KANISA TABORA LAANZISHA KILIMO CHA KOROSHO, MAEMBE

JIMBO Kuu Katoliki Tabora hivi karibuni limezindua kilimo cha korosho na miembe ya muda mfupi katika eneo lake la hija   ili kutoa mfano wa kilimo cha kibiashara.
Akiongea na Gazeti hili kwa niaba ya Askofu Mkuu Paul Ruzoka, mhasibu wa jimbo hilo Padri Nicolaus Bulabuza amesema kuwa Jimbo Kuu Tabora limeamua kuanzisha kilimo cha korosho na miembe ya muda mfupi ili kutoa elimu kwa wanatabora kubadili mawazo na kuona bado Tabora inaweza kuingia katika kilimo hiki kipya.
Aidha Padri Bulabuza amesema kuwa wao kama Kanisa hawana budi kuona ni kwa namna gani wanaweza kuunga mkono kauli mbiu ya serikali ya awamu ya Tano yaani Tanzania ya viwanda.  “Kila mwana Tabora hana budi kuona yeye anaingiaje katika mnyororo wa Tanzania ya viwanda,” ameongeza.
Akifafanua zaidi Padri Bulabuza amesema mazao ya korosho na miembe hayana budi kupewa kipaumbele kwani yana faida nyingi baadhi yake ikiwa ni kutumika kama chakula, na pia ni biashara.
Pia amesema kuwa wana Tabora hawana budi kupokea mazao hayo kwa mikono miwili ili kujiongezea chakula na kipato cha kaya, wilaya, mkoa na hatimae Taifa.  Hii imetokana na wana Tabora wengi kujikita katika kilimo cha tumbaku kwa muda mrefu kitu ambacho kimesababisha uharibifu wa mazingira na afya kwa wakulima.
Padri Bulabuza amesema kilimo cha korosho na miembe ni rafiki wa mazingira tofauti na zao la tumbaku ambalo kwa miaka mingi limeicha Tabora katika hali mbaya kimazingira.
Kilimo hicho kilichozinduliwa chini ya Afisa Ugani wa kata ya Ifucha katika Manispaa ya Tabora, ni mategemeo kuwa mashamba hayo yatakuwa darasa kwa wanakijiji wa kijiji cha Ifucha na vitongoji vyake.

Jimbo Kuu Tabora tayari limepanda zao la korosho kwa ukubwa wa Ekari 4, na Ekari mbili za miembe ya muda mfupi.  

Comments

Popular posts from this blog

SALA YA ASUBUHI:SALI HIVI..

Ujio wa Wamisionari wa Kwanza Tanzania Bara (2)

HISTORIA YA SHEREHE YA MOYO MTAKATIFU WA YESU