Ask. Amani aagwa Moshi, awaachia ujumbe
·
Na
Pascal Mwanache, Dar
ASKOFU
Mkuu Mteule wa Jimbo Kuu Katoliki Arusha Mhashamu Isaac Amani ameagwa rasmi na
waamini wa Jimbo Katoliki Moshi katika Adhimisho la Misa Takatifu lililofanyika
katika Kanisa Kuu la Kristo Mfalme Moshi, Aprili 4, 2018.
Akitoa homilia katika
Misa hiyo Askofu Amani amewaasa waamini kuwa vyombo vya wokovu kwa kuwatetea
wanyonge, kuwafariji, kupigania haki zao na kuwaonya wanaopotosha haki na kuwakosesha
wengine amani. Amesema kuwa kila mkristo anapaswa kushiriki kazi ya Yesu ya
kuwasaidia na kuwaimarisha wale wanaowahitaji, huku akitaka ukarimu wao uwe
zaidi ya fedha na dhahabu.
“Ni lazima tuwashike
mkono na tuwainue wale waliotengwa na wenye shida. Tunaowasaidia wanamshangilia
Mungu kwa kuwa wameonja furaha ya uhai. Baada ya kufufuka Yesu hakufanya
miujiza ya uponyaji, hivyo hilo ni jukumu letu kuwa vyombo vya wokovu”
ameeleza.
Awali Askofu Amani ametoa
salamu za Pasaka kwa waamini wa majimbo ya Moshi na Mbulu ambapo amesema kuwa
Kanisa linapoadhimisha Jubilei ya Miaka 150 ya Uinjilishaji Tanzania Bara
inafaa kila muumini ajitathmini nafsi yake kwa kutafakari jinsi anavyoelewa na kuishi maagano ya
ubatizo.
Amesema kuwa baadhi ya
waamini wanazo hali za kusikitisha hasa ushirikina, kutojali amri za Mungu na
za Kanisa, kuishi usuria, kuendekeza chuki na kukataa kusameheana na kupatana.
Amemtaka kila muumini atafakari changamoto hizo na kujiuliza anakwenda wapi na katika
changamoto za kuishi maagano ya ubatizo.
“Wamisionari walituletea
Injili ili ituangazie namna ya kuwa watoto wa Mungu na wa Kanisa. Chimbuko la
ubatizo ni Pasaka; yaani mateso, kifo na ufufuko wa Mkombozi wetu Yesu Kristo.
Ubatizo hutuingiza katika ushindi wa mkombozi. Je tunayo maisha ya ushindi? Je
imani, matumaini na mapendo yetu yamejikita kwa Yesu mfufuka? Je ninajivunia
kuwa mkristo na kuchangamkia ukristo?” amehoji Askofu Amani.
Aidha amesema kuwa tunda
la ubatizo wa maji ni kufanya toba kwa kukataa maisha duni ya dhambi, chuki,
uasi, mafarakano na hofu, hivyo amewataka waamini hao kukataa uasi na kila
ubaya ili wawe safi.
“Ubatizo siyo ngonjera au
maigizo; ubatizo huokoa; ubatizo ni kuzaliwa upya kwa maisha mapya. Uhai wa
maisha mapya huonekana katika tabia za kusali, kupokea sakramenti, kusoma neno
la Mungu, kujitahidi kushirikiana na wakristo wengine katika vyama vya kitume
na kujitolea kuwasaidia wenye shida” amesema.
Askofu Amani anatarajiwa
kusimikwa kuwa Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki Arusha hapo Aprili 8, kuanzia
saa 3 asubuhi katika viwanja vya Kanisa Kuu la Mt. Theresia wa Mtoto Yesu.
Comments
Post a Comment