Ulinzi waimarishwa Dodoma kuelekea sherehe za uhuru
JESHI la Polisi
Mkoani Dodoma limeendelea kuimarisha ulinzi kwa kufanya operesheni mbalimbali
na misako, katika kuelekea maadhimisho ya miaka 56 ya Uhuru wa Tanganyika,
yatakayofanyika mkoani humo Disemba 9 mwaka huu.
Kamanda wa Polisi
mkoani Dodoma Kamishna Msaidizi Mwandamizi Gilles Muroto amesema kuwa kwa sasa
Mkoa wa Dodoma una wageni wengi waliokuja kwa ajili ya shughuli za sherehe ya
uhuru ambazo kitaifa zinafanyika mkoani hapo ambapo wahalifu hutumia nafasi
hiyo kufanya vitendo vya kihalifu.
Akizungumza na
waandishi wa habari hivi karibuni mkoani Dodoma, Kamanda Muroto ameongeza kuwa
kufuatia upekuzi utakaohusisha nyumba
za wageni na doria, jeshi la polisi limefanya kazi nyingine za misako ambapo
wamekamata watu watatu wakiwa na meno ya tembo, yenye uzito wa kilogram 16
yaliyokuwa yamebebwa kwenye pikipiki kutoka Kondoa yakipelekwa Dodoma mjini.
Pia amesema zoezi
la kubomoa vibanda vya biashara visivyo rasmi eneo la Railway linaendelea
likisimamiwa na vyombo mbalimbali vya ulinzi na usalama na kuwa ubomoaji huo
unalenga kupanua ujenzi wa miundombinu ya reli baada ya eneo hilo kuvamiwa na
wafanyabiashara ambapo katika zoezi hilo wamekamata watuhumiwa watatu kwa
makosa ya wizi wa mali za wafanyabiashara.
“Kufuatia sherehe
za maadhimisho ya uhuru wakazi wa mji huu wanapaswa kuwa waadilifu ili kuiendeleza
amani ikiwa ni pamoja na kusaidiana na jeshi la polisi kuwafichua wahalifu
watakaojitokeza,” amesema.
Sambamba na hayo
ametoa tahadhari kwa watu wanaokwenda Dodoma kufanya uhalifu kuwa sehemu hiyo
siyo salama kwao na kutoa wito kwa wakazi wa Dodoma katika
kipindi hiki kinachoambatana na
shamrashamra nyingi wawe watulivu , wafanye shughuli zao kwa kufuata sheria na
watumie fursa hiyo kujiletea maendeleo halali na kushirikiana na vyombo vya
ulinzi na usalama kuwafichua wahalifu wote.
Maadhimisho ya siku
ya uhuru wa Tanganyika yanafanyika kitaifa mkoani Dodoma huku Rais wa Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania John Magufuli akitajwa kuwa mgeni rasmi.
Comments
Post a Comment