Waliovamia kiwanja cha Kanisa waitwa kwa Lukuvi
WAZIRI wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo
ya Makazi, William Lukuvi ameagiza mmiliki wa Kituo cha mafuta cha Victoria
Service Station kilichopo maeneo ya Msimbazi Center, Dar es salaam kuwasilisha
kwake nyaraka zote kuthibitisha uhalali wa umiliki wake katika eneo hilo.
Waziri
Lukuvi ametoa agizo hilo katikati ya juma alipofanya ziara katika kituo hicho
cha mafuta kinachodaiwa kuendesha katika eneo halali la Kanisa katoliki Jimbo
Kuu Katoliki Dar es Salaam, kupitia Parokia ya Msimbazi.
Akiwa
katika eneo hilo pamoja na paroko wa parokia ya Msimbazi, Padri Gregory Josephat, Mwenyekiti wa Kamati ya
Ardhi ya Jimbo Kuu Katoliki Dar es Salaam, Albert Singombe, amemwambia waziri
kuwa, eneo kilipo kituo hicho cha biashara ya mafuta, ni mali ya Kanisa tangu
mwaka 1965 na nyaraka halali za umiliki zipo.
Baada
ya Padri Greogory na Bw Singomnbe kumwonesha nyaraka za umiliki wa eneo hilo na
kusikiliza maelezo ya mwendeshaji wa kituo hicho, waziri Lukuvi amesema nyaraka
hizo za Kanisa ikiwamo hati na zile zilizopo ofisini kwake zinabainisha kuwa,
wamiliki wa kiwanja hicho ni Kanisa Katoliki kwa kuwa tangu mwaka 1965 Kanisa
lilipopata hati hiyo, haikuwahi kufutwa.
Amesema
ingawa anazitaka pande zote husika katika mgogoro huo wa ardhi kufika ijumaa
hii ofisini kwake jijini Dar es Salaam na vielelezo husika, kwa kawaida na
kisheria kama hati ya umiliki wa Kanisa Katoliki haikufutwa, basi kama kuna
nyingine iliyotolewa katika kiwanja hicho hicho, hiyo nyingine ni batili.
“Kisheria
ili kuhamisha umiliki, lazima ile ya kwanza ifutwe. Sasa kama haikufutwa, hii
nyingine ni batili maana hakuna hati inayotolewa juu ya hati nyingine, wala
mchoro wa kiwanja unaochorwa juu ya mchoro mwingine,” amesema Waziri Lukuvi.
Katika
maelezo yake kwa waziri, mmiliki huyo wa Victoria services station, amesema
eneo hilo aliuziwa na Hawel (Abdalla Thabit Hawel) mwenye asili ya Kiarabu,
aliyempa nyaraka akimhakikishia kuwa kiwanja hicho ni mali yake.
Baada
ya kusikia maelezo hayo waziri Lukuvi akasema: “Njoo Ijumaa pale ofisini kwangu
na nyaraka zako zote; na hata Kanisa njooni na nyaraka zote na mtu yeyote
anayejua vizuri aneo hili.”
Akaongeza;
“Kwa mara ya kwanza leo ndipo nimesikia kuwa mwarabu anamuuzia mswahili eneo,
badala ya mswahili kumuuzia mwarabu… halafu waarabu kwa biashara hii ya mafuta
tena katika eneo hili la barabarani mpaka akuuzie, lazima alijua kuna bomu hapo na nadhani ndugu yangu
hapa kuna mchezo mchafu umefanyika umeingizwa mkenge.”
Aidha
amesema nyaraka zilizowasilishwa na Kanisa sambamba na maelezo ya wawili,
zinaonesha kuwa eno hilo ni mali ya Kanisa kwa kuwa hati ya Kanisa ni hai na
haijafutwa.
“Askofu
Nzigilwa (Askofu Msaidizi wa Jimbo Kuu Katoliki Dar es Salaam) alikuja pale
ofisini akanionesha hati zote na tumezichunguza na kuangalia nakala zetu ,
tumejiridhisha kuwa, bado eneo hili ni mali halali ya Kanisa maana hati bado ni
hai,” ameeleza Lukuvi.
Awali
katika ziara hiyo, waziri Lukuvi alimrudishia bw. Ramadhani Sood Bulenga jengo
lake la ghorofa nne lililopo maeneo ya mzunguko wa kigogo wilayani Ilala baada
ya jengo na eneo hilo kumilikishwa kinyume na taratibu kwa mtu aliyefahamika
kwa jina la Hans Macha.
Lukuvi
amesema kutokana na hali hiyo, amemwondoa kazini kamishina aliyehusika na
ukiukaji huo wa taratibu na kumteua David Mshendwa kushika wadhifa huo.
Comments
Post a Comment