Padri Mtui afariki kwa ajali Shinyanga
Na Joachim Mahona,
Shinyanga
Waselesiani
wa Mtakatifu Yohane Bosco na Jimbo Katoliki Shinyanga wamepata simanzi baada ya
Padri Richard Stanslaus Mtui kufariki
dunia baada ya gari alilokuwa akisafiria kugongana uso kwa uso na Lori la
mizigo huko mkoani Singida.
Padri
Mtui alikuwa
ni Gombera wa shule ya Sekondari ya Don Bosco Didia, inayomilikiwa na Waselesiani
wa Mtakatifu Yohane Bosco iliyopo Didia
katika Wilaya ya Shinyanga.
Kwa
mujibu wa taarifa za kipolisi na zile zilizotolewa na msaidizi wake Padri
Mathias Isaka ambaye ni Mkuu wa seminari hiyo ndogo, Padri Mtui amefariki dunia
majira ya saa saba usiku, kuamkia Ijumaa kuu baada ya gari alilokuwa akisafiria aina ya Toyota
Noah lenye namba za usajili Z463 GH
kugongana uso kwa uso na lori la mizingo
lenye namba T9992 DLN aina ya Scania mali ya kampuni ya BHANJI lililokuwa likitokea Dar-es-salaam kuelekea
Burundi katika eneo la Kyengege wilaya ya Iramba mkoani Singida barabara kuu ya
Mwanza Dar es salaam.
Taarifa
zaidi zinaeleza kuwa dereva wa Noah aliyokuwa amepanda marehemu padre Mtui kutoka Singida
alikuwa akiendesha kwa mwendo kasi, kiasi kwamba alipoteza uelekeo baada ya kukuta gari aina ya fuso likiwa
limeegeshwa kandokando ya barabara. Wakati
akijaribu kuikwepa alikutana na lori hilo ambalo aligongana nalo uso kwa uso na
kusababisha kifo cha Padre Mtui papo hapo na mtu mwingine aliyekuwa amepanda kwenye
Noah hiyo alijeruhiwa vibaya ambapo amevunjika mikono na miguu yote. Dereva
wa Noah alifanikiwa kukimbia baada ya ajali hiyo kutokea.
Padre
Mathis amebainisha kuwa marehemu Padri Mtui aliwaaga siku ya Jumatatu yaani
Machi 26, 2018 kuwa anakwenda Moshi Mkoani Kilimanjaro kwa ajili ya kuadhimisha
misa ya maziko ya mama yake mkubwa ambayo ilikuwa ifanyika Jumanne yaani Machi
27, 2018.
Baada
ya maziko, siku ya Alhamisi Machi 29, 2018 alikwenda mpaka Arusha akitokea Moshi. Akiwa
Arusha siku hiyo aliondoka majira ya saa kumi
jioni kwa gari binafsi ambalo
lilimfikisha mpaka Singida ambapo alipanda gari hilo la Noah kuja Shinyanga kwa lengo la kuwahi kuja kuadhimisha Ibada ya
Ijumaa Kuu.
Akizungumza
huku akibubujikwa na machozi Padri Mathias amefafanaua kuwa alipata taarifa kuwa Padre Mtui amefariki kwa
ajali ya gari kutoka kwa Padri wa shirika lao aliyeko Iringa siku ya Ijumaa Kuu
mchana wakati akijiaandaa kwenda Tinde kwa ajili ya adhimisho la Ibada ya
Ijumaa Kuu.
Padri
huyo alimweleza kuwa alipigiwa simu na askari aliyeangalia namba katika simu ya
marehemu baada ya ajali kutokea. Aliendelea kusema kuwa, baada ya kupata
taarifa hizo yeye pamoja na watu wengine kadhaa walifunga safari ya kwenda
Singida. Walipofika walikwenda moja kwa moja
katika kituo cha polisi na baadaye Maaskari walimpeleka katika hospitali ya Kiomboi ili kuutambua mwili
wa marehemu na kuthibitisha kuwa ndie
yeye.
Misa
ya kuuaga mwili wa marehemu Padre Mtui imefanyika Aprili 3, 2018 na ikiongozwa
na Mhashamu Askofu Liberatus Sangu wa Jimbo Katoliki Shinyanga.
Ibada
hiyo ilifanyika katika Viunga vya shule ya Sekondari Don Bosco - Didia na kuhudhuriwa
na Mapadri, Watawa, Viongozi wa Serikali, Viongozi wa vyama vya siasa, Wafanyakazi
wa shule hiyo, Waamini, Wanafunzi na
watu wote wenye mapenzi mema.
Katika
misa hiyo, Askofu Sangu amewataka watu wote waendelee kumwombea Padri Mtui ili
aweze kuyafikia aliyokuwa akiyaadhimisha na kuyatumainia.
Askofu
Sangu amesema kuwa, Kanisa limempoteza padri kijana ambaye alikuwa mahili wa
kazi. Aliwasisitiza Wakristo daima kujiweka tayari wakati wote na kutotetereka kiimani pale misiba au matatizo
yoyote yanapotokea, kwa kuwa kifo ni
njia na mlango wa kwenda kule ambako Kristo ametuahidia sote.
Kwa
upande wake Mkuu wa Shirika hilo katika Ukanda wa Afrika Mashariki Padri Simon
Asira amewashukuru watu wote kwa namna walivyoshiriki tangu kutokea kwa kifo
hicho.
Amewaomba
kuendelea kumtumainia Mungu ambaye amependa kumwita kwake Padri Mtui na kwamba
pamoja na kifo chake Shirika hilo
litaendelea kuwepo na kutoa huduma za kielimu na nyinginezo kama kawaida katika
jamii.
Mwili
wa marehemu Padre Richard Mtui ulisafirishwa kwenda Moshi mkoani Kilimanjaro April 4, 2018 kwa ajili ya maziko ambayo yamefanyika Aprili 5, 2018 katika eneo la
nyumba ya malezi ya Shirika iliyoko huko Moshi.
Marehemu
Padri Richard Mtui amezaliwa Juni 19 mwaka 1977 katika kijiji cha Mbahe bondeni
wilayani Marangu mkoani Kilimanjaro.
Baada ya kumaliza malezi katika nyumba za malezi za Shirika la Mtakatifu
Yohane Bosco katika Novitiate huko Nairobi Kenya na Ethiopia. Baada ya masomo yake
ya Falsafa na Theolojia alifunga nadhiri za daima mnamo Agosti 16 mwaka 2009.
Alipewa
Daraja Takatifu la Ushemasi Mei 8 mwaka 2010 na baadaye Julai 21 Mwaka 2011 alipewa
Daraja Takatifu la Upadri.
Baada
ya kupewa Daraja la Upadri alipangiwa kwenda kufanya kazi katika shule ya Sekondari
Don Bosco iliyoko Embu nchini Kenya na baadaye Julai mwaka 2016 aliteuliwa kuwa
Mkuu wa nyumba Jumuiya ya Shirika Didia na Gambera wa shule ya Sekondari Don
Bosco - Didia jimboni Shinyanga mpaka mauti yalipomkuta.
Roho
ya Marehemu Padri Richard Mtui ipate rehema kwa Mungu ipumzike kwa amani.
Amina.
Such unforgettable tragedy. RIP my school mate.
ReplyDelete