Kardinali Pengo afanya ziara ya kichungaji Shinyanga
ASkofu Mkuu Mstaafu wa Jimbo Kuu
Katoliki Dar es Salaam, Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo amewataka mapadri
kuambatana daima na Kristo katika utume wao badala ya kujiambatanisha na
malimwengu.
Kadinali Pengo ameyabainisha hayo
katika Kanisa Kuu Mama Mwenyehuruma Ngokolo Shinyanga wakati wa mahubiri yake
katika adhimisho la Ekaristi Takatifu na utowaji wa Daraja Takatifu la Upadri
kwa mashemasi sita katika sherehe ya Kupalizwa Mbinguni Bikira Maria
iliyofanyika 15 Agosti, 2019.
Katika ujumbe wake,Kadinali Pengo
amewataka mapadri hao wapya kwenda kufanya utume wao kwa uaminifu huku
wakitambua kuwa upadri ni kujitoa sadaka
kwa Mungu, hivyo wasifanye utume wao
kinyume na matarajio ya Wakristo ambao wanamategemeo makubwa juu yao na badala
yake wamtangulize Kristo katika huduma
yao kwa Kristo na Kanisa lake.
Aidha Kadinali Pengo ametoa wito
kwa waamini wa jimbo Katoliki Shinyanga
kuendelea kuwaombea mapadri wapya na mapadri wote kwa kuwa utume wa mapadri
hauwezi kufanikiwa bila sala za waamini.
Mashemasi waliopewa Daraja
Takatifu la Upadri ni Richard Masunga wa Parokia ya Malili, Gregory Samike wa
parokia ya Salawe, Peter Mkunya wa parokia ya Malampaka na Peter Tungu wa
parokia ya Mwanhuzi. Wengine ni Martine Masanja na Martine Jilala wote wa
parokia ya Mipa.
Akitoa neno la Shukrani kwa niaba
ya wanajimbo la Shinyanga kwa Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo, Askofu wa
Jimbo Katoliki Shinyanga Mhashamu Liberatus Sangu amesema kuwa ziara ya siku
nne ya Askofu Mkuu Mstaafu wa Jimbo Kuu Katoliki Dar es salaam Mwadhama Polcarp
Kadinali Pengo imekuwa kichocheo kikubwa cha miito ya upadri jimboni hapa baada
ya kuwapa Daraja Takatifu la Upadri mashemasi sita wa jimbo kwa mpingo, tukio ambalo lilitokea miaka 25 iliyopita katika historia ya jimbo
“tangu mwaka 1994 jimbo halijawahi kupata mapadri sita kwa mkupuo na leo wewe
Mwadhama umewapa Daraja hilo Takatifu la Upadri kupitia mikono yako mashemasi
sita wa jimbo” .
Askofu Sangu pia amemwelezea Kardinali Pengo
kuwa amekuwa chachu ya kujenga umoja, upendo na mshikamano katika taifa la
Tanzania na nje ya Tanzania kutokana na
kazi mbalimbali alizozifanya za kuwaunganisha watu wakati wote wa utume wake
katika Kanisa.
Askofu Sangu pia alitumia nafasi
hiyo kutoa shukrani zake kwa jinsi
serikali ya mkoa wa Shinyanga inavyoshirikiana na viongozi wa dini na ameahidi
kuendeleza ushirikiano huo ili kuhakikisha hali ya umoja, upendo na mshikamano
vinatawala katika jamii hatua ambayo
itasawaidia watu kujiletea maendeleo.
Kwa upande Mkuu wa mkoa wa
Shinyanga Bi Zainab Telack amelezea namna ambavyo viongozi wa dini likiwemo
Kanisa Katoliki wanavyotoa mchango katika kudumisha amani miongoni mwa jamii.
Ametolea mfano jinsi ambavyo
wamesaidia kukomesha mauaji ya vikongwe katika mkoa wa Shinyanga pamoja na kujenga misingi ya utulivu ambayo
imewasaidia viongozi wa serikali kuwaongoza watu bila migongano na kwa unafuu
mkubwa.
Mwadhama Polcarp Kadinali Pengo
aliwasili jimboni Shinyanga kupitia uwanja wa ndege wa Kahama siku ya Jumatano
Agost 14 mwaka huu na kupokelewa na Askofu wa Jimbo la Shinyanga Mhashamu
Liberatus aliyekuwa ameambatana na Askofu wa Jimbo Katoliki Kahama Mhashamu
Ludovick Joseph Minde, mapadri, watawa, waamini pamoja na viongozi wa serikali
akiwemo Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Zainab Telack.
Akiwa Kahama Kadinali Pengo amebariki mawe ya msingi ambayo yatatumika
katika miradi mbalimbali ya Jimbo Katoliki Kahama na kutoa Baraka kwa waamini
wa jimbo hilo na baadaye alifanya mazungumzo mafupi na askofu Minde.
Aidha akiwa jimboni Shinyanga
Kadinali Pengo ametumia siku ya pili ya mapumziko yake kubariki jengo la nyumba
ya mapadri linaloendelea kujengwa katika parokia teule ya Lubaga mjini
Shinyanga na kupanda mti wa kumbukumbu.
Comments
Post a Comment