Kardinali Pengo atimiza miaka 75, atoa neno kuhusu kustaafu
WAAMINI
nchini wametakiwa kutambua kuwa kutimiza umri wa miaka 75 ya kuzaliwa siyo
kigezo pekee cha kustaafu nafasi ya uaskofu kwa maaskofu wa Kanisa Katoliki,
bali mwenye ruhusa ya kutoa kibali cha kufanya hivyo ni Baba Mtakatifu pekee.
Angalizo hilo limetolewa na Askofu Mkuu wa
Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo,
wakati wa Misa Takatifu ya Kutabaruku
Kanisa na Altare, katika Parokia ya Mtakatifu Augustino Salasala jimboni humo.
Kardinali Pengo ambaye alitoa kauli hiyo siku
moja kabla ya kutimiza umri wa miaka 75 ya kuzaliwa, alisema askofu yeyote
hawezi kujiamria kustaafu kwa kigezo kwamba ametimiza wa umri, bali atafanya
hivyo kwa kuruhusa ya Baba Mtakatifu ambaye ndiye kiongozi Mkuu wa Kanisa
Katoliki Duniani.
“Lakini askofu anaweza kuomba kwa Baba
Mtakatifu ampumzishe kusimamia kazi za jimbo anapotimiza umri wa miaka 75 na
kama yeye (Papa) hajakwambia ustaafu basi utaendelea na majukumu yako kama
kawaida,” alisisitiza.
Aliongeza “ Mimi binafsi nimetumikia nafasi
ya uaskofu kwa kipindi cha miaka 35… ni kipindi kirefu na tayari
nimeishamjulisha Baba Mtakatifu kuwa kesho (Agosti 5, 2019) natimiza miaka 75 ya kuzaliwa… hivyo
niendelee ama nisiendelee kulitumikia
Kanisa katika nafasi yangu, hilo ni jukumu la Baba Mtakatifu mwenyewe.”
Sanjari na hilo, Kardinali Pengo
aliwapongeza waamini wa Parokia hiyo ya Mtakatifu Augustino, Salasala, kwa moyo
wa majitoleo ambapo wamefanikisha ujenzi wa Kanisa kwa nguvu zao wenyewe, jambo
linalotakiwa kuigwa na waamini wa Parokia nyingine.
“Kujitolea kwa michango mbalimbali ikiwemo
ya kifedha hadi kukamilisha ujenzi wa Kanisa hili ambalo ni kubwa na zuri na ujenzi wake kuchukua muda mfupi,
ni ishara ya nje ambayo inapaswa kudhihirisha roho iliyo ndani mwenu ambayo imejaa upendo na mshikamano,” alisema.
Aliongeza “Tungeweza kukaa hata chini ya
mkorosho na kuabudu…lakini kwa vile mwanadamu ni mwili na roho, ndiyo maana
tumeweza kufanya ujenzi kama huu… hii ni udhihirisho wa upendo mlionao kwa
Mungu na si kwetu tu kama Wakristo Wakatoliki, lakini hata kwa wasiyo
Wakatoliki,” alisema.
Hata hivyo alisema, kukamilika kwa kazi
hiyo ya ujenzi wa Kanisa si mwisho wamejitoleo kwa waamini hao wa Salasala,
bali ni mwanzo wa kuendelea kujitolea zaidi ili kazi ya Mungu iendelee kusonga
mbele.
Akielezea maana halisi ya kutabaruku Kanisa
na Altare, Kardinali Pengo alisema “ hii ni kwamba mahali hapa hata kama
tunatamani pawe ukumbi wa kufanyia mkutano au biashara nyingine… kwa sasa baada
ya kutabarukiwa, mahali hapa patatumika kwa ajili ya shughuli za Kiibada tu
kuanzia leo na hata milele,si shughuli nyininezo,”.
Naye Paroko wa Parokia hiyo, Padri Peter
Assenga, CSSp, aliwashukuru wanaparokia na timu ya wataalam, waliojitolewa kwa
namna ya pekee kuhakikisha ujenzi huu unakamilika kwa ufanisi tena ndani ya muda
mfupi, hivyo akwaomba waendelee na moyo huu wa majitoleo.
Ujenzi wa jengo hilo la Kanisa la Mtakatifu
Augustino Salasla ulianza rasmi Novemba 2015 chini ya Padri Greogory Mallya,
CSSp ,(aliyekuwa Paroko kwa kipindi hicho) na kwa mujibu wa Mwenyekiti wa
Kamati ya Ujenzi, Bibi Frola Minja, sehemu kubwa ya ujenzi huu imechangiwa na
waamini wenyewe.
Parokia ya Mtakatifu Aigustino Salasala
ilitangazwa rasmi na Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo, mnamo
Agosti 15 mwaka 2004 na kabla ya hapo ilikuwa na moja ya vigango vya Parokia ya
Mtakatifu Nicholaus Mtongani.
Comments
Post a Comment