‘Bila ushirikiano wa Serikali na Kanisa hakuna maendeleo’
ASKOFU
wa Jimbo Katoliki Singida Mhashamu Edward Mapunda, ameipongeza serikali ya Mkoa
wa Singida, kwa kutoa ushirikiano na Kanisa katoliki katika shughuli za
maendeleo.
Askofu Mapunda ameyasema
hivi karibuni katika uzinduzi wa miaka 22 ya Radio Maria Tanzania iliyofanyika
Parokia ya moyo Mtakatifu wa Yesu Jimbo Katoliki Singida.
Katika homilia yake
Askofu Mapunda amesema kuwa ushirikiano ukidumishwa Kati ya serikali na Kanisa
ni lazima maendeleo yawepo,kwani miongoni mwa mambo ambayo yanaleta chachu ya
Nguvu, umoja na mshikamano ni ushirikiano ambao kwa kiasi kikubwa unaleta hali
ya kujaliana, hivyo anategemea maendeleo makubwa zaidi katika Jimbo la singida
Askofu mapunda
amesisitiza kuwa, ili imani ya Kanisa Katoliki iendelee kudumu zaidi ni lazima
kwa kila mkristo mkatoliki mmbatizwa afahamu umuhimu wake wa kuchangia vyombo
vinavyoweza kuisambaza injili hiyo kwa kasi zaidi ulimwenguni kote ikiwemo
Radio Maria, kwani hiyo ni njia pekee ambayo ina uwezo mkubwa zaidi wa kuhubiri
neno la Mungu haraka zaidi na kwa kasi kubwa.
“Kuna mtu alijitokeza
wakati nikiwa Ulaya akataka kunipa Radio, nami nikamwambia sidhani kama
ninahitaji Radio maana nchini Tanzania kuna RAadio Maria na Redio ya mama
inatosha’’ amesema Askofu Mapunda.
Kwa upande wake Mkuu wa
Mkoa wa Singida Dr Rehema Nchimbi ambaye alikuwa ni mgeni rasmi katika uzinduzi
huo, amewataka wakristo kote ulimwenguni kujiwekea Utaratibu maalum wa kusali
Rozari Takatifu, huku akisisitiza kuwa, Pamoja na mambo mengi ambayo
yanafanyika hapa duniani, ni lazima yasindikizwe na nguvu ya sala kwani sala
pekee ndiyo silaha ya kukuweka mbali na muovu shetani.
“Waamini wenzangu naomba
mtambue ya kuwa Salamu Maria moja Ina
nguvu kuliko bomu la nyuklia.
Kama unataka kuwa
mkandarasi mzuri ambaye hakuna hata mtu mmoja anayeweza kukuondoa katika kazi
yako basi ni lazima kwanza uwe mkandarasi wa Yesu,” amesema Dr Nchimbi huku
akisema ya kwamba kujitoa katika matukio mbalimbali ya Kanisa pamoja na kusali
ndiyo mahusiano pekee yanayodumu milele kwani yanakuwa yameunganishwa na Mungu
ambayo hakuna mwanadamu yeyote anayeweza kuyavunja kamwe.
Sanjari na hayo Dr
Nchimbi ametoa zawadi ya Rozari elfu
mbili kwa Radio Maria Tanzania huku akisema kuwa itakuwa chachu ya kuwajengea
mazingira mazuri zaidi waamini katika sala, kwani kupitia Rozari Takatifu
miujiza mingi zaidi inawatokea wanaosali kwa imani.
Naye Mkurugenzi wa
Matangazo Radio Maria Tanzania Padri John Maendeleo, amewashukuru viongozi wote
wa Kanisa waamini, pamoja na viongozi wa Serikali ambao walijitokeza kwa furaha
kubwa katika uzinduzi huo na kusema kuwa kuwezesha habari njema kufikia watu
wengi zaidi kupitia Radio Maria ni sawa na Kupanda mbegu katika udongo mzuri,
jambo ambalo linakupa uhakika wa kujipatia mazao mengi na ya kutosha siku za usoni.
Uzinduzi wa maadhimisho
ya miaka 22 ya Radio Maria Tanzania umefanyika Jimboni Singida, huku kilele
chake kikiwa ni Tarehe 1/7/2018 Jimboni humo.
Comments
Post a Comment