Maaskofu Afrika na Madagaska wahitimisha miaka 50 ya SECAM
SHirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Afrika na
Madagascar, SECAM, limehitimisha Maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 50 tangu
kuanzishwa kwake.
Kilele cha maadhimisho
hayo kimefanyika July 28 mwaka 2019 kwa
Ibada ya Misa Takatifu iliyoadhimishwa kwenye Madhabahu ya Mashahidi wa Uganda,
Namgongo, Kampala- Uganda.
Maadhimisho hayo
yameongozwa na kauli mbiu “Kanisa, familia ya Mungu Barani Afrika; Sherehekea
Jubilei yako! Mtangaze Kristo Yesu Mkombozi wako”.
Katika hitimisho la
maadhimisho hayo maaskofu wa SECAM wakiwemo takribani maaskofu saba kutoka
Tanzania kwa pamoja wametoa maazimio kwa
ajili ya kuendelea kuimarisha imani kwa waamini Afrika na Madagaska.
katika Ujumbe wao kwa Watu wa Mungu Barani
Afrika na Madagaska, maaskofu hao
wanakazia umuhimu wa Jubilei kama muda wa kushukuru, muda wa kujenga
umoja wao na kupanga yaliyo mbeleni kwa umoja na mshikamano.
Ujumbe kwa familia ya
Mungu Barani Afrika na Madagaska unaoongozwa na kauli mbiu ‘Na uzima wa milele
ndio huu: wakujue wewe, ili wawe na uzima, kisha wawe nao tele’ (Yoh. 13:3:
10:10).
Maaskofu wa SECAM
wameambatanisha pia mwaliko kwa familia ya Mungu kujidhatiti zaidi katika
imani, kwa kuendeleza toba na wongofu wa ndani.
Pia wanaendelea kuboresha
“Hati ya Kampala” itakayotoa dira na mwelekeo wa Kanisa Barani Afrika kwa siku
za usoni.
Waamini wawekeze katika Maandiko Matakatifu
Wametoa wosia unaopaswa
kuzingatiwa na familia ya Mungu katika ujumla wake kwa kukazia masuala
mbalimbali ikiwemo; Kanisa Barani Afrika kuwekeza zaidi katika Maandiko
Matakatifu, Taalimungu, Maadili, Malezi na maisha ya kiroho kwa waamini Barani
Afrika.
Waendelee kuboresha
maisha yao ya kiroho kwa njia ya tafakari ya Neno la Mungu na ushiriki
mkamilifu wa Sakramenti za Kanisa, ili kusaidia mchakato wa kumwilisha tunu
msingi za Kiinjili katika uhalisia wa maisha ya waamini.
Watakatifu na mashuhuda
wa imani kutoka Barani Afrika, wawe ni mfano bora wa kuigwa kwa kujikita katika
imani yao bila kuyumbishwa.
Waamini wa Kanisa
Katoliki wawe makini na sera na mikakati inayosigana na imani, kanuni na
maadili ya Kanisa Katoliki.
Kanisa liimarishe jumuiya Ndogondogo za
Kikristo
Maaskofu wa SECAM wanawataka waamini kuhakikisha
kwamba, wanashiriki kikamilifu katika maisha na utume wa Jumuiya ndogo ndogo za
Kikristo ambazo ni utambulisho wa Kanisa kama familia ya Mungu inayowajibika
Barani Afrika.
Waamini wahamasike
kujiunga na vyama na mashirika ya kitume, ili kulea na kukuza imani yao kwa
Kristo Yesu na Kanisa lake, na kama sehemu ya ushiriki wao mkamilifu katika
ujenzi wa Kanisa.
Utume wa familia
unapaswa kuimarishwa ili kweli familia ziweze kuwa ni chombo na shuhuda wa
unabii katika jamii.
Kuna haja kwa Kanisa
Barani Afrika kuendelea kujidhatiti zaidi na zaidi katika maadili na katika
maisha ya kiroho kwa kuhakikisha kwamba, watoto na vijana wanarithishwa tunu
msingi za kiinjili, kimaadili na utu wema, kuanzia kwenye familia zao, ili
kuwakinga na uwezekano wa kuingizwa katika misimamo mikali ya kidini na
kiimani; fujo na ghasia mbali mbali.
Kanisa litumie kwa makini maendeleo ya sayansi na teknolojia
Familia ya Mungu Barani
Afrika inahimizwa kutumia kwa umakini mkubwa maendeleo ya sayansi na teknolojia
ya mawasiliano ya jamii.
Wanakumbusha kwamba, hata njia za mawasiliano
ya jamii zinapaswa kuinjilishwa pia.
