WAZAZI IRINGA WATAKIWA KUWASOMESHA WATOTO WA KIKE
n Na Getrude Madembwe, Iringa
WITO
umetolewa kwa wazazi na walezi kuona umuhimu wa Elimu kwa kuwasomesha watoto wa
kike ili waweze kutimiza ndoto zao na kulisaidia Taifa katika nyanja
mbalimbali.
Wito
huo umetolewa hivi karibuni na mgeni rasmi kwenye mahafali ya pili ya shule ya
sekondari ya wasichana ya Regina Pacis, Josephat Mwagala inayomilikiwa na Jimbo
Katoliki Iringa parokia ya Kibao, yaliyofanyika shuleni hapo.
Mwagala
amesema kuwa kumekuwa na fikra potofu kuwa kumsomesha mtoto wa kike ni kupoteza
rasilimali fedha kitu ambacho amesema siyo kweli kwani maisha ya sasa bila
elimu ni changamoto kubwa hasa kwa mtoto wa kike.
Mwagala
amesema kuwa mtoto wa kike akipatiwa elimu kuna uwezekano mkubwa kwa taifa kuwa
na maendeleo kutokana na kuwajibika kwao katika maisha ya kila siku, hivyo
wazazi na walezi ni muhimu kuwasomesha watoto wa kike kwa lengo la kuendeleza
ndoto walizonazo.
Wakati
akijibu risala ya shule, mgeni huyo rasmi ametoa kiasi cha Tsh.300, 000 kwa
ajili ya walimu ikiwa ni pongezi kwa kazi nzuri wanayoifanya na ameahidi
kukabidhi mifuko 100 ya saruji, kuchimba visima viwili vya maji vyenye thamani
ya Tsh. Milioni 3 kwa ajili ya matumizi ya wanafunzi.
Aidha
katika mahafali hayo ameongoza harambee ya ununuzi wa keki ambapo kiasi cha
Tsh.700, 000 kimepatikana.
Ameipongeza
shule hiyo kwa kuwa moja ya shule zinazofanya vizuri mkoani Iringa kielimu na
kitabia kwani ni moja ya shule ambazo idara ya elimu haipati malalamiko ya mara
kwa mara kutoka shuleni hapo.
Amewataka
wahitimu hao kuyasoma vyema mazingira ya maisha popote watakapokuwa na kuamua
namna ya kujiajiri ili mradi isiwe shughuli zinazopingana na sheria na maadili ya
kijamii, kama vile kuuza dawa za kulevya, ukahaba, unyang’anyi na mambo mengine
yanayofanana na hayo ambayo watajiingiza matatani na kuonekana wabaya.
‘Ninawaomba
mkirudi nyumbani kwa muda huu mfupi wa kusubiri matokeo, zingatieni maadili
mliyofundishwa mkiwa hapa shuleni, bado nyie ni wanafunzi, hakikisheni
mnajiepusha na mambo yasiyofaa ambayo yanaweza kukatisha ndoto zenu za
kuendelea na masomo ya juu,” Ameasa Bw. Mwagala.
Awali
Mkuu wa shule ya wasichana Regina Pacis, Marco Shayo akimkaribisha mgeni rasmi
amesema kuwa uongozi wa shule umeweka mikakati mbalimbali inayoendelea
kutekelezwa ikiwa ni pamoja na ujenzi wa jengo la shule linaloendelea kujengwa,
kuchimba visima vya maji ili maji yaweze kukidhi mahitaji ya wanafunzi.
Shayo
amewasihi wahitimu hao kuyazingatia maadili waliyoyapata wakiwa shuleni hapo
ili waweze kuepukana na vishawishi vitakavyoweza kukatiza ndoto zao na hatimaye
kuwaingiza katika mambo yasiyofaa katika jamii na Taifa kwa ujumla.
Pamoja
na mafanikio mengi, lakini shule inakabiliwa na changamoto kadhaa ikiwemo
upungufu wa nyumba za walimu, uhaba wa vyumba cha maktaba na upungufu wa visima
vya maji.
Comments
Post a Comment