Vyombo vya habari vya Katoliki vyaaswa kufahamisha umma juu ya miaka 150 ya uinjilishaji
Wanamawasiliano wa Vyombo vya Habari vya Kanisa Katoliki
wametakiwa kuweka mikakati madhubuti kupitia njia za mawasiliano ikiwemo
Televisheni, Radio na Magazeti ili kurahisisha na kuendeleza utume wa Kanisa.
Aidha Vyombo hivyo vya habari viweke mikakati madhubuti ili kuelimisha na
kufahamisha uma kuhusu Jubilei ya Miaka
150 ya Ukristo Tanzania.
Wito huo umetolewa hivi karibuni na Katibu Mkuu wa Baraza la Maaskofu
Katoliki Tanzania (TEC), Padri Raymond Saba wakati akifungua Mkutano Mkuu wa
Mwaka wa Wakurugenzi wa Mawasiliano Majimboni na wa Vyombo vya Habari
vya Kanisa uliofanyika hivi karibuni Kurasini, Jijini Dar es salaam.
Padri Saba amesema kuwa, kama
wanamawasiliano hawana budi kuweka mikakati ya kuhamasisha waamini juu ya
matukio mbalimbali katika Kanisa ikiwemo Maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 150 ya
Uinjilishaji Tanzania Bara.
“Ni wajibu wa Vyombo vyetu vya Habari vya Kanisa Katoliki kuhakikisha
waaamini wanajua, wanashiriki na kuyaishi yale yote mazuri yaliyokuwepo ndani
ya Miaka 150 ya uinjilishaji ili waweze kuimarisha Imani yao,” amesema.
Aidha ameongeza kuwa ni vyema wakajenga utamaduni wa kusoma na
kujifunza masuala mbalimbali muhimu
katika Kanisa ili yawasaidie katika kazi zao za kila siku sambamba na
kuzingatia matumizi fasaha ya lugha.
Kwa Upande wake Mkurugenzi wa Mawasiliano Jimbo Kuu Katoliki Dar es Salaam, Padri Joseph Masenge wakati
akiwasilisha mada ya weledi katika
Uandishi wa habari na uandaaji wa vipindi amesema uandishi ni wito , hivyo kama
wanamawasiliano wanapaswa kufanya kazi kwa weledi na haki sambamba na
kuzingatia maadili ya Uandishi wa Habari.
“Si sahihi kuongeza maneno ama kumlisha mtu maneno ili kuuza gazeti. Si
sahihi kupindisha ama kukuza vichwa vya habari kwa ajili ya soko la gazeti.
Maadili ya uandishi ndiyo ninayosisitiza.
Andikeni kwa ufasaha, ubunifu na weledi ili kuhabarisha umma na
kujiaminisha katika jamii,” amesisitiza Padri Masenge.
Mkutano huo wa Mwaka wa Wanamawasiliano uliwakutanisha Wakurugenzi wa Majimbo nane wakiwemo wasimamizi wa vipindi
kutoka katika Redio zinazomilikiwa
na Kanisa Katoliki majimboni ikiwemo Tumaini Media, Redio Ukweli ya
Morogoro, Redio Mwangaza ya Dodoma, Redio Fadhila ya Tunduru Masasi, Redio Faraja
ya Shinyanga, Redio Chemchem ya Sumbawanga, Redio Huruma ya Tanga, Redio Mbiu
ya Bukoba iliyopo kwenye majaribio na Redio Maria Tanzania.
Kanisa Katoliki Tanzania lina jumla ya Majimbo 34 kati ya hayo Majimbo
Makuu ni sita ambayo ni Jimbo Kuu Katoliki Dar es Salaam, Arusha, Tabora,
Mwanza, Dodoma na Songea.
Comments
Post a Comment