Viongozi wa dini watangaza vita dhidi ya ukatili wa kijinsia
VUGUVUGU la
kiimani kwa ajili ya kutetea usawa wa kijinsia na kupinga ukatili wa kijinsia nchini limezinduliwa jijini Dar es salaama
hivi karibuni, ikiwa ni nguvu ya pamoja ya viongozi wa dini na wadau mbalimbali
katika kuibadilisha jamii iondokane na mila zinazochochea ukatili.
Vuguvugu hilo
linaloitwa ‘Side by side’ yaani ‘bega kwa bega’ limezinduliwa Novemba 30, 2017
katika Hoteli ya Golden Tulip jijini Dar es salaam, ambapo wadau mbalimbali na
viongozi wa dini wameeleza kuwa uwepo wa vuguvugu hilo utasaidia mapambano
dhidi ya ukatili wa kijinsia.
Akizungumza katika
hafla hiyo Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Kikristo Tanzania (CCT) Rev. Moses Matonya
amesema kuwa lengo la vuguvugu hilo ni kuweka nguvu za pamoja kama viongozi wa
dini kwa kushirikiana na wadau wengine ili kupinga ukatili wa kijinsia.
Amesema kuwa
wanaunga mkono jitihada za serikali na wadau katika mapambano dhidi ya vitendo
vya ukatili wa kijinsia kwa kuihimiza jamii na kuielimisha ili ibadilike na
kuachana na mila potofu zinazochochea ukatili.
“Tunalenga
kuibadilisha jamii iache vitendo vya ukatili kwa watoto, wanawake na wanaume,
tukikemea lugha za matusi na udhalilishaji wa utu wa binadamu. Ukatili unaweza
kutokomezwa ikiwa jamii yenyewe itaamua na kuyapa kipaumbele masuala yanayohusu
usawa wa kijinsia. Nasi kama viongozi wa dini tunawiwa kutafsiri neno la Mungu
kwa mtazamo wa kijinsia na kuachana na mila kandamizi. Pia tunalenga
kuihamasisha jamii kusema hadharani juu ya vitendo vya udhalilishaji” ameeleza.
Kwa upande wake
Mkuu wa Wilaya ya Gairo Siriel Mchembe amewapongeza wana vuguvugu la ‘bega kwa
bega’ akisema kuwa ukatili wa kijinsia ni changamoto kubwa hapa nchini kama
ilivyo katika nchi nyingine, na kusema kuwa vuguvugu hilo linaenda sambamba na
maadhimisho ya siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia.
Aidha amesema kuwa
jitihada hizo zitasaidia kupunguza vifo vitokanavyo na uzazi ambapo idadi ya
vifo hivyo inaongezeka ambapo mwaka 2010 ilikua asilimia 23 na 2015 ilifikia
asilimia 27.
Comments
Post a Comment