Wawakilishi wa Caritas wakutana Tz, watoa neno kwa maaskofu
WAKATI
wafanyakazi wa Shirika la Misaada
la Kanisa Katoliki (Caritas) wakitakiwa kujitathimini kuona kama utendaji wao
unabeba utambulisho wa chombo hicho, Maaskofu nchini wameombwa kulichukulia shirika hilo kama nyenzo yao
ya kuhudumia jamii kiroho na kimwili,
hivyo kuhakikisha wanazifuatilia kwa karibu shughuli za utendaji wake.
Ombi hilo limetolewa na Katibu Mtendaji Msaidizi
wa Caritas Internationalis, Roma, Monsinyori Pierre Cibambo, wakati wa mkutano
baina ya timu ya wawakilishi wa Caritas ilipomtembelea Mwenyekiti wa Idara ya
Caritas- Tanzania, Askofu Mkuu Yuda
Thaddeus Ruwa’ichi, uliofanyika nyumbani kwake, Kurasini jijini Dar es Salaam
mwanzoni mwa juma.
Monsinyori
Pierre ambaye katika ziara hiyo aliongozana na Makatibu Watendaji wa Caritas Afrika, AMECEA na watendaji wa Caritas- Tanzania ngazi ya taifa, amesema
kuwa tangu kuanzishwa kwake, Caritas ni
chombo cha maaskofu lengo lake likiwa ni kufanya matendo ya huruma kwa makundi
mbalimbali ndani ya jamii hususan maskini,
hivyo ili kiweze kutimiza majuku yake ipasavyo, hakina budi kupata
ushirikiano kutoka kwa viongozi hao wa kiroho.
“CARITAS-
Tanzania ni kioo cha maaskofu wote wa TEC na Kanisa la Tanzania kwa ujumla,
hivyo kufanya kwake vizuri ni taswira nzuri pia kwa baraza ambalo maaskofu wake
walioshiriki kwa namna ya pekee kuanzishwa kwa shirika hili la hisani, “ amesema.
Sanjari
na hilo, Monsinyori Pierre alisema, ukaribu wa Maaskofu kwa Caritas kutawafanya
hata watendaji wa shirika hilo kufanya kazi zake katika uwajibikaji wa hali ya
juu , wakitambua kuwa juu yao kipo chombo kinachowasimamia na kuwafuatilia kwa
karibu.
“Hata
kama utapata misaada lakini kama hauna chombo ama mtu wa kusimamia kwa karibu,
bila shaka huwezi kufika mbali katika kutimiza lengo lililokusudiwa, kwani
mtekelezaji wa shughuli utakuwa ni wewe mwenyewe, unajifanyia tathmini mwenyewe
na hata ukaguzi wa mahesabu ni mwenyewe… ukifanya kazi namna hii bila shaka
hauwezi kufika mbali,” alisema.
Hata
hivyo Monsinyori Pierre alisema, katika utafiti wao sehemu mbalimbali duniani,
wamebaini kuwa kuna baadhi ya nchi ambako
Caritas inafanya kazi kama baadhi ya NGO, ambapo watendaji wake
wanajali zaidi maslahi yao binafsi
ikiwemo mishahara mkubwa na stahiki
nyingine, hivyo kupoteza utambulisho wa kuanzishwa kwake kama chombo cha kueneza
upendo na kufanya matendo ya huruma kwa masikini.
“Caritas haitakiwi kufanya kazi yake
kwa ushindani kama zilivyo baadhi ya NGOs, bali utekelezaji wa majukumu
yake lazima uendane na utume wa Kanisa wa kumuhudumia mtu kimwili na kiroho na
hasa suala la ujenzi wa amani, kutoa misaada ya kiutu kwa watu wanaopata
majanga na matatizo mbalimbali na huduma nyinginezo, hivyo kutekeleza tunu
ya viongozi wa Kanisa ya kuwa sauti ya
wasiyokuwa na sauti,” alisisitiza.
Aliongeza
“Ni kutokakana na sintofahamu iliyojitokeza ndani ya Caritas hasa ya
kupoteza utambulisho wake, kulikopelekea hata Kiongozi wa Kanisa Katoliki
Duniani, kuliagiza shirika hili kujitathmini ili kuona kama utendaji wa
shughuli zake unaendana na madhumuni ya uanzishwaji wake ama vinginevyo,”
alisema.
