UISHINI UTAKATIFU KABLA YA KIFO-ASK MSONGANZILA

n Na Veronica Modest, Musoma

ASKOFU wa Jimbo Katoliki Musoma Mhashamu Michael Msonganzila amewakumbusha waamini wa Kanisa hilo, kuhakikisha wanajiweka katika maisha ya Utakatifu kabla ya kufariki dunia kwa kuwa mchakato wa kutangazwa mtakatifu ni wa muda mrefu. 
Askofu Msonganzila ameyasema hayo katika Misa Takatifu ya kuweka nadhiri za kwanza kwa masista 9 wa shirika la Moyo Safi wa Bikira Maria Afrika, jubilei ya miaka 25 kwa masista wawili na jubilei ya miaka 50 ya utawa kwa sista mmoja, Misa iliyofanyika katika Kanisa la Novisiati lililopo parokia ya Nyamiongo jimboni humo.
Amesema kuwa waamini wengi wamekuwa wakisubiri kutangazwa watakatifu baada ya kufariki kitendo ambacho kimekuwa kikichukua muda mrefu, hivyo ni vyema kila mkristo akahakikisha anaishi maisha ya unyenyekevu, upendo, utii na usafi wa moyo kabla ya kusubiri mchakato wa kutangazwa kuwa mtakatifu. 
Pia amewapongeza watawa wote kwa hatua yao ya utume ambapo amewaomba waliotimiza miaka 25 na 50 kusimulia maisha na changamoto walizopitia, lakini pia kutokusahau kusimulia mambo makuu ambayo Mwenyezi Mungu amewatendea katika uhai wao.
Kwa upande wake, Mama Mkuu wa shirika hilo Sista Maria Lucy Magumba amewapongeza watawa hao walioweka nadhiri zao za kwanza pamoja na waliotimiza jubilei ya miaka 25 na 50 kwa kufikia hatua hiyo, licha ya changamoto nyingi ambazo wamepitia. 
Nao watawa walioweka nadhiri za kwanza wamemshukuru Mungu kwa kuwafikisha katika siku hiyo, kwa kuwa walianza wengi lakini kutokana na changamoto mbalimbali wengine hawakufika katika safari yao ambapo wameahidi kumtumikia Mungu katika maisha yao yote.


Comments

Popular posts from this blog

SALA YA ASUBUHI:SALI HIVI..

Ujio wa Wamisionari wa Kwanza Tanzania Bara (2)

HISTORIA YA SHEREHE YA MOYO MTAKATIFU WA YESU