Papa akutana na Baraza la Maaskofu Katoliki Nigeria
Baraza la
Maaskofu Katoliki Nigeria, kuanzia Aprili 24-30, 2018 linafanya hija ya kitume
mjini Vatikani kwa kukutana na kuzungumza na Baba Mtakatifu Fransisko pamoja na
waandamizi wake.
Hii ni
hija ambayo kadiri ya sheria kanuni za Kanisa hufanyika walau kila baada ya
miaka mitano! Kanisa Katoliki nchini Nigeria linaundwa na Majimbo makuu 9 na
chini yake kuna majimbo 45.
Ni
Kanisa ambalo bado ni changa, lakini linakabiliwa na changamoto, matatizo na
fursa katika maisha na utume wake wa kumtangaza na kumshuhudia Kristo Yesu
aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu!
Uongozi mbaya, rushwa na ufisadi wa mali ya
umma; ukabila, udini na misimamo mikali ya kiimani ni kati ya mambo
yanayoendelea kusababisha vita, kinzani na mipasuko ya kijamii na kidini sehemu
mbali mbali za Bara la Afrika, lakini Nigeria kwa namna ya pekee kabisa!
Wanaigeria ni watu wa dini na kwamba, imani ni sehemu muhimu sana ya
utambulisho na maisha yao. Sehemu kubwa ya wananchi wa Nigeria ni waamini wa
dini ya Kiislam na Kikristo.
Takwimu
zinaonesha kwamba, kuna Wakristo milioni 70 na kati yao Wakatoliki ni waamini
milioni 26. Kwa bahati mbaya, ukabila na udini usiokuwa na mashiko ni kati ya
mambo yanayowatafuna na kuwanyong’onesha sana wananchi wa Nigeria. Inasikitisha
sana kuona kwamba, udini na ukabila umetumiwa sana kuwagawa wananchi wa Nigeria
hata katika masuala ya kiuchumi, kisiasa na kijamii. Kikundi cha kigaidi cha
Boko Haramu katika miaka ya hivi karibuni kimekuwa ni chanzo kikuu cha maafa na
mauaji ya watu wasiokuwa na hatia. Kimesababisha uharibifu mkubwa wa miundo
mbinu ya shule, huduma ya afya na barabara.
Takwimu
zinaonesha kwamba, tangu mwaka 2006 hadi wakati huu, wakristo waliouwawa
kutokana na misimamo mikali ya kidini nchini Nigeria ni zaidi ya waamini 13,
000. Watu milioni 1.5 wamelazimika kuyakimbia makazi yao kwa kuhofia usalama wa
maisha na mali zao. Kikundi cha Boko Haramu kimekuwa pia kikiendesha vitendo
vya kigaidi nchini Chad, Cameroon na Niger. Wanawake na wasichana wamekuwa
wakitekwa nyara na kubakwa! Watoto na vijana wamekuwa wakibebeshwa mabomu ya
kujitoa mhanga, hali ambayo imepandikiza utamaduni wa kifo. Jitihada za
Serikali ya Rais Muhammad Buhari aliyeingia madarakani kunako mwaka 2015 kutaka
kurejesha: usalama wa raia na mali zao; amani na utulivu, hadi sasa zimegonga
mwamba nchini Nigeria.
Mgogoro
wa ardhi kati ya jamii ya wakulima na wafugaji, athari za mabadiliko ya
tabianchi pamoja na athari za mtikisiko wa uchumi kitaifa na kimataifa ni mambo
ambayo yanaendelea kuchangia hali ngumu ya maisha ya wananchi wa Nigeria.
Kinzani za kidini kati ya Wakristo na Waislam huko Jos pamoja na utekwaji nyara
wa wanafunzi wa shule ya Chibok ni kati ya matukio ambayo yametikisa Jumuiya ya
Kimataifa. Wanafunzi 82 waliachiliwa huru, lakini hadi sasa hatima ya wanafunzi
wengine 113 haijulikani. Katika shida, mahangaiko na changamoto zinazoikabili
familia ya Mungu nchini Nigeria, Baba Mtakatifu Francisko amekuwa daima
akiikumbuka na kuisindikiza. Baba Mtakatifu kunako mwaka 2015 aliwaandikia
barua Maaskofu wa Nigeria, akiwashukuru na kuwatia moyo kwani licha ya matatizo
na changamoto mbali mbali walizo nazo nchini humo, lakini bado Kanisa limekuwa
ni chombo na shuhuda wa ukarimu, huruma na msamaha, tunu msingi katika maisha
na utambulisho wa Kanisa.
