‘Magufuli anatekeleza ndoto za Nyerere’

Na Dalphina Rubyema
IMEELEZWA kuwa kazi nzuri inayotekelezwa na Serikali ya Awamu ya Tano, ni utekelezaji wa dira na ndoto za Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, ambaye enzi wa uhai wake alitamani kuona Tanzania inainua uchumi wake kwa kutumia raslimali zilizopo nchini na hasa sekta ya viwanda.
Hayo yamebainishwa na mwanadiplomasia na wanasiasa mkongwe nchini, Balozi Nicholaus Alfred Kuhanga, katika mahojiano maalum na KIONGOZI, yaliyofanyika jijini Dar es Salaam katikati ya juma, ambapo alisema, ndoto ya Mwalimu Nyerere ilikuwa ni kuona Tanzania inakuwa miongoni mwa nchi zenye maendeleo ya hali ya juu barani Afrika na dunia  kwa ujumla, hivyo kuondoka kwenye kundi la chi tegemezi.
Baba wa Taifa katika kutimizi ndoto yake hiyo, kwa mujibu wa Balozi Kuhanga ambaye alifanikiwa kufanya kazi  chini ya utawala wa Mwalimu Nyerere kwa nyadhida mbalimbali ikiwemo ya Uwaziri, Ubalozi na Umakamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), alihakikisha nashirikisha watu kwenye michakato wa kimaendeleo ili hata kama atamaliza uongozi wake kabla hajafikia ndoto alizokusudia, basi wanaobaki waendelee kusukuma gurumu hilo la maendeleo.
Balozi Kuhanga hakusita kuzipongeza juhudi zinazofanywa na Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Rais John Magufuli, kuwa zimetekeleza kwa vitendo ndoto na mipango ya Mwalimu, ambayo kwa namna moja ama nyingine hazikupewa kipaumbele baada ya kung’atuka kwakwe.
 “Watanzania tunaweza kujivunia kwani sasa urithi aliotuachia umeanza kutekelezwa kwa vitendo…kwani tunachokiona kinafanyika leo ni mawazo na mipango aliyoiacha Mwalimu Nyerere na kilichokuwa kinafanyika kipindi cha nyuma ni kuyapuuzia na kuyaweka kapuni,” alisema.
Aliongeza “mfano mzuri  ni hili suala la viwanda ambalo mimi naweza kusema kwamba nalo ni wazo la Mwalimu  na ndiyo maana wakati wa uongozi wake, alifanikiwa kuanzisha viwanda vingi ambavyo vilikuwa ninaendeshwa kwa malighafi zilizopatikana nchini, hivyo ilikuwa ni motisha kwa wakulima na  makundi mengine kwani walikuwa na uhakika wa kupata masoko ya kile wanachokizalisha… baadaye viwanda vingi vilikufa,’.
Hata hivyo katika kuzidi kutekeleza kwa vitendo mawazo ya Mwalimu, Balozi Kuhanga alishauri serikali na wadau wengine, kuhakikisha wanawashirikisha watu katika mipango ya maendeleo  kwani kwa kufanya hivyo kutawasaidia kutekeleza kile wanachokifahamu tangu mwanzo.
Sanjari na hayo, Balozi huyo Mstaafu pia alishauri vyombo vilivyoshikiria madaraka, kuhurusu nafasi ya mazingumzo pindi kunapojitokeza hali ya kutokuelewana, kwa kufanya hivyo kutaepusha migogoro ambayo wakati mwingine inaweza kusababisha uvunjifu wa amani vikiwemo vifo vya watu wasiokuwa na hatia.
“Tuige mfano wa Mwalimu kwani alijiuliza na kupima  madhara yanayoweza kujitokeza endapo atakubali kuingiza nchi yake kwenye migogoro ikiwemo ya kivita na alipojitafakari na kupata majibu basi alikuwa radhi kutoa ushauri wake ili migogoro hiyo imalizika kwa amani kupitia pande husika kuketi meza moja na kufanya mazungumzo,” alisema.
“Nakumbuka aliwahi hata kuingiria mgogoro wa mafuta nchini Iraq na Umoja wa Mataifa (UN) kuhusiana na mgogoro wa mafuta… pia alikuwa ni kiungo cha upatanishi si tu ndani ya nchi yake, bali pia kwa nchi za Bara la Afrika  ambapo daima alisisitiza kutumia mazungumzo kama njia nzuri ya kuepusha migogoro badala ya kuingia katika mapigano ya kivita,’ alisema.
Kutokana na ushawishi aliokuwa nao, Mataifa ya Afrika yalimwamini na  yalimutumia Mwalimu kuwa msemaji wao kwenye   mikutano ya Kimataifa.
Hata hivyo Balozi Kuhanga alisema, katika uwakilishi huo, Mwalimu alikuwa makini na mwenye msimamo wa kuchambua kile alichokuwa akienda kuwakilisha kwenye mikutano hiyo na kwamba, endapo angebaini kuwa ujumbe aliopewa hauna lengo la kujenga badala yake ni kubomoa ambako matokeo yake yangesababisha uvunjifu wa amani, basi hakuwa tayari kufanya uwakilishi huo.
Katika kuendelea kumwenzi Baba wa Taifa, Balozi Kuhanga amesisitiza suala la kila mmoja kujituma kwa kufanya kazi kwa bidii pamoja na ngazi za utawala kuheshimu mawazo ya kila mmoja pamoja na kuwashirikisha watu katika mipango ya maendeleo.
Mwalimu Julius Kambare Nyerere alizaliwa Aprili 13 mwaka 1922 katika kijiji cha Butihama mkoani Mara na katika uhai wake amefanikiwa kulitumikia Taifa katika nyadhifa mbalimbali,  ambapo mwaka 1961-1964 alikuwa Waziri Mkuu wa Tanganyika kabla hajawa Rais wa Awamu ya Kwanza wa serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, wadhifa alioushika tangu mwaka 1964-1985 alipong’atuka.
Mwalimu Nyerere ambaye Tanzania imempa hadhi ya kuwa Baba wa Taifa, kitaaluma akiwa ni Mwalimu, alifariki duniani Oktoba 14 mwaka 1985 katika Hospitali ya St. Thomas, London Uingereza  alipokuwa amelazwa kutokana na kansa ya damu.


Comments

Popular posts from this blog

SALA YA ASUBUHI:SALI HIVI..

Ujio wa Wamisionari wa Kwanza Tanzania Bara (2)

MJUE MTAKATIFU MARIA GORETTI