'Jumuiya zitoe viongozi waaminifu' Ask. Chengula

Na Pascal Mwanache, Mbeya
ASKOFU wa Jimbo Katoliki Mbeya Mhashamu Evarist Chengula amezitaka Jumuiya Ndogo ndogo za Kikristo ziwe chachu ya kutoa viongozi bora, wenye uwezo wa kutambua mahitaji ya watu wengine na wenye uwezo wa kushawishi walio juu kutupa macho chini na kuwasaidia wenye uhitaji.
Ameyasema hayo katika Adhimisho la Misa Takatifu ya Pasaka Kitaifa lililofanyika katika Kanisa la Bikira Maria wa Fatima Parokia ya Mwanjelwa, Jimbo Katoliki Mbeya.
Amesema kuwa Taifa linapojiandaa kwa uchaguzi wa Serikali za Mitaa hapo mwaka 2019, Jumuiya Ndogo ndogo za Kikristo zianze kutathmini watu wanaofaa kuwaongoza wananchi, kwa kuwa viongozi hao watapatikana miongoni mwao. Amewasihi watanzania kutochagua mtu kwa sababu ya chama bali waangalie uwezo wake wa kuleta umoja, na awe tayari kuumia kwa ajili ya maendeleo ya wengine.
“Ni aibu kulalamika baada ya uchaguzi kuisha. Ukiona kiongozi aliyechaguliwa hafai basi ujue wewe uliyemchagua ndiye haufai na ndiye uliyesababisha. Jumuiya zetu zianze sasa kutathmini yupi ana nguvu ya kujitolea na kusema ukweli. Hata kama siyo mkatoliki, au hata kama siyo wa chama unachokipenda, ili mradi ana uelekeo wa kuwasaidia watu huyo anafaa kuchaguliwa” ameeleza.
Akitoa homilia katika Misa hiyo Askofu Chengula amesema kuwa Pasaka inalenga kuwakumbusha waamini kuendeleza upya wa maisha ya kikristo waliyoahidi kuyaishi walipobatizwa, ili kujenga taifa jipya lenye furaha, upendo na amani.
Amewaasa waamini na watu wenye mapenzi mema kuwa watenda mema wa kudumu huku wakiwaponya watu wenye magonjwa ya kiroho ili waamke na kutenda matendo mema kwa kusali, kujali watu na kuishi sakramenti za Kanisa.
“Siku zote lazima tuwe wapya katika kumuishi Kristo. Huu ni lazima uwe mwendelezo na siyo kitu cha kufanya kwa wakati fulani tu. Katika familia tuanze upya na kuacha nyuma maisha ya kale ya kila mmoja kufanya mambo yake kwa njia zake mwenyewe, ni lazima tugeukie maisha ya umoja. Sherehe hii inamkumbusha kila mmoja wetu wajibu wake katika familia na Taifa” amesema.
Agusia ujumbe wa kwaresima wa TEC

Akiongoza waamini katika Ibada ya Ijumaa Kuu iliyofanyika kitaifa Parokia ya Mwanjelwa Jimbo Katoliki Mbeya, Askofu Chengula pia amegusia juu ya Ujumbe wa Kwaresima uliotolewa na Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania akisema kuwa ujumbe huo haukumlenga mtu wala kikundi cha watu, bali ni kwa kila mmoja anayejiita mkristo na mwenye mapenzi mema.

“Ujumbe huu unawahusu wale wanaojiita wakristo lakini matendo yao hayaendani na matakwa ya ukristo” ameeleza Askofu Chengula. Pia akiuelezea ujumbe huo amewataka wakristo wote kuwa wamisionari kwa kuipeleka mbele kazi ya uinjilishaji iliyoanzishwa na wamisionari wa kwanza hapo mwaka 1868.
Amewaasa waamini kuwa sehemu na kiini cha uinjilishaji badala ya kuwanyooshea wengine vidole kwa kudhani kuwa maendeleo ya kanisa yanaletwa na mapadri, maaskofu na watawa pekee. Amemtaka kila mkristo kuwa wakala wa uinjilishaji, huku akiwaalika waamini wote na watu wenye mapenzi mema kuhudhuria kilele cha jubilei ya miaka 150 ya uinjilishaji Tanzania Bara ambacho kitafanyika Novemba 2018 huko Bagamoyo.
Aidha amechambua ujumbe huo wa kwaresima kwa kuwasihi waamini kujiandaa vema kwa uchaguzi wa serikali za mitaa unaotarajiwa kufanyika hapo mwaka 2019, akiwataka wasali, watafakari katika jumuiya ndogo ndogo za kikristo, na kuona ni nani hasa wanastahili kuongoza wananchi na kuwafanya wawe na amani.
“Kila mara uchaguzi unapoisha tunaanza kuona vurugu za watu kukimbizana kama sungura na mbwa. Haifai kwa wananchi kuchagua chama fulani kwa kudhani kwamba chama ndiyo msingi wa maendeleo na amani. Ni vizuri mkajua kuwa mtu sahihi, asiye mbinafsi  na ambaye atatuhakikishia amani yetu. Haina maana yoyote kuwa na viongozi ambao wanatufanya sisi tuliowachagua tuishi kwa wasiwasi kila muda. Hivyo ni lazima msali, mshiriki vema na mujitathmini ndani ya jumuiya zenu” ameeleza Askofu Chengula.
Pia amewaasa waamini kukitumia kipindi cha pasaka kujitathmini upya ili kuchota nguvu za kupyaisha maisha yanayompendeza Mungu na jirani.


Comments

Popular posts from this blog

SALA YA ASUBUHI:SALI HIVI..

Ujio wa Wamisionari wa Kwanza Tanzania Bara (2)

MJUE MTAKATIFU MARIA GORETTI