KARDINALI PENGO APONGEZA JUHUDI ZA ASKOFU SANGU
n Na Joachim Mahona, Shinyanga.
ASKOFU
Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki Dar-es-salaam Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo
amepongeza juhudi mbalimbali zinazofanywa na Askofu wa Jimbo Katoliki Shinyanga
Mhashamu Liberatus Sangu za kulistawisha Jimbo na kutoa huduma mbalimbali za
kijamii jimboni humo.
Akizungumza
mara baada ya kuongoza misa takatifu ya dominika ya kwanza ya majilio katika
Kanisa Kuu la Mama Mwenye Huruma Ngokolo mjini Shinyanga wakati wa kuhitimisha
ziara yake ya siku nne aliyoifanya jimboni Shinyanga, Kardinali Pengo
amebainisha kuwa amepata faraja kubwa baada ya kutembelea miradi mbalimbali na
kuona jinsi Askofu Sangu anavyofanya juhudi kubwa za kulistawisha Jimbo kwa
kushirikiana na mapadri na waamini kwa kipindi kifupi tu cha miaka miwili tangu
aanze utume wake.
“Narudi
Dar-es-Salaam nikiwa naamini kuwa Jimbo hili limepiga hatua kubwa katika hali
ya kushangaza, nilikuwa na wasiwasi wakati wa kumwekea mikono siku ile
tuliyokuwa tukimweka wakfu kuwa Askofu wa Shinyanga. Lakini kwa sasa
nimefarijika sana kuona akifanya juhudi mbalimbali za kulistawisha Jimbo hili,”
Amesema.
Kardinali
Pengo ametumia nafasi hiyo kuwataka mapadri wa Jimbo Katoliki Shinyanga kuwa na
umoja na kuendelea kushirikiana na Askofu wao ili kazi anazozifanya ziwe za
mafanikio.
Katika
hatua nyingine Kardinali Pengo amemuomba Askofu Sangu kuhakikisha anafanya
juhudi za kuongeza idadi ya parokia mpya ili Jimbo liwe na parokia nyingi zaidi
na kwa kuanza aanze na malengo ya kuwa na parokia 75 kwani kwa sasa Jimbo
lina parokia 32 tu.
“Mimi
wakati naanza kufanya utume katika Jimbo Kuu Katoliki Dar-es-salaam mwaka 1992,
nilikuta kukiwa na parokia ishirini tu (20), lakini niliwatangazia waamini wa
Dar-es salaam kuwa lazima tumwongezee wachumba Kristo, maana Kanisa ni mchumba
wa Kristo. Kwa hiyo watu walihamasika mpaka sasa tumefanya juhudi na kufikisha
parokia 107. Kwa hiyo baba Sangu jitahidi kuongeza parokia nyingi zaidi ya
ulizonazo hivi sasa na ikiwezekana ujiwekee malengo ya kawaida ya kufikia
parokia 75.”
Kardinali
Pengo pia amepongeza wazo la Askofu Sangu la kuanzisha kituo cha kulelea watoto
yatima kiitwacho (Bishop Sangu Orphanage Centre) kilichopo katika eneo la
Uzunguni mjini Shinyanga. Hatua ambayo imeonesha upendo na ubinadamu kwa watoto
hao ambao ni miongoni mwa makundi yaliyoko katika dhiki kubwa na yaliyosahauliwa.
Naye
Askofu Sangu amemshukuru Kardinali Pengo kwa ukarimu uliouonyesha kwa kukubali
kulitembelea Jimbo Katoliki Shinyanga katika ziara ambayo aliitaja kuwa
imewajenga waamini kiimani. Ametumia nafasi hiyo kumwalika tena katika
uzinduzi wa Jubilei ya miaka 25 ya parokia ya Kanisa Kuu la Mama Mwenye Huruma
Ngokolo na Jubilei yake ya miaka 25 ya upadri. Uzinduzi ambao unatarajiwa
kufanyika mwezi Agosti mwaka 2018.
Ziara
ya Kardinali Pengo ya siku 4 katika Jimbo Katoliki Shinyanga ilikuwa mwaliko
maalum aliopewa na Askofu Liberatus Sangu ambayo pamoja na mambo mengine
ilikuwa na lengo la kuwaimarisha kiimani waamini, kudumisha umoja wa Kanisa na
kujenga mahusiano kati ya majimbo mawili ya Shinyanga na Jimbo Kuu
Dar-es-salaam.
Akiwa
katika ziara hiyo jimboni Shinyanga, Kardinali Pengo alifanya shughuli
mbalimbali za kuweka mawe ya msingi na kubariki mahali ambapo patajengwa nyumba
ya mapadri katika parokia teule ya Lubaga, jengo la kituo cha kulelea watoto
yatima ambacho kinatarajiwa kuanzishwa na Askofu Sangu katika eneo la Uzunguni
mtaa wa Mitimirefu yalipokuwa makazi ya aliyekuwa Askofu wa tatu wa Jimbo
Katoliki Shinyanga hayati Aloysius Balina, jengo la hosteli mpya za
mapadri zinazoendelea kujengwa katika eneo la Ngokolo mitumbani mjini
Shinyanga, jengo la ofisi mpya za parokia zinazoendelea kujengwa katika
Kanisa Kuu la Mama Mwenye Huruma Ngokolo, kubariki na kufungua kikanisa cha
kuabudia Ekaristi takatifu katika parokia ya Ngokolo pamoja na kuwapa komunyo
ya kwanza waamini wapatao 222 katika adhimisho la misa takatifu Dominika ya
kwanza ya Majilio iliyofanyika katika Kanisa Kuu la Ngokolo Desemba 3, 2017.
Comments
Post a Comment