Kanisa
Katoliki nchini Nigeria, limeendelea kujikita katika mchakato wamajadiliano ya
kidini na kiekumene katika ukweli na uwazi; ili kulinda na kudumisha: utu,
heshima, haki msingi za binadamu; ustawi, mafao na maendeleo ya wengi. Kanisa
bado liko mstari wa mbele katika kuhimiza umuhimu wa upatanisho unaofumbatwa
katika; majadiliano na msamaha ili kudumisha umoja na mshikamano wa kitaifa.
Majadiliano ya kidini na kiekumene yanafumbatwa kwa namna ya pekee katika
huduma makini kwa waathirika wa vitendo vya kigaidi nchini Nigeria sanjari na
ujenzi wa nyumba za ibada, ili kweli dini ziweze kusaidia kuponya madonda ya
chuki, utengano na uhasama unaobubujika kutokana na misimamo mikali ya kidini
na kiimani!
Baraza
la Maaskofu Katoliki Nigeria linakaza kusema, licha ya changamoto na matatizo
yote haya, lakini bado kuna miito mingi ya maisha ya kipadre na kitawa.
Wakristo wengi wanashiriki kikamilifu katika maisha na utume wa Kanisa.
Changamoto kubwa kwa wakati huu ni utamaduni wa kifo unaoendelea kupandikizwa
nchini Nigeria kwa kukumbatia sera za utoaji wa mimba pamoja na vitendo vya
kigaidi ambavyo vimepeleka familia nyingi zikijikuta zikiwa na watoto yatima,
wajane na watoto wanaoishi katika mazingira magumu na hatarishi.
Sera za
usawa wa kijinsia na uzazi salama ni hatari sana kwa tunu msingi za maisha ya
ndoa na familia. Biashara na matumizi haramu ya dawa za kulevya, biashara ya
binadamu na utumwa mamboleo ni kati ya mambo yanayochafua utu na heshima ya
binadamu; umoja, mshikamano na mafungamano ya kijamii. Maaskofu nchini Nigeria
wanaitaka familia ya Mungu nchini humo, kujenga na kudumisha Injili ya familia
inayofumbatwa katika Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo.
Kanisa
kwa kushirikiana na Serikali pamoja na wadau mbali mbali wa maendeleo endelevu
ya binadamu, limekuwa mstari wa mbele katika mapambano dhidi ya umaskini wa
hali na kipato; dhidi ya mmong’onyoko wa tunu msingi za kiroho, kanuni maadili
na utu wema. Maaskofu wanasema, sera makini na endelevu katika masuala ya
kiuchumi ni muhimu sana katika mapambano dhidi ya ukosefu wa fursa za kazi na
ajira miongoni mwa vijana wa kizazi kipya! Baraza la Maaskofu Katoliki Nigeria
linasema limefadhaishwa sana na matukio yaliyojitokeza Jimbo Katoliki la Ahiara
ambako tangu mwaka 2012, Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI alipomteua Askofu
Peter Okpaleke, hakufanikiwa kukanyaga mguu ndani ya Jimbo lake! Baada ya vuta
nikuvute, tarehe 19 Februari 2018, Baba Mtakatifu Francisko akaridhia Askofu
Peter Okpaleke ang’atuke madarakani kwa ajili ya ustawi, mafao na maendeleo ya
familia ya Mungu Jimbo Katoliki la Ahiara. Ni tukio ambalo bado linahitaji toba
na wongofu wa ndani, ili kuanza kuandika historia ya nidhamu, utii na maendeleo
ya watu wa Mungu!
Na Padri Richard A. Mjigwa, C.PP.S.
Vatican News!
Comments
Post a Comment