Paroko: Wakeketeni watoto kiimani siyo kimwili
|
PAROKO wa Parokia ya Sirari katika Jimbo
Katoliki la Musoma, Padri Erenest Kamugisha amesema umefika wakati sasa jamii
ikawakeketa watoto na vijana kiimani ili wawe waamini na raia wema, badala ya
kuwakeketa kimwili hali inayowapa mateso.
Kwa msingi huo amesema,
mabadailiko ya waamini kuachana na sherehe zinazohusu ukeketaji na kuhamia
katika sherehe za kikanisa kama Ubatizo, yatasaidia kuondoa uhalifu na ukatili
kama mauaji katikajamii na kuwaongezea uhusiano na Mungu.
Aidha, amewasisitiza Wakristo
kuacha vitu na mambo ya anasa kwa kuwa yanawafanya watu kumchukiza Mungu kwa
mambo mbalimbali ya hatari kimwili na kiroho kama mauaji, utoaji mimba, utekaji
watoto, wizi, ushoga na usagaji.
Ukeketaji wa kimwili ni ukatili
ambao wamekuwa wakifanyiwa baadhi ya wanawake na watoto wa kike katika jamii
kadhaa nchini huku ukitajwa kama hatari kwa afya na kisaikolojia kwa wahusika.
Padri Kamugisha alisema hayo hivi
karibuni wakati akitoa Sakramenti za Ubatizo na Komunio ya Kwanza kwa waamini
zaidi ya 70, katika Misa Takatifu iliyofanyika katika Senta za Sirari na Pemba
za Kigango cha Nyabitocho parokiani Sirari.
“Tumefikia hatua hatuwezi
kumaliza wiki bila kusikia tukio mojawapo kati ya hayo, hivyo inatubidi tusali
kumuomba Mungu aweze kuingilia kati maana zamani watu ndio walikuwa wanaogopa
fisi na samba, lakini sasa mwanadamu amegeuka kuwa chui na simba na anaogopwa
sana; ni heri kupita ndani ya hifadhi
ukakutana na wanyama wakali kuliko mwanadamu
maana amekuwa mwovu zaidi,” alisema.
Hata hivyo, paroko huyo
aliwapongeza waamini wa eneo hilo kwa kuanza kubadili mtazamo mintarafu suala
la kuwafanyia sherehe watoto wao wanapopokea sakramenti mbalimbali ndani ya
Kanisa kama Ubatizo, Komuniyo na Kipaimara badala ya kuwafanyia sherehe wakati
wa ukeketaji ambao ni ukatili wa kijinsia.
“Niniwapongeza kwa moyo wa dhati
kabisa kutokana na mabadiliko ninayoyaona maana zile sherehe mlizokuwa
mnazifanya wakati wa ‘salo’ (ukeketaji) sasa zihamishieni kanisani wakeketeni
watoto kiimani kama mlivyofanya sasa,” amesema Padri Kamugisha.
Mmoja wa waamini waliopokea
sakramenti katika tukio hilo, Anastazia Joseph alisema anamshukuru Mungu kwa
kumfikisha katika hatua hiyo aliyoitamani kwa muda mrefu.
Alimshukuru pia Padri Kamugisha
kwa kukubali kuwapatia sakramenti katika misa iliyofanyika katika kigangoni
Nyabitocho katika Parokia ya Sirari.
Nao wasimamizi wa watoto hao na
viaana waliopata sakramenti wameahidi kuwalea watoto katika misingi
inayompendeza Mungu ikiwa ni pamoja na kuwatembelea mara kwa mara na
kushirikiana nao katika shughuli mbalimbali za kiimani.
Comments
Post a Comment