Waliosoma Chanjale seminari wamuunga mkono Askofu Kimaryo kuendeleza jimbo
Wanamalezi
wote waliosoma katika seminari ya Chanjale tokea ilipoanzishwa wameungana na
Askofu wa Jimbo Katoliki Same Mkoani Kilimanjaro Mhasham Rogathy Kimario
kuendeleza utume katika jimbo hilo.
|
Awali walianza kujumuika katika hija ya kusali njia ya msalaba siku ya
Ijumaa Kuu kwa kupandisha mlima kuanzia Njoro hadi Chuo cha Malezi Dido ambapo
wanafunzi wanapata elimu ya awali ya sekondari (pre-form one) kabla ya kuingia
kidato cha Kwanza huko Chanjale Seminari wilaya ya Mwanga Kilimanjaro.
Kwenye hija wanamalezi hao
waliosoma katika Seminari hiyo miaka ya 1983 hadi 2015 wameahidi kumuunga mkono
Askofu Kimaryo katika kulipeleka mbele
jimbo Katoliki Same.
Wanamalezi hao wakiongozwa na Ndg Karol Kadeghe na Goodluck Kavugha walimkabidhi Askofu Kimaryo Television moja
kama zawadi kwa watoto wanaosoma katika Chuo cha Malezi Dido, vazi la Askofu la
kuendeshea ibada na kumuonesha ujenzi wa vyoo na mabafu ya kisasa ambao wanaujenga kwaajili ya
wanafunzi hao na yatakabidhiwa mara tu baada ya kukamilika hivi karibuni.
Akipokea zawadi hizo Askofu Rogathy kwa kuonesha uso wa furaha mbele ya waamini amesema kuwa, hakosi
kutoa machozi ya furaha kila anapoona mambo mazuri yanafanyika. Amewashukuru
kwa kujitolea kuendeleza seminari hiyo na kuwa wazalendo wa Seminari ya
Chanjale iliyowafanya wawe kama walivyo leo.
“Hii ni imani na moyo wa ukarimu kwa wadogo zenu. Ninawashukuru sana,”
amesema Askofu Kimaryo.
Pia amewaomba wanamalezi hao kumsaidia kujenga ukumbi wa Seminari ya
Chanjale kwa ajili ya mahitaji mbalimbali ombi ambalo lililopokelewa kwa mikono
miwili na wanamalezi hao.
Aidha,
wanamalezi hao wamewekeana mikakati mbalimbali ambayo wataifanya ili kutimiza
majukumu la kulipeleka Jimbo la Same Mbele kwa kushirikiana na Askofu wa jimbo
hilo, mapadri, watawa na waamini.
Mratibu Mkuu wa Kikundi hicho Gudluck Kavunga amewaasa wote waliosoma
katika Seminari ya Chanjale kuunga mkono jitihada za kundi hilo ili kuendeleza
elimu jimboni Same na kuwasaidia wanafunzi wanaosoma Dido na Chanjale seminari
kutimiza ndoto zao kama wao walivyofanikiwa.
“Kutoa ni kupokea, kutoa ni moyo si utajiri. Yule mwenye ujuzi wowote,
kipaji, fedha, mali yoyote itakayofaa kuiendeleza Chanjale na Dido
anakaribishwa kushirikiana na kikundi hiki cha Chanjale Alumni kwa ajili ya
maendeleo ya jimbo letu.
Zamani tulikuwa na wafadhili kutoka ndani na n je ya nchi lakini sasa
hatuna wafadhili wa nje. Wafadhili wa maendeleo ya Same ni sisi wenyewe. Tuwe
wamisionari kweli kwa vitendo kwa ajili ya uinjilishaji wa nyakati zetu hasa
wakati huu Kanisa Katoliki nchini linaposherehekea Jubilei ya Miaka 150 ya
Uinjilishaji. Tutimize wajibu wetu kama wakristo wa Kanisa Katoliki,”
amesisitiza.
Kwasasa kikundi hicho cha wanamalezi kina watu 200 ambapo awali walikuwa
wakiwasiliana na kupanga mambo yao kupitia mitandao ya kijamii na mikutano
mbalimbali.Wamewataka wanamalezi wazawa na wasio wazawa ambao hawajajiunga nao
wajiunge ili washirikiane kwenye shughuli mbalimbali kwaajili ya maendeleo ya
jimbo la Same na kwaajili ya maendeleo ya Kanisa la Mungu kwa ujumla (uinjilishaji wa kina).
Comments
Post a Comment