Alitoa
wito kwa wafanyakazi wote wa Caritasi kutambua utendaji wa shughuli zao upo
chini ya askofu wa eneo husika iwe ngazi ya Taifa ama Jimbo, hivyo hawanabudi
kufanya kazi zao kwa uwazi na kuwajibika vilivyo kwa viongozi wa maeneo husika.
“
Pia mapdri na watawa wa kike na kiume washirikishwe ili waweze kuitambua
Caritas na shughuli zake…jambo hili pia ni vyema likaendana na kuwafundisha
waamini katika ngazi zote kuanzia kwenye jumuiya Ndogondogo za Kikristo, juu ya
kufanya matendo ya huruma, hivyo kuwahamasisha kutoa kwa ajili ya wahitaji
wakiwemo masikini na watu wenye kupata majanga mbalimbali,” alisisitiza.
Katika
hili aliongeza kuwa hata Ulaya wanaotoa misaada siyo matajiri bali ni watu
wenye kipato cha kawaida ambao wanaupendo na hofu ya Kimungu ya kuwasaidia
wengine, hivyo akatoa wito pia kwa ofisi ya Caritas Taifa kuendelea kutekeleza
majukumu yake hasa ya kuratibu kazi za majimbo pamoja na kusimamia miradi
inayofadhiliwa na Caritas Internatiolis, badala ya kutekeleza moja kwa moja
miradi hiyo.
Hata
hivyo hakusita kutoa pongezi zake kwa Katibu Mkuu wa Baraza la Maaskofu
Katoliki Tanzania(TEC), Padri Charles Kitima, ambapo alisema baada ya
kuzungumza naye, alionyesha kulifahamu vilivyo lengo la Caritas na zaidi,
Katibu Mkuu huyo aliahidi kuwa TEC katika mipango yake, itaweka vipaumbele vya
kulifanya Shirika hili kutekeleza kazi zake kama ilivyokusudiwa.
Upande
wake Mwenyekiti wa Caritas-Tanzania, Askofu Mkuu Yuda Thaddeus Ruwa’ichi alisema Kanisa la
Tanzania linaheshimu kazi nzuri inayofanywa na shirika hilo na kwamba kama kuna
mapungufu, basi sula hilo litajadiliwa kwenye vikao mbalimbali vya maaskofu ili
yaweze kufanyiwa kazi, hivyo kuendeleza ustawi mzuri kwa manufaa ya jamii,
Kanisa na Taifa kwa ujumla.
“Kama
maaskofu tupo bega kwa bega na Caritas, tunaitambua na kuthamini kama chombo
chetu cha kuihudumia jamii… ni kweli changamoto zipo, lakini hili ni jambo
linaloendelea kufanyiwa kazi na masuala mengine yatajadiliwa kwenye mikutano
mbalimbali ya maaskofu,” alisema.
Katibu
Mtendaji Caritas- Afrika, Bw. Albert Mashika, ametoa wito kwa shirika hilo
upande wa Tanzania kuwa na mpango mkakati
wenye kulenga kutekeleza shughuli mbalimbali za kijamii, ambapo hata
hivyo mkakati huo usitofautiane sana na
ule wa CARITAS Afrika uliopangwa kutekelezwa ndani ya kipindi cha miaka mitano
, kuanzia 2019-2023. “Kwenye mkakati wenu pia lazima muwe na vipaumbele na
kuvifanyia kazi kwa wakati,” alisema.
Katibu
Mtendaji wa Caritas- AMECEA, Padri Paul
Igweta, kwa upande wake alisema, kama chombo cha Kanisa, shughuli za Caritas
zinategemeana, hivyo kufanya vizuri kwa Caritas Tanzania si tu ni mafanikio ya
TEC, bali pia ni mafanikio ya AMECEA, Caritas Afrika na hata Caritas
Internationalis, hivyo akaomba ushirikiano
ili lengo hili litimie.
Timu
hii ya Caritas Internationalis, Afrika na AMECEA ilifanikiwa kukutana na
watendaji wa Caritas Tanzania, ambapo
ambapo pamoja na mambo mengine walifanikiwa kubadilishana uzoefu wa
kiutendaji, kujua maendeleo ya Catitas Tanzania na changamoto zake pamoja na
kuweka mkakati wa kuzitatua.
Comments
Post a Comment