Miaka 56 ya uhuru
Tanzania inahitaji awamu ya pili kupigania uhuru
Na
Pascal Mwanache, Dar
IMEELEZWA
kuwa Tanzania inapaswa iingie katika awamu ya pili ya kupigana vita vya uhuru
wa kiuchumi ili kuondokana na hali ya kuwa koloni la mfumo wa kimataifa wa
uchumi.
Hayo yameelezwa na Mkuu wa Idara ya Haki, Amani na Uadilifu
wa uumbaji ambaye pia ni Kaimu Mkurugenzi wa Kurugenzi ya Uchungaji Katika
Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC) Dkt. Camilius Kassala, alipoangazia
tathmini ya miaka 56 ya uhuru wa Tanganyika.
Dkt. Kassala ameeleza kuwa hakuna njia yoyote ya kuondokana
na umaskini isipokuwa kupigana vita ya ukombozi wa kiuchumi, ili usimamizi wa
kiuchumi na rasilimali uwe mikononi mwa watanzania.
“Ili kuweza kufika hapo kunahitaji awamu ya pili ya
kupigania uhuru, kutoka kisiasa kwenda kiuchumi. Tafakari maswali haya: Vitu
tunavyonunua madukani, asilimia ngapi vinatengenezwa hapa nchini? Asilimia
ngapi ya wanataaluma wetu wanaomaliza vyuoni wanaingia katika sekta ya uchumi
ili wausimamie? Bidhaa tunazouza nchi za nje, kwa kiwango gani tuna maamuzi
kuhusu bei zake? Na ukilinganisha wawekezaji wa nje na wa ndani, upande upi ni
wengi zaidi” amehoji Dkt. Kassala.
Pia amesema kuwa katika kipindi cha miaka 56 tangu ipate
uhuru, nchi inajivunia mambo mengi ikiwa ni pamoja na kuthamini uelewano,
kutojali tofauti za kidini na kikabila, kuwa na lugha moja ya kitaifa, kuwa na
kiwango cha demokrasia, na kuwa na uchumi ambao unakidhi mahitaji ya lazima ya
wananchi.
Kuhusu kiwango cha demokrasia nchini Dkt. Kassala amesema kuwa
Tanzania inajivunia demokrasia kwa kiwango kinachozidi wastani wa demokrasia
katika nchi nyingi za kiafrika. Pia amesema uelewa wa watanzania kuhusu haki
zao ni wa kiwango cha juu, ambapo mara nyingi wanatafuta namna ya kupata haki
zao bila kuvuruga amani.
Amesema kuwa ili kuimarisha demokrasia nchini serikali haina
budi kutoa uhuru wa habari na uhuru wa shughuli za siasa ili watu wapewe fursa
ya kuwa huru katika sekta ya habari.
“Hata hivyo tunahitaji demokrasia ipanuke zaidi ambapo elimu
ya siasa inapaswa ifundishwe katika shule na vyuo, hii itasaidia kuepukana na
upotoshaji wa maswala ya siasa kama ilivyo sasa” ameongeza.
Aidha amebainisha kuwa sera za uchumi zinapaswa ziangaliwe
upya ili kukabiliana na mfumo wa ubepari unaoashiria kurudi hasa kuongezeka kwa
matabaka ambapo wachache wa tabaka la juu wanachukua sehemu kubwa ya mapato ya
taifa kuliko wengi, na hivyo kuwakosesha kufurahia matunda ya uhuru.
Kuhusu utoaji wa huduma za jamii, Dkt Kassala ametaka
viwango vya ubora wa huduma za jamii kama vile matibabu, elimu, makazi na
usafiri vifanyiwe kazi ili viongezeke. Kuhusu suala la ajira amesema linapaswa
lihusishwe na mfumo wa elimu na mafunzo na lisibaki mikononi mwa sekta binafsi.
Wakati huo huo Dkt Kassala ametahadharisha kuwa vita dhidi
ya rushwa na ufisadi haviwezi kushinda nje ya utaratibu wa maadili. Amesema
kuwa badala ya kuwa na TAKUKURU, Tume ya Maadili ya viongozi iangalie suala la
rushwa kwa mtazamo mpana.
“Wanajaribu kuangalia katika umiliki wa mali, lakini kwa
sasa viongozi wana fursa nyingi za kumiliki mali bila kuvunja sheria. Kila
kiongozi anayesajili mali zake aeleze amezipata kwa njia gani” amesisitiza.
Comments
Post a Comment