenye kuhuisha teknolojia
katika viwanda vilivyoko ndani ya jumuiya ya Maendelea kusini mwa afrika (SADC)
pamoja na kushughulikia kwa haraka zaidi vikwazo vinavyochelewesha ukuaji wa
viwanda.
“Viwanda ni Sekta
muhimu katika kukuza uchumi wa nchi yeyote, kuondoa umasikini, kuongeza ajira
na Sekta hii imeziletea maendeleo makubwa nchi zilizoendelea, kwa hiyo mkutano
huu ni dhahiri kuwa sasa nchi za SADC zimeanza kuchukua hatua madhubuti za
kukuza sekta hii na ikiwa mkakati huu utatekelezwa utasaidia kukuza uchumi wa
nchi zetu”, Rais Magufuli.
Akielezea suala la
teknolojia Rais Magufuli amesema kuwa ukuzaji wa teknolojia na ubunifu kwenye
sekta ya viwanda ni silaha muhimu kwa nchi za SADC kuendelea na kutegemeana
kwani utazalisha ajira, biashara kubwa, na kuepuka kuuza malighafi kwa wingi nje ya Afrika kama ilivyosasa.
Aidha Rais Magufuli
amezitaka nchi wanachama wa SADC kujikita zaidi katika kukuza ubunifu na
teknolojia rahisi kwenye sekta ya viwanda kwa kuwaendeleza vijana na kuimarisha
viwanda vidogo vidogo vilivyoko kwenye jumuiya, kwa hiyo wiki ya viwanda ni
fursa muhimu kwa nchi zote wananchama.
“Wiki ya Viwanda ya
SADC ni fursa ya kubadilishana uzoefu miongoni mwa wadau kuhusu utekelezaji wa
mikakati ya miaka 49 ya uendelezaji wa viwanda katika jumuiya yetu, bado tuna
safari ndefu kuhakikisha sekta ya viwanda inazidi kukua na kuleta mageuzi ya
kiuchumi katika nchi zetu”, amesema Rais Magufuli.
Kwa upande wake Waziri
wa Viwanda na Biashara wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Innocent Bashungwa
amesema kuwa uthubutu wa Rais Magufuli kuipeleka Tanzania katika uchumi wa kati
wenye viwanda ni mkubwa na matokea yake yanaonekana sasa. Hivyo, maonesho haya ni
moja ya njia muhimu ya kuimarisha sekta ya viwanda nchini.
“Maonesho haya ya wiki
ya viwanda yanawawezesha wanachama wa SADC kuona namna nchi wenyeji
inavyotekeleza uwekezaji kwenye sekta ya Viwanda. Aidha, tunaamini wazalishaji, wafanyabiashara, na wananchi
kwa ujumla watachangamkia fursa mbalimbali zitazotokana na mkutano huu wa
SADC.”, Waziri Bashungwa.
Waziri Bashungwa
amesema kuwa Tanzania inafanya vizuri kwenye biashara ndani ya SADC kwani takwimu zinaonyesha kuwa mauzo ya
Tanzania kwenda SADC mwaka 2018 yalikuwa dola za kimarekani milioni 999
ikilinganishwa na dola za kimarekani milioni 875 mwaka 2017 ikiwa na ongezeko
la asilimia 12.16.
Kwa upande wake Katibu
Mtendaji wa SADC, Dkt.Stagomena Tax, amesema kuwa juhudi za Serikali ya
Tanzania kutekeleza mradi mkubwa wa kufua na kuzalisha umeme mto Rufiji ni moja
ya njia madhubuti katika kuimarisha na kukuza sekta ya viwanda kwa Jumuiya ya
SADC.
“Kutekelezwa kwa Mradi
wa umeme mto rufiji tunaamini kuwa Tanzania itazalisha umeme wa kutosha,
tunaomba ziada iweze kwenda kwenye nchi wanachama wa SADC kwani kumekuwa na
changamoto ya kubwa mgawo wa umeme na uendeshwaji wa viwanda unahitaji mambo
mengi ikiwemo umeme huwezi kuwa na viwanda bila kuwa na umeme unaozalishwa kwa
urahisi, kwa hiyo Tanzania imechukuia maamuzi mazuri kuzalisha umeme mto
Rufiji.”, Stagomena Tax, Katibu Mtendaji, SADC.
Comments
Post a Comment