Wamegusia umuhimu wa
uekumene: wa damu, maisha ya kiroho, sala na huduma makini kwa watu wa Mungu
Barani Afrika sanjari na majadiliano ya kidini ili kujenga na kudumisha misingi
ya haki, amani na maridhiano kati ya watu wa Mataifa.
Kanisa Afrika, Madagaska lishikamane na
viongozi wa siasa
Kanisa Barani Afrika
halina budi kuendelea kushirikiana na kushikamana na viongozi wa kisiasa, kuwasaidia
kuwajibika zaidi, ili kutafuta na kudumisha: ustawi, maendeleo na mafao ya watu
wa Mungu Barani Afrika.
Rasilimali na utajiri
wa Bara la Afrika uwe ni kwa ajili ya kuchochea mchakato wa maendeleo fungamani
ya binadamu yanayofaidisha watu wote, daima misingi ya haki, amani na
maridhiano kati ya watu, ikipewa kipaumbele cha kwanza.
Serikali Barani Afrika
hazina budi kujipanga kikamilifu ili kukabiliana na mambo yanayosababisha wimbi
kubwa la wakimbizi na wahamiaji kutoka Barani Afrika. Sera na mikakati hii
isaidie pia kuzuia na kudhibiti biashara ya binadamu na utumwa mamboleo Barani
Afrika.
Wanalitaka Shirikisho
la Mashirika ya Kitawa na Kazi za Kitume Barani Afrika, COMSAM, kuishi kweli za
wito wake, kwa kuwa ni chombo na shuhuda wa uinjilishaji. Katika Majimbo ambayo
kuna uhaba mkubwa wa Mapadri hasa Kaskazini mwa Bara la Afrika, uwepo utaratibu
wa kupeleka wamisionari watakao tangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu,
jambo la msingi yawepo mawasiliano na Kanisa la Kiulimwengu.
Wamekazia kwa namna ya
pekee malezi ya wakleri na watawa Barani Afrika, ili kuhakikisha kwamba,
wanajenga na kudumisha mahusiano na Kristo Yesu.
Wanawataka waamini
kukazia ukomavu wa maisha ya kiroho, kiutu. Wajenge na kudumisha ndani mwao ari
na mwamko wa huduma kwa watu wa Mungu; daima wakiwajibika mbele ya Mungu na
Kanisa.
Waendelee kujitioa
sadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya Kristo na Kanisa lake Barani Afrika.
Waamini walei
wanakumbushwa kwamba, wameitwa na kutumwa kuyatakatifuza malimwengu kwa njia ya
chachu ya tunu msingi za kiinjili.
Kila kaya inasisitizwa
kuwa na Biblia Takatifu, Katekesimu ya
Kanisa Katoliki pamoja na Mafundisho Jamii ya Kanisa Katoliki.
Makanisa mahalia
yaendelee kujibidisha kutoa malezi makini kwa wafanyakazi wa umma pamoja na
wanasiasa, ili kupambana na rushwa, ufisadi wa mali ya umma pamoja na
mmong’onyoko wa maadili na utu. Kanisa liendelee kukazia misingi ya utawala
bora pamoja na matumizi sahihi ya rasilimali na utajiri wa nchi husika.
Wakristo Barani Afrika
wajitahidi kujenga na kudumisha umoja na udugu wa kibinadamu; washirikiane na
kushikamana kupambana na: magonjwa, umaskini na ujinga maadui wakubwa wa
maendeleo Barani Afrika.
Huduma ya kichungaji na
maisha ya kiroho kwa wafanyakazi wa sekta ya afya bado ni muhimu sana. Juhudi
hizi hazina budi kwenda sanjari na utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote.
Wataalam na wasomi
Barani Afrika waendelee kufanya tafiti na kuzichapisha kuhusu: Dini asilia
Barani Afrika, Uislam, Madhehebu ya kidini yanayoendelea kuibuka kila kukicha, jamii
za kisiri pamoja na matatizo na changamoto zinazoibuliwa na imani za
kishirikina. Mwishoni, wanawataka wadau mbali mbali wa vyambo vya mawasiliano
ya jamii kuhakikisha kwamba, wanasaidia kueneza uelewa wa SECAM katika maisha
na utume wa Kanisa Barani Afrika.
Tamko la Kampala,
likisha kutolewa litakuwa ni dira na mwongozo wa maisha na utume wa Kanisa
Barani Afrika.
Hati hii ikisha
kutolewa iendelee kusambazwa sehemu mbali mbali za Bara la Afrika.
Comments
Post a Comment