SEMINARI ARUSHA YAFANYA JUBILEI YA MIAKA 50
ASKOFU
Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki Arusha Mhashamu Josaphat Lebulu amesema kuwa Shule
za Seminari hapa Nchini zimekuwa mfano bora katika kukuza maadili kwenye jamii
kutokana na malezi bora ya kiroho na kimwili.
Askofu
Mkuu Lebulu ameyasema hivi karibuni alipokuwa akiongoza Misa ya Jubilee ya
miaka 50 tangu kuanzishwa kwa Seminari ya Arusha iliyopo Oldonyo Sambu Jimbo
Kuu Katoliki Arusha.
Amesema
kuwa tangu kuanzishwa kwa seminari hiyo iliyoanzishwa mwaka 1967 lengo likiwa
ni kulea vijana wa kiume kuwa mapadri na kupata wakristo wenye maadili mema
katika jamii, kumekuwa na mafanikio makubwa ambayo yameisaidia Serikali na
jamii kwa ujumla kubadilisha mienendo ya vijana ambao walikuwa na tabia mbaya.
“Seminari
zimekuwa zikifundisha vijana wote bila kujali itikadi za Dini mambo ya kiroho
na kimwili na kujua mpango wa Mungu katika maisha yao huku wakifundishwa
kutambua kwamba binadamu wote ni sawa kwa kuheshimu utu wa mtu,” Amesema.
Kutokana
na Elimu inayotolewa na Shule za Seminari, Serikali na jamii imekuwa na watu
wenye maadili na hofu ya Mungu wanaofanya kazi katika sekta mbalimbali ambao
wanafuata Sera za Taifa kutokana na maadili waliyonayo.
“Tunamshukuru
Mungu kufikia hatua hii tangu kuanzishwa kwa seminari hii tumekuwa na mafanikio
makubwa hususani kuelimisha maadili ya Kiafrika wapo vijana wanakuja wakiwa na
tabia mbaya lakini wakifika hapa tunawabadilisha na hatimaye wengine ni
viongozi wazuri sana katika Kanisa na Serikali,” amesema Askofu Mkuu Lebulu.
Seminari
zimekuwa zikifundisha vijana wote bila kujali itikadi za Dini mambo ya kiroho
na kimwili na kujua mpango wa Mungu katika maisha yao huku wakifundishwa
kutambua kwamba binadamu wote ni sawa kwa kuheshimu utu wa mtu.
Amewataka
vijana wenye wito kutokata tamaa mbali na changamoto wanazokumbana nazo ambapo
wengi wao wameishia njiani, bali wanapaswa kuzingatia yale wanayofundishwa ili
waweze kutimiza malengo yao.
Ameongeza
kuwa wapo baadhi ya viongozi wa Kanisa na Serikali ambao wamekuwa hawasemi
ukweli pale mtu anapokosea wanaficha ukweli hivyo kuwa na ukosefu wa maadili.
“Kama
kiongozi wa Kanisa na Serikali mnapaswa kuwa wakweli mbele za Mungu mtu akikosa
mkosoeni na kumwambia ukweli kwani ukweli bila maadili hupoteza malengo,”
amesema Askofu Mkuu Lebulu.
Naye
Gombera wa Seminari ambaye ndiye msimamizi Mkuu Padri Edwin Kiromo amesema kuwa
mbali na elimu ya kiroho wamekuwa wakitoa elimu ya kilimo na ufugaji, afya,
uhifadhi wa mazingira kwa kujenga miundombinu jambo ambalo limesaidia wanafunzi
kujitambua na kufanya kazi za mikono.
Mbali
na mafanikio waliyoyapata ya kuwa na hospitali, shule na vituo vya watoto
yatima bado wamekumbana na changamoto nyingi zikiwemo kuchakaa kwa miundombinu
ya Seminari hiyo, uchakavu wa Kanisa wanalotumia kusali, mabweni hayatoshi
ikiwa ni pamoja na fedha za kuendesha seminari hiyo.
Hata
hivyo seminari hiyo ina mipango endelevu ya kudumisha umoja uliopo, kurudisha
kidato cha tano na sita, kuongeza wanafunzi, kuwezesha kupata viongozi wenye
kiwango cha juu ,kuwapata wataalamu wa Kanisa wazuri na viongozi wa walei,
kuongeza mabweni pamoja na nyumba za walimu.
Kwa
upande wake Mwenyekiti wa wanaseminari waliosoma Seminari ya Arusha, Oldonyo
Sambu, George Stephen wameamua kuanzisha umoja wao ili kuendeleza yake mema
waliyoyakuta kwa kurudisha shule hiyo kuleta maendeleo ambapo wamezindua
madarasa matatu ambayo ni matunda yao kwa nia ya kutoa shukrani kwa elimu na
maadili waliyoyapata shuleni hapo.
Amewataka
wale wote wanaomaliza shule walizotoka kuwa na kasumba ya kurudisha fadhila kwa
kujenga miundombinu ikiwa ni manufaa kwa vizazi vijavyo.
Comments
Post a Comment