Ask. Ngalalekumtwa awataka waamini kumuombea Rais Magufuli
Na Getrude Madembwe, Iringa.
ASKOFU
Tarcisius Ngalalekumtwa wa Jimbo Katoliki Iringa amewataka
waamini kumuombea Rais Dk. John Magufuli na serikali yake ili aweze kuliongoza
Taifa kwa haki na amani.
Askofu Ngalalekumtwa ambaye pia ni Rais wa Baraza la Maaskofu
Katoliki Tanzania (TEC) ameyasema hayo hivi karibuni wakati wa Misa Takatifu ya
Pasaka katika Kanisa Kuu la Moyo Mt. wa Yesu Parokia ya Kihesa Iringa.
“Amani tuliyonayo ni tunu kutoka kwa Mungu hivyo watanzania
tunapasika kuilinda, tumuombee pia Rais wetu na serikali yake ili iwe yenye
huruma na inayoongoza kwa kufuata msingi ya haki .
Pasaka hii inatufundisha kutendeana mema, Tunapoadhimisha
pasaka kila mmoja wetu atafute haki, amani, atambue na aone kuwa mwenzake
anastahili kulindwa na kutendewa haki.
Wadogo na wanyonge wapewe upendeleo katika akili zao na ndipo
Mungu wetu atapendezwa maana ametoa jukumu kwa kila mmoja wetu kuwalinda na
kuwajali wanyonge na wenye shida,” amesema Askofu Ngalalekumtwa.
Amewataka waamini kuombea ustawi wa imani yao na hasa kwa
kipindi hiki wanapomshukuru Mungu kwa miaka 150 ya uinjilishaji .
“Haitoshi mtu kujiita mkristo kwa maneno, tuishi Injili kwa
matendo tukikumbatiwa na unyenyekevu ndani ya moyo, upole, utulivu na amani ili
kuleta tumaini jipya na wokovu katika jamii,” amesisitiza Askofu Ngalalekumtwa.
Comments
Post a Comment