Dodoma yapewa hadhi ya kuwa jiji
KATIKA
maadhimisho ya miaka 54 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, iliyokuwa
halmashauri ya Manispaa ya Dodoma imepandishwa hadhi na kuwa jiji.
|
Akihutubia wananchi katika sherehe hizo za muungano katika uwanja wa
Jamhuri Dodoma hivi karibuni,Rais wa Jamhuri ya muungano wa Tanzania Dkt.John
Pombe Magufuli amesema kutokana na mamlaka aliyo nayo anatangaza rasmi kuupa
hadhi ya jiji mji wa Dodoma.
Pamoja na hayo amesema, kutokana na kuupadisha mji wa Dodoma kuwa na hadhi ya jiji , hivyo
aliyekuwa Mkurugenzi wa Manispaa ataitwa Mkurugenzi wa Jiji la Dodoma
hatua ambayo imeungwa mkono na wananchi
waliokuwa uwanjani kusherehekea muungano .
Sambamba na hayo amesema dhamira ya serikali kuhamishia makao yake makuu
bado ipo pale pale na kwamba zaidi ya watumishi wa serikali 3800 tayari
wamehamia Jijini Dodoma.
Wakizungumzia hatua hiyo, baadhi ya wananchi mkoani humo wamesema kutokana na Dodoma kutangazwa kuwa jiji
mzunguko wa kibiashara utakuwa mkubwa na hivyo kuwa fursa kwa wawekezaji na
wafanyabiashara wengine.
“Dodoma kuwa jiji ni fursa kubwa kwetu wafanyabiashara kwani itaongeza
tija na uhamasishaji wa shughuli za maendeleo kupitia miradi mbali mbali
iliyopo,” amesema mfanyabiashara mmoja .
Wakati huo huo Rais Magufuli
amesema serikali itaendelea kuulinda ,kuutunza na kuuimarisha muungano wa
Tanganyika na Zanzibar kwa gharama yoyote ile na kamwe haitomwonea haya mtu
yeyote atakaye diriki kuuvunja muungano uliopo.
“Mimi na Dkt Shein tutaendelea kuulindà muungano kwa gharama yoyote kwani tunaamini muungano
wetu ndiyo nguvu yetu na ninawahakikishia kuwa tupo imara ,” amesisitiza.
Hata hivyo Rais amewatoa hofu wananchi kwa kusema kuwa, licha ya kwamba
muungano huo unakabiliwa na changamoto
ndogo ndogo za kimuungano, serikali za pande mbili yaani Tanzania bara na visiwani
zimejipanga kutatua na kuondoa mizozo.
Pamoja na hayo amezitaja faida ambazo Tanzania inanufaika kwa
muungano huo kuwa ni pamoja na nchi
kuheshimika, kuwa na nguvu ya pamoja,mafanikio katika nyanja za
kiuchumi,kisiasa na kijamii pamoja na kutoa mchango wa harakati za kusuruhisha
migogoro katika nchi nyingine.
Tanganyika na Zanzibar ziliungana kutokana na ukaribu wa kijiografia
,muingiliano wa masuala ya utamaduni na urafiki baina ya viongozi waasisi .
Sherehe za muungano mwaka huu zimehudhuriwa na viongozi mbalimbali
akiwemo Rais msaafu wa Jamhuri ya muungano wa Tanzania Benjamin Mkapa, Rais wa
Zanzibar Dkt.Shein, Mawaziri Wakuu
Wastaafu ,wabunge na na viongozi mbalimbali wa nchi.
Comments
Post a